2017-05-26 14:35:00

Ujumbe wa Papa Francisko wa Siku ya 51 ya Upashanaji Habari Duniani


Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni, inayoadhimishwa Jumapili tarehe 28 Mei 2017 ni Siku ambayo pia Mama Kanisa anaadhimisha Siku ya 51 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni ambayo kwa mwaka huu inaongozwa na kauli mbiu “Usiogope, maana mimi ni pamoja nawe” kutangaza matumaini na imani katika nyakati hizi. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake anasema, maendeleo ya sayansi na teknolojia katika tasnia ya mawasiliano yamewawezesha watu wengi zaidi kupata na kusambaza habari kwa haraka sana.

Habari hizi zinaweza kuwa za kweli au za uwongo; zinaweza kuwa ni njema au mbaya, hapa kila mtu ana uamuzi wa kusuka au kunyoa! Lakini, wadau wa tasnia ya mawasiliano wanayo dhamana ya kuhakikisha kwamba, wanatoa habari sahihi na kweli ili kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa mawasiliano yanayosaidia kudumisha utamaduni wa watu kukutana, ili kuangalia ukweli wa mambo kwa imani na matumaini! Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa Siku ya Upashanaji Habari Ulimwenguni anakazia mambo makuu matatu: Habari njema; umuhimu wa kuwa na matumaini katika Ufalme wa Mungu na mwishoni ni juu ya mwelekeo wa Roho Mtakatifu!

Baba Mtakatifu anasema, kuna haja ya kuondokana na taarifa zinazowajengea watu hofu kwa kuwalisha habari mbaya kuhusu: vita, vitendo vya kigaidi na kashfa zinazotawala katika maisha ya watu sehemu mbali mbali za dunia, mambo yanayoonesha udhaifu na mapungufu ya binadamu! Ni wazi kwamba, taarifa za mateso na mahangaiko ya binadamu inapaswa kushughulikiwa kwa umakini mkubwa. Watu wana haki ya kupata na kusikia habari njema badala ya mwelekeo wa sasa wa kutaka kuchezea hisia za watu kiasi cha kuwajengea hali ya kukata na kujikatia tamaa. Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa kujikita katika mawasiliano yaliyo wazi, kweli na yanayofumbatwa katika kipaji cha ubunifu ili kutengeneza habari nzuri!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, maisha ya binadamu ni historia inayopaswa kusimuliwa kwa umakini mkubwa kwa kuchagua mambo msingi na yenye maana, ili hatimaye kusoma matukio haya kwa miwani sahihi! Kwa Wakristo miwani sahihi ni Injili ya Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai! Huu ndio mwanzo wa Habari Njema kama anavyosimulia Mwinjili Marko! Lakini Yesu Kristo mwenyewe ndiye Habari Njema anayesimuliwa kwa kina na mapana katika Agano Jipya. Yesu ni kiini cha Habari Njema, kwani amateswa, akafa na kufufuka ili kumshirikisha mwanadamu upendo wa Baba yake wa mbinguni, anayewapenda na kuwajali watoto wake walioumbwa kwa sura na mfano wake.

Yesu ni kielelezo makini cha mateso na mahangaiko ya binadamu, ndani yake giza na mauti vinakuwa ni fursa ya umoja na Kristo ambaye ni chemchemi ya Mwanga, Maisha na Matumaini kwa wale wote waliokata tamaa! Ni chemchemi ya matumaini yasiyodanganya kwa sababu upendo wa Mungu tayari umekwisha kumiminwa nyoyoni mwa waja wake, ili kuchipusha maisha mapya na kukuza mbegu iliyoanguka ardhini. Kumbe, katika historia, dunia inakuwa ni mahali pa habari njema inayojikita katika upendo unaopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Yesu Kristo aliwapatia wafuasi wake miwani sahihi ya kuweza kuangalia matukio ya ulimwengu kwa njia ya Ufalme wa mbinguni unaosimikwa katika hali ya unyenyekevu; unaojikita katika huruma inayosikiliza kwa makini pamoja na kutoa uhuru wa kuupokea na kuufanyia rejea mintarafu Fumbo la Pasaka, ambamo Msalaba unakuwa ni chombo cha utekelezaji wa wokovu wa Mungu kwa binadamu badala ya  kuwani chombo cha uadui. Msalaba unaonesha udhaifu wa binadamu, lakini unafumbata upendo wa hali ya juu kabisa kutoka kwa Mwenyezi Mungu anayetenda kazi kati ya watu wake. Waamini wanakumbushwa kwamba, Ufalme wa Mungu uko kati yao kama mbegu iliyofichama lakini inaendelea kukua katika hali ya ukimya, inaweza kuonekana tu na wale wenye miwani angavu ya Roho Mtakatifu, kiasi kwamba, hakuna hata mtu mmoja anayeweza kuwapoka furaha ya Ufalme wa Mungu hata kama daima magugu yataendelea kuwepo!

Matumaini yanayofumbatwa katika Habari Njema ambayo ni Yesu Kristo Mwenyewe yanawawezesha waamini kuwa na mwelekeo mpana zaidi wa kutafakari Liturujia ya Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni, anayewakirimia waja wake matumaini kwa kuinua ubinadamu wao hadi mbinguni ili kuwawezesha kuwa na uhuru kamili na ujasiri wa kuweza kupaingia patakatifu kwa Damu Azizi ya Yesu, njia mpya na hai iliyoanzishwa na Kristo Yesu yaani kwa njia ya Mwili wake. Kwa nguvu ya Roho Mtakatifu anasema Baba Mtakatifu, waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanaweza kuwa ni mashuhuda na watangazaji wa ubinadamu mpya, uliokombolewa hadi miisho ya dunia.

Matumaini ya mbegu ya Ufalme wa Mungu na mantiki ya Fumbo la Pasaka ni njia muafaka ya kutekeleza dhamana na wajibu wa mawasiliano katika ulimwengu mamboleo unaofumbatwa katika ushawishi kwani kuna uwezekano wa kutambua na kuangaza habari njema iliyoko katika uhalisia wa kila historia na sura ya binadamu! Roho Mtakatifu awawezeshe watu wote kung’amua kile kinachotendeka kati ya Mwenyezi Mungu na binadamu kwani bado anaendelea kutekeleza historia ya wokovu inayofumbatwa katika matumaini yanayobubujika kutoka kwa Roho Mtakatifu Mfariji. Matumaini yanaendelea kujificha katika madonda ya maisha ya mwanadamu, lakini yanapyaishwa daima kwa kusoma Habari Njema ambayo ni Injili iliyoendelea kuandikwa kwa maisha ya watakatifu na watu ambao wamekuwa kweli ni kielelezo cha upendo wa Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko, mwishoni mwa ujumbe wake wa Siku ya 51 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni, anawaomba waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumwachia nafasi Roho Mtakatifu anayependikiza mbegu ya Ufalme wa Mungu kwa njia mbali mbali; kwa wale wanaoongozwa na Habari Njema katika historia ya maisha, wao wanakuwa kama taa katika giza nene; wanayaangazia mapambano na kufungua mielekeo mingine imani na matumaini!

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.