2017-05-26 15:45:00

Papa Francisko: Yesu ni chemchemi ya faraja, imani na matumaini!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 27 Mei 2017 anafanya hija ya kichungaji Jimbo kuu la Genova, Kaskazini mwa Italia na anatarajia kwa namna ya pekee kwenda kuwatembelea na kuwafariji watoto waliolazwa kwenye hospitali ya ya Watoto ya “Giannina Gaslini”. Baba Mtakatifu ametanguliza shukrani zake za dhati kwa kuwapigia simu watoto waliolazwa kwenye Hospitali ya “Giannina Gaslini” kupitia Kituo cha “Radio Fra le Note” kilichoanzishwa na Padre Roberto Fiscer, kinachotoa kipindi maalum kwa watoto wagonjwa kila Jumatano.

Baba Mtakatifu amechukua fursa hii kuwatakia heri na baraka kwa matumaini ya kukutana na kuzungumza nao pamoja na wazazi na walezi wao, Jumamosi wakati anapotembelea Jimbo kuu la Genova. Anasema, anapenda kukaa nao walau kidogo, ili aweze kuwasikiliza na kuwapatia faraja inayotoka kwa Kristo Yesu ambaye daima amekuwa karibu na waja wake, hasa wale wanaoteseka kwa magonjwa. Yesu daima ni chemchemi ya imani na matumaini. Baba Mtakatifu anasema, tangu wakati huu anaendelea kusali kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea. Anawaomba watoto waliolazwa kwenye Hospitali ya “Giannina Gaslini” kumkumbuka na kumwombea katika maisha na utume wake. Baada ya ujumbe, huu, Baba Mtakatifu na watoto waliokuwa wanamsikiliza mubashara wamesali pamoja Salam Maria.

Padre Aldo Campone, mhudumu wa maisha ya kiroho kwenye Hospitali ya“Giannina Gaslini” katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, nia ya Baba Mtakatifu Francisko kutembelea watoto wagonjwa hospitalini hapo ni kielelezo cha uwepo wa karibu wa Kanisa katika huduma ya upendo kwa wagonjwa, lakini kwa namna ya pekee watoto wagonjwa. Huu ni ushuhuda wa huruma na upendo wa Mungu unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha, licha ya dawa na huduma mbali mbali wanazopata watoto hawa, lakini uwepo wa Baba Mtakatifu ni ushuhuda wa faraja na matumaini; ni kielelezo cha udugu na mshikamano kwa wale wanaoteseka kutokana na magonjwa!

Padre Aldo Campone anasema, uwepo na huduma yake hospitalini hapo miongoni mwa watoto wagonjwa ni hija ya toba na wongofu wa ndani inayopaswa kutekelezwa kila siku ya maisha! Si rahisi sana kuweza kukubali mpango wa Mungu katika maisha ya watoto hawa wadogo. Kumbe, mateso na mahangaiko ya binadamu yanabaki kuwa ni fumbo kubwa mbele ya binadamu. Huduma kubwa anayoitoa hospitalini hapo ni sala kama kielelezo cha umoja na mshikamano wa upendo na udugu.

Ni uwepo unaomwilishwa zaidi katika kusikiliza kilio na mahangaiko ya watoto hawa hata pengine bila ya kuwa na majibu muafaka ya shida na mahangaiko yao ya ndani! Hospitali hii inawahudumia watoto kutoka katika mataifa 90, watu wa kila kabila, lugha na jamaa; watu wanaoamini dini mbali mbali! Huduma hii ni sehemu ya majadiliano ya kidini yanayofumbatwa katika huduma ya upendo isiyomtenga mtu awaye yote! Mapadre wanaohudumia hospitalini ni ushuhuda wa faraja na neema kutoka kwa Kristo Yesu aliyeonesha upendeleo wa pekee kwa wagonjwa, akawapatia tiba ya mwili na kuwaondolea dhambi zao, tiba muafaka ya maisha ya kiroho.

Padre Aldo Campone anapenda kuchukua fursa hii kumshukuru Baba Mtakatifu Francisko ambaye katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro ameonesha kuwa ni shuhuda na chombo cha huruma ya Mungu kwa wagonjwa, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Baba Mtakatifu atashuhudia mateso na mahangaiko ya watoto wagonjwa; wazazi na walezi wanaoteseka na watoto wao, kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria chini ya Msalaba kwa kushuhudia mateso na hatimaye, kifo cha Mwanaye mpendwa Yesu Kristo! Hospitalini kuna wahudumu wa afya, kuna watoto wagonjwa na wazazi pamoja na walezi wao! Wote hawa wanahitaji kuonjeshwa huruma na faraja ya Mama Kanisa ili waweze kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.