2017-05-24 16:37:00

Kardinali Gualtiero Bassetti ateuliwa kuwa Rais Mpya wa CEI


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Kardinali Gualtiero Bassetti, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Perugia kuwa Rais mpya wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia na hivyo kuchukua nafasi ya Kardinali Angelo Bagnasco anayeng’atuka kutoka madarakani baada ya kumaliza muda wake wa uongozi wa miaka 10 kama Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia.

Uteuzi wa Baba Mtakatifu Francisko umetangazwa rasmi na Kardinali Angelo Bagnasco mara baada ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumatano, tarehe 24 Mei 2017. Itakumbukwa kwamba, Kardinali Gualtiero Bassetti, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Perugia alizaliwa kunako tarehe 7 Aprili 1942 huko Firenze. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, kunako tarehe 29 Juni 1966 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Katika maisha na utume wake, amewahi kuwa Paroko, Gombera na Makamu Askofu wa Jimbo kuu la Firenze. Tarehe 9 Julai 1994 akateuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Massa Marittima-Piombino na kuwekwa wakfu kuwa Askofu tarehe 8 Septemba 1994. Tarehe 21 Novemba 1998 akahamishiwa Jimbo la Arezzo-Cortona-Sansepolcro na kuanza kuwahudumia watu wa Mungu kwa muda wa miaka kumi na moja. 

Tarehe 16 Julai 2009 akateuliwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Perugia- Citta della Pieve. Tarehe 29 Juni 2010 akapewa Pallio Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Tarehe 12 Januari 2014 akateuliwa na Papa Francisko kuwa Kardinali na kuanzia mwaka 2009 hadi mwaka 2014 alikuwa ni Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Italia. Kufuatia uteuzi huu, Kardinali Gualtiero Bassetti, Rais mpya wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia amepokea wingi wa salam za pongezi kutoka kwa Mashirika ya Kitawa na Taasisi mbali mbali pamoja na kumshukuru Kardinali Angelo Bagnasco aliyemaliza muda wake wa uongozi kwa kipindi cha miaka kumi kama Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.