2017-05-25 14:43:00

Siku kuu ya Kupaa Bwana mbinguni, alama ya matumaini!


Yesu alipaa mbinguni, amekaa kuume kwa Mungu Baba Mwenyezi. Toka huko atakuja kuwahukumu wazima na wafu! Lakini, Yesu kabla ya kupaa mbinguni aliwaambia mitume wake ”Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na la Mwana na la Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi”. Kumbe, uinjilishaji ni dhamana na utume endelevu ambao unapaswa kutekelezwa na Wakristo wote, kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu bado anaendelea kuwa pamoja na wafuasi wake hadi utimilifu wa dahali. Huu ni uwepo unaofariji na kutia hamasa katika uinjilishaji!

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu wakati wa maadhimisho ya Siku kuu ya Kupaa Bwana, Mbinguni, yaani Siku arobaini baada ya Ufufuko wa Kristo, tarehe 25 Mei 2017, Jimboni Bata, huko Equatorial Guinea sanjari na Jubilei ya miaka 40 tangu Askofu Juan Matogo Oyama alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre na Miaka 25 tangu alipowekwa wakfu kuwa Askofu. Ameikumbusha familia ya Mungu Jimboni Bata kwamba, Kanisa kwa asili, dhamana na utume wake ni kuinjilisha, changamoto iliyovaliwa njuga nchini na Wakapuchini kunako mwaka 1645 na baadaye kufuatiwa na Mashirika mbali mbali ya kitawa na kazi za kitume, yakiwa na dhamana ya kuwaonesha watu wa Mungu wokovu unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu.

Kanisa linawashukuru na kuwapongeza wale wote waliojisadaka bila ya kujiachia kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kiasi hata cha kuweka msingi wa Kanisa mahalia nchini humo. Tangu mwanzo, Yesu aliwataka wafuasi wake kuwa ni mashuhuda wa mateso, kifo na ufufuko wake katika Uyahudi wote na Samaria, na hata mwisho wa nchi, mwaliko na changamoto ya kuwa kweli ni mashuhuda wenye mvuto na mashiko wanaosikilizwa kwa makini na walimwengu mamboleo.

Dhamana ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu ni kwa Wakristo wote, wanaopaswa daima kuwa ni mwanga wa mataifa na chumvi ya dunia dhidi ya: biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya; wizi na ufisadi wa mali ya umma; imani za kishirikina; kinzani na mipasuko ya kifamilia; ukabila usiokuwa na tija wala mvuto kwa ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu katika ujumla wake. Waamini wawe ni mwanga na chumvi tayari kuleta mwelekeo mpya kwa wale wanaotaka kuvuruga imani kwa kupandika ndago dhidi ya imani.

Waamini walei wanapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wao ili kuweza kuyatakatifuza malimwengu, ili hatimaye, dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi, kwa njia ya ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo. Lengo ni kuwaonesha watu njia itakayowasaidia kumpenda na kumtumikia Mungu katika maisha yao! Waamini wawe ni mwanga na chumvi ya dunia katika masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijami, daima wakitambua kwamba, wao ni mabalozi wema wa Kristo, ili kweli familia ya Mungu Barani Afrika iweze kuonja ladha ya utakatifu wa maisha unaobubujika kutoka katika Injili ya Kristo.

Waamini wakuze na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kujenga jamii inayosimikwa katika misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu! Watambue kwamba, wao ni wadau wakuu wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu kwa nyakati hizi. Huu ni ufalme unaofumbatwa katika upendo, ukweli, haki na amani changamoto kubwa kwa Wakristo wote. Waamini wanapaswa kuwa kweli ni mashuhuda wa Yesu anayeishi na kutenda kazi ndani ya Kanisa na katika nyoyo za watu kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu!

Kila mwamini anahamasishwa na Mama Kanisa kuchangia katika mchakato wa ukuaji wa Ufalme wa Mungu duniani; kwa kuwa ni vyombo vya matumaini kwa maskini, wagonjwa, waliotengwa na kukata tamaa; wawe ni mashuhuda kwa wale wenye kiu ya upendo, uhuru, ukweli na amani, daima wakiendelea kudumu katika Mafundisho ya Mitume, umoja na udugu mambo yaliyoisaidia Jumuiya ya kwanza ya Wakristo kukua na kupanuka hadi miisho ya dunia. Hakuna sababu ya kuwa na woga usiokuwa na mashiko, kwani Kristo Yesu yuko pamoja na waja wake hadi utimilifu wa dahali.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.