2017-05-26 16:32:00

Papa Francisko: Zingatieni kumbu kumbu endelevu, sala na utume!


Wakristo wanakumbushwa kwamba, wako duniani kwa ajili ya kumtangaza na kumshuhudia Kristo, lakini wanapaswa kutambua kwamba, hapa duniani ni mahujaji na wala hawana makazi ya kudumu, bali wajitahidi kujielekeza zaidi kwa mambo ya mbinguni. Yesu anawakumbusha wafuasi wake kwamba, anawatangulia Galilaya, huko ndiko watakakakokutana naye, ili kumtambua na kushiriki katika furaha yake. Kila mwamini anayo Galilaya yake ya kwanza katika maisha, siku ile alipokutana na Kristo Yesu. Ili kuwa kweli mwamini bora, kuna haja ya kuwa na kumbu kumbu endelevu ya siku ile ya kwanza ya kukutana na Yesu pamoja na mwendelezo wake. Hii ni neema ya kumbu kumbu inayomwezesha mwamini kuwa na uhakika wa usalama wa maisha yake wakati wa majaribu!

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko; Ijumaa tarehe 26 Mei 2017 katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican. Baba Mtakatifu anawahimiza waamini kudumu katika maisha ya sala kama njia ya kuungana na Kristo Yesu aliyelipa deni la dhambi za binadamu kwa njia ya Fumbo la Msalaba. Waamini wawe na ujasiri wa kuomba neema ya kumtafakari Yesu, ili kujenga mahusiano mema naye, ili hatimaye, kushiriki katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko.

Baba Mtakatifu anasema, hii inatokana na ukweli kwamba, binadamu amekombolewa  kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, ili hatimaye, kuweza kuungana naye katika maisha ya uzima wa milele mbinguni! Mambo makuu matatu yanaendelea kukaziwa na Baba Mtakatifu  yaani: kumbu kumbu endelevu, sala na utume wa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyewatangulia Galilaya na hatimaye kupaa mbinguni, kuume kwa Baba wa milele! Huko Yesu anaendelea kuwaombea waja wake. Waamini wahakikishe kwamba, wanashiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa wa kutangaza na kumshuhudia Kristo Mfufuka kwa njia ya mifano bora ya maisha yenye mvuto na mashiko! Utume wa Kanisa unasimikwa katika matendo yanayodhihirisha furaha ya Injili, huduma makini, sala na tafakari ya Neno la Mungu. Wakristo daima wawe ni mashuhuda wa furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu; furaha ambayo kamwe hakuna mtu anayeweza kuwapokonya kutoka katika sakafu ya nyoyo zao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.