2017-05-26 16:07:00

Askofu Angelo De Donatis ateuliwa kuwa Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma


Baba Mtakatifu Francisko ameridhia ombi la kung’atuka kutoka madarakani lililowasilishwa kwake na Kardinali Agostino Vallini kama Makamu wa Askofu, Jimbo kuu la Roma. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu amemteua Askofu Msaidizi Angelo De Donatis wa Jimbo Kuu la Roma kuwa Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma na kumpandisha hadhi kuwa ni Askofu mkuu. Askofu mkuu  mteule Angelo De Donatis alizaliwa kunako tarehe 4 Januari 1954 huko Casarano, Jimbo Katoliki la Nardo-Gallipoli. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, kunako tarehe 12 Aprili 1980 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre na kuanzia tarehe 28 Novemba akahamia Jimbo kuu la Roma. Tangu wakati huo ametekeleza utume wake kama Paroko usu, mwalimu wa dini shuleni; Afisa katika Sekretarieti ya Jimbo kuu la Roma; Mtunza nyaraka wa Baraza la Makardinali; Mkurugenzi wa Ofisi ya Wakleri, Jimbo kuu la Roma; Baba wa maisha ya kiroho, Seminari kuu ya Jimbo kuu la Roma.

Kuanzia mwaka 2003 akateuliwa kuwa Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Marko,  Mwinjili na Msaidizi wa Chama cha ndugu na wazazi wa Wakleri Jimbo kuu la Roma. Kunako mwaka 2014 akateuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuongoza mafungo ya Kipindi cha Kwaresima kwa Baba Mtakatifu Francisko na waandamizi wake kuu. Tarehe 14 Septemba 2015 akateuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Roma.

Yafuatayo ni mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati alipokuwa anamweka wakfu Askofu mkuu mteule Angelo De Donatis wa Jimbo Kuu la Roma. Yesu Kristo katika utekelezaji wa utume wake hapa duniani aliwachagua Mitume pamoja na waandamizi wao ili kuendeleza mchakato wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa watu wote, wakiwa chini ya mchungaji mmoja pamoja na kuendelea kuwatakatifuza, kuwafundisha na kuwaongoza kuelekea kwenye uzima wa milele. Dhamana hii imeendelezwa katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya Sakramenti ya Daraja takatifu, kielelezo makini cha uwepo endelevu wa Kristo katika Kanisa lake hadi nyakati hizi.

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 9 Novemba 2015 wakati alipokuwa anamweka wakfu Askofu msaidizi Angelo De Donatis, Ibada ambayo imeadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano sanjari na siku kuu ya kutabarukiwa kwa Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano. Baba Mtakatifu alikuwa amezungukwa na umati mkubwa wa Maaskofu na Mapadre kutoka Jimbo kuu la Roma, kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo Kuhani mkuu kati ya watu wake.

Kwa njia ya Maaskofu, Yesu Kristo anaendelea kuwatangazia watu wa mataifa Habari Njema ya Wokovu; kuwatakatifuza watu kwa njia ya maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa pamoja na kupata watoto wapya wa Kanisa; mambo yanayopaswa kujionesha katika hekima na unyenyekevu wa Askofu anayewaongoza watu wake kuelekea kwenye furaha ya uzima wa milele. Huu ni mwaliko kwa Familia ya Mungu Jimbo kuu la Roma kumpokea Askofu mpya miongoni wa urika wa maaskofu, kwa kumpatia heshima anayostahili kama mtumishi wa Kristo na mgawaji wa mafumbo ya Kanisa, ambayo anapaswa kuyatolea ushuhuda wa maisha.

Baba Mtakatifu amemkumbusha Askofu Angelo De Donatis kwamba, ameteuliwa kutoka miongoni mwa watu kwa ajili ya mambo yamhusuyo Mungu; kwa ajili ya huduma kadiri ya mfano wa Kristo mchungaji mwema na wala si kwa ajili ya kuwatala watu. Amemtaka kutangaza na kushuhudia Injili na Mafundisho ya Kanisa. Mahubiri yawe ni chemchemi ya neema kwa watu wa Mungu, ili waweze kuwa wema na watakatifu zaidi. Awe ni mchungaji na mlezi mwema wa Mapadre na Majandokasisi pamoja na kuendelea kuonesha upendo kwa waamini wote, hususan maskini, wagonjwa na wote wanaohitaji msaada wa Kanisa.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini wa Jimbo kuu la Roma kuonesha ushirikiano mkubwa kwa Askofu msaidizi De Donatis ambaye atapaswa kuwasikiliza kwa makini na katika hali ya uvumilivu sanjari na kuendeleza majadiliano ya kidini na kiekumene. Awe ni mfano wa ukarimu wa Kanisa la Roma, kwa kuwasaidia maskini na wote wanaohitaji msaada wa hali na mali. Kanisa katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu, Askofu msaidizi De Donatis anachangamotishwa na Baba Mtakatifu kuhakikisha kwamba, anakuwa kweli mtu wa huruma, kwa kuwafundisha wengine njia inayowaelekeza kwenye huruma bila kubagua. Awalinde na kuwahudumia waamini kwa kufuata mfano wa Yesu Kristo: Mwalimu, Kuhani mkuu na Mchungaji mkuu na kwa njia ya Roho Mtakatifu analijalia Kanisa maisha mapya pamoja na kuwaimarisha viongozi wa Kanisa licha ya udhaifu wao wa kibinadamu. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu anamtaka Askofu msaidizi De Donatis kuwa mlinzi na mtetezi wa familia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.