2017-05-24 14:04:00

Rais Donald Trump akutana uso kwa uso na Papa Francisko!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 24 Mei 2017 amekutana na kuzungumza na Rais Donald Trump wa Marekani pamoja na ujumbe wake na baadaye amekutana pia na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican. Katika mazungumzo yao, Baba Mtakatifu amepongeza uhusiano mwema uliopo kati ya Vatican na Marekani pamoja na mshikamano unaooneshwa na nchi hizi mbili katika kulinda na kudumisha uhai, uhuru wa kidini na uhuru wa dhamiri.

Ni matumaini ya viongozi hawa wawili kwamba, Serikali ya Marekani itaendelea kushirikiana kwa karibu na Kanisa nchini humo kwa ajili ya huduma kwa familia ya Mungu katika sekta ya afya, elimu na huduma makini kwa wakimbizi na wahamiaji. Baadaye, viongozi hawa wawili wamejielekeza zaidi katika masuala ya kimataifa hasa katika mchakato wa kukuza na kudumisha amani duniani kwa njia ya majadiliano ya kisiasa na kidini katika ukweli na uwazi hususan huko Mashariki ya Kati sanjari na ulinzi kwa Wakristo katika maeneo haya!

Baba Mtakatifu amemzawadia Rais Trump Nyaraka zake kuhusu: Furaha ya upendo ndani ya familia; Amoris laetitia; Furaha ya Injili: Evangelii gaudium pamoja na “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”: Laudato si. Hizi ni nyaraka zinazogusia dira na mwongozo wa utume wa familia, furaha ya Uinjilishaji pamoja na utunzaji bora wa mazingira. Amempatia pia Medali ya tawi la mzeituni alama ya amani pamoja na ujumbe wake wa Siku ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2017.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.