2017-05-24 14:56:00

Papa Francisko asema: Njia ya Emau ni njia ya matumaini ya Kikristo!


Wanafunzi wa Emau walibahatika kuandamana na Yesu katika safari yao ya matumaini ya Kikristo bila kumtambua kwani macho yao yalikuwa yamefumbwa! Lakini, wakamtambua Yesu wakati wa kuumega mkate na hapo hapo akatoweka tena machoni pao! Nao wakaambiana, Je, mioyo yetu haikuwaka ndani yetu pale alipokuwa akizungumza na kufafanua Maandiko Matakatifu? Wanafunzi wa Emau walikuwa na majonzi makubwa mioyoni mwao kwani Fumbo la Msalaba, yaani mateso na kifo cha Kristo Yesu liliwaachia machungu makubwa kwani liliyeyusha matumaini na maisha yao; wakaonekana kushindwa vita hata kabla ya kuianza.

Wanafunzi wa Emau walikuwa wanakuza matumaini ya kibinadamu, kinyume kabisa na mpango wa Mungu. Mapema siku ile ya kwanza ya juma wakaamua kutoroka kutoka Yerusalemu, kwani Pasaka ingekuwa ni siku ya kushangilia kwa kuimba wimbo wa kukombolewa, lakini mambo yalikwenda mrama! Njiani palikuwa ni mahali pa kusimuliana historia ya maisha na utume wa Kanisa; yaani matendo makuu ya Mungu aliyotenda kwa waja wake. Lakini, kufumba na kufumbua wanakutana na Yesu njiani anayewakirimia tiba ya matumaini kwa kusimulia yale yaliyoandikwa juu yake katika Maandiko Matakatifu na utimilifu wake!

Hii ni sehemu ya katekesi iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano, tarehe 24 Mei 2017 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican! Wanafunzi wa Emau waliokuwa wamekata tamaa, kielelezo cha hali ya maisha ya waamini wengi hata leo hii, walianza kuona cheche za matumaini wakati Kristo Yesu alipokuwa anawafafanulia Maandiko Matakatifu! Si rahisi kuweza kuwaona mabingwa wa matumaini katika Biblia, kwani Mwenyezi Mungu anataka kuthaminiwa na kupendwa kutoka katika undani wa mtu na wala si kwa maneno matupu!

Yesu Kristo anasema Baba Mtakatifu, alirudia tena kitendo cha kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na hitimisho la maisha na utume wa Kanisa. Hili ni tukio linalorudiwa pale Mama Kanisa anapoadhimisha Ibada ya Misa Takatifu! Yesu anajimega na kujisadaka kwa ajili ya upendo kwa mwanadamu, kwani hakuna upendo pasi na sadaka inayotolewa kwa wote! Tukio la Yesu kukutana na kuambatana na Wanafunzi wa Emau ni muhtasari wa maisha ya Jumuiya ya Kikristo inayohamasishwa kutoka kifua mbele ili kuwatangazia watu waliokata tamaa Injili ya matumaini.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Mama Kanisa anasikiliza historia ya watu mbali mbali inayobubujika kutoka katika dhamiri za watu binafsi, ili hatimaye, kuwapatia Neno la uzima, ushuhuda wa upendo aminifu na hivyo, moyo wa mwanadamu unarudia tena kuwaka moto wa matumaini! Kila mwamini katika historia ya maisha yake amewahi kukumbana na matatizo na changamoto za maisha, kiasi cha kutembea wakiwa wamesheheni simanzi na majonzi; ni watu waliokuwa wanatembea pasi na kuwa na mwelekeo wala dira sahihi ya maisha, kiasi cha kuona ukuta na giza nene mbele ya maisha yao! Lakini, waamini wanapaswa kukumbuka kwamba, Kristo Yesu daima anaambatana nao katika safari ya maisha yao ya kiroho, licha ya kinzani na mwelekeo tofauti, bado Mwenyezi Mungu anawapenda na kuwathamini waja wake!

Mwenyezi Mungu ni chemchemi ya matumaini ya watu wake. Baba Mtakatifu anawaalika waamini wenye shida, mashaka na mahangaiko ya ndani wakati huu wa Mwezi Mei, kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu ameikumbuka na kuiombea familia ya Mungu nchini China, inapoadhimisha Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Sheshan! Amewatia shime waamini wanaotoka huko Mashariki ya Kati, wanaoendelea kutembea pasi na matumaini kama walivyokuwa wanafunzi wa Emau kutokana na vita, dhuluma na nyanyaso, kutokukata tamaa, bali waendelee kuwa na matumaini thabiti! Bikira Maria msaada wa Wakristo na Kikao cha hekima, awe ni ngao na tunza kwa waamini wote. Amewataka waamini kutoka Ukcraine kusali kwa ajili ya kuombea amani nchini mwao! Siku kuu ya Kupaa Bwana Mbinguni inayoadhimishwa mjini Vatican, Alhamisi tarehe 25 Mei, 2017 lakini kwa Kanisa zima itakuwa ni Jumapili tarehe 28 Mei 2017 iwe ni nafasi ya kuamsha: imani, mapendo na matumaini kati ya watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.