2017-05-23 14:53:00

Yaliyojiri wakati Kardinali Filoni alipokutana na Maaskofu E. Guinea


Maaskofu wamepewa dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Uamuzi wa Baba Mtakatifu Francisko wa kuunda majimbo mawili mapya nchini Equatorial Guinea ni kutaka kusogeza huduma za kichungaji kwa familia ya Mungu, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Maaskofu wanahimizwa kujenga na kudumisha ari na moyo wa kimissionari; umoja, upendo na mshikamano; kwa kutambua kwamba, kama Maaskofu wanapaswa kuonesha ubaba unaofumbatwa katika udugu; umoja na mshikamano na familia ya Mungu katika majimbo husika.

Maaskofu katika utekelezaji wa dhamana na majukumu yao, wajitahidi kuwa na Baraza la Washauri na Baraza la Wakleri; Baraza la shughuli za kichungaji na uchumi. Maaskofu wanapaswa kujisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya majimbo yao mahalia kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko! Haya ni kati ya mambo msingi yaliyotolewa na Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu alipokutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu katoliki Equatorial Guinea, Jumatatu, tarehe 22 Mei 2017.

Maaskofu waendeleze mshikamano na watawa wa Mashirika mbali mbali kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji. Kwa sasa mkazo lazima uelekezwe katika malezi na majiundo ya kipadre na kitawa; katekesi makini na endelevu; huduma bora katika sekta ya afya, elimu na ustawi wa jamii. Katika masuala haya, watawa wa Mashirika mbali mbali wamekuwa na mchango mkubwa kwa familia ya Mungu Barani Afrika. Majiundo makini kwa mapadre yawasaidie kukuza na kudumisha maisha ya kiroho, kiutu, kimaadili na katika shughuli za kichungaji. Ukabila, chuki na kinzani ni mambo ambayo yako nje kabisa ya maisha na utume wa Kanisa, kumbe yanapaswa kushughulikiwa kikamilifu ili kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa familia ya Mungu.

Maaskofu watambue kwamba, wao ni Mababa wa familia ya Mungu katika majimbo yao mahalia; wawe na ujasiri wa kukemea na kuonya pale mambo yanapokwenda mrama; wasaidie kukuza na kudumisha unyofu, utakatifu na sadaka ya Mapadre na watawa wao kwa njia ya mafungo, sala na ibada zinazoonesha umoja na mshikamano wa familia ya Mungu. Maaskofu wajifunge kibwebwe kukuza na kupalilia miito mitakatifu ndani ya Kanisa ili kweli Kanisa liweze kupata wanafamilia bora na makini; mapadre na watawa watakatifu wanaoweza kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Mwongozo wa Malezi ya Wito na Maisha ya Kipadre uliotolewa hivi karibuni unapaswa kuzingatiwa na wote. Ili kuwa na Mapadre wema, watakakatifu na waliokomaa katika maisha na wito wao, kuna haja ya kuwa na majalimu na walezi walioandaliwa vyema kwa elimu, lakini zaidi kwa ushuhuda wa maisha bora zaidi.

Katika maisha na utume wa Kanisa: Vijana na Familia wapewe kipaumbele cha pekee kwa kuzingatia dira na mwongozo unaotolewa na Kanisa. Parokia na vyama vya kitume viwe ni mahali muafaka pa malezi, majiundo na makuzi ya maisha ya kiroho na kimwili kwa familia ya Mungu katika Jimbo husika. Waamini walei washirikishwe kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kwa kupewa malezi na majiundo makini ya awali na endelevu. Kanisa liwe na ujasiri wa kutoka kifua mbele kwenda pembezoni mwa maisha ya watu ili kuwatangazia na kuwashirikisha furaha ya Injili, imani, matumaini, amani, upendo na mshikamano.

Kardinali Fernando Filoni, wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mongomo, amekazia kwa namna ya pekee: umoja, upendo na mshikamano kati ya: maaskofu, wakleri, watawa na waamini walei; ili kukuza na kudumisha ari na mwamko wa kimissionari miongoni mwa familia ya Mungu Equatorial Guinea. Kuna changamoto za uwepo wa madhehebu mbali mbali ya Kikristo nchini mwao; imani za kishirikina, ukabila, upweke, ubinafsi pamoja na kumong’onyoka kwa kanuni maadili na utu wema. Changamoto zote hizi zinapaswa kushughulikiwa kikamilifu katika mwanga wa ukweli na uwazi; kwa kujikita katika ushuhuda wa imani tendaji, ili kuonesha kwamba, kweli Kristo Yesu ndiye mkombozi wa ulimwengu. Maaskofu wanakumbushwa kwamba, wao ni wahudumu wa Neno na Sakramenti za Kanisa; daima wawe tayari kuwatafuta kondoo waliopotea kwa upole, wema, upendo na huruma kama wachungaji wema. Maaskofu wawe ni mashuhuda na vyombo vya kutangaza Habari Njema ya Wokovu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo cha imani tendaji!

Ikumbukwe kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya wokovu na kielelezo cha huruma ya Mungu, kumbe, mchakato wa utangazaji na ushuhuda wa Injili ya Kristo ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga na Wakristo wote. Ili kuweza kutekeleza dhamana na wito wa kimissionari, kuna haja kwa familia ya Mungu kujiaminisha na kwa kujiweka chini ya ulinzi na mwongozo wa Roho Mtakatifu, mhusika mkuu katika azma ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kanisa nchini Equatorial Guinea lazima lijisikie kwamba, lina wajibu wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.