2017-05-23 10:06:00

Wosia wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Maaskofu Katoliki Italia


Baraza la Maaskofu Katoliki Italia limeanza maadhimisho ya mkutano wake wa 70 kwa hotuba elekezi ya Baba Mtakatifu Francisko aliyoitoa Jumatatu, tarehe 22 Mei 2017 kwanza kabisa kwa kumshukuru Kardinali Angelo Bagnasco, ambaye anang’atuka madarakani baada ya kuliongoza Baraza la Maaskofu Katoliki Italia kwa kipindi cha miaka 10. Baba Mtakatifu alipenda kuitumia siku ya kwanza ya mkutano wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia kuwa ni siku ya majadiliano ya kina katika ukweli na uwazi; katika umoja na upendo wa kidugu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu ndani na nje ya Italia.

Ni mkutano wa uchaguzi, ambamo Maaskofu watapendekeza majina matatu na hatimaye, Baba Mtakatifu mwenyewe atateua kati ya majina yaliyopendekezwa na Maaskofu wenyewe. Haya ni mabadiliko makubwa yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko. Baba Mtakatifu anasema, kama hakuna majadiliano katika ukweli, uwazi, upendo na maridhiano, matokeo yake ni majungu ambayo kimsingi si mtaji. Maaskofu wanapaswa kujiaminisha kwa Roho Mtakatifu anayewaonesha dira na mwongozo na hatimaye, kuwapatanisha katika upendo wa kidugu!

Katika hotuba yake ambayo amewapatia Maaskofu kwa maandishi, amewaalika Maaskofu kumwomba Roho Mtakatifu ili aweze kuwajalia mwanga utakaoondoa woga na wasi wasi wao wa ndani kwa kutambua kwamba, wamekombolewa kwa njia ya upendo, changamoto na mwaliko wa kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa upendo wa Mungu kwa watu. Maaskofu waoneshe ujasiri wa kuweza kujisadaka, kujitoa ili kushirikishana, kusikilizana, kufarijiana na kuonesha pia kipaji cha ubunifu katika kutajirishana kwenye urika wao kama Maaskofu. Maaskofu wanapaswa kutembea huku wakiwa wameshikamana ili kusoma alama za nyakati mintarafu jicho na moyo wa Mungu, ili hatimaye, waweze kuwa kweli ni wahudumu wa Injili ya uhai katika ulimwengu mamboleo ambamo maisha yamejeruhiwa sana! Huu ni wakati wa kujadiliana kama Sinodi ili kutoa maamuzi ya pamoja yatakayopyaisha sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa familia ya Mungu nchini Italia.

Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu kuondokana na kinzani pamoja na tabia ya kutaka kujifungia katika ubinafsi hali inayoonesha ukosefu wa uaminifu wao katika amana ya imani! Mwelekeo huu ni hatari sana kuliko hata madhulumu ambayo Kanisa linaweza kutendewa! Kitabu cha Ufunuo ni muhtasari wa matumaini ya Kikristo, mwaliko kwa Maaskofu ni kuwa tayari kumsikiliza Roho Mtakatifu. Kama ilivyokuwa kwa Kanisa la Efeso ambalo liliuacha upendo wake wa kwanza kwa Mungu, sasa linaalikwa kukumbuka ni wapi walipoanguka, ili watubu na kujirekebisha, tayari kumwachia nafasi Kristo Yesu ili aweze kuwaongoza kwa mwanga na Neno lake.

Baba Mtakatifu anasema, pengine kama ilivyokuwa kwa Kanisa la Smirna lililokumbwa kwa dhiki, dhuluma na umaskini, pengine hata Maaskofu nao wanajikuta wakiwa wameelemewa na uchovu, upweke na wasi wasi wa mambo ya mbeleni lakini wakumbuke kwamba, Mwenyezi Mungu anatekeleza mipango yake tofauti kabisa na mawazo ya binadamu! Kumbe, wanaweza kujikatia tamaa na kukumbana na makwazo, lakini jambo la msingi ni kumwachia Mungu nafasi ya kuweza kuwashangaza; waoneshe ile nguvu na uaminifu wa waungama imani, kwani yeye ashindaye yote haya hatapatikana na madhara ya mauti ya pili.

Baba Mtakatifu anasema, kama ilivyokuwa kwa Kanisa la Pergamo, ambako waamini walimezwa sana na malimwengu, kiasi hata cha kumwasi Mwenyezi Mungu, hali hii pia inaweza kujitokeza miongoni mwa Maaskofu kwa kumezwa mno na malimwengu, kiasi hata cha kupindisha maisha ya Kiinjili, kutokana na uchu wa madaraka, mafanikio ya haraka haraka kwa kudhani kwamba, wamekuwa ni wafanyakazi wa masuala jamii ya Kanisa. Hiki ni kishawishi cha kutaka kuwatumikia mabwana wawili, kielelezo makini cha udhaifu wa maisha ya kiroho. Baba Mtakatifu anawaalika Maaskofu kuondokana na mambo yasiyokuwa na tija wala mashiko kwa maisha na utume wao, ili kuweza kuishi kikamilifu chini ya jicho angavu la Kristo Yesu anayejionesha kati ya maelfu ya watu wanaodhalilishwa na kunyanyaswa. Kwa Kristo Yesu, Maaskofu wataweza kukutana na ukweli utakaowaweka huru!

Kanisa la Thiatira lilionywa kutokana na mafundisho potofu yaliyochafua matendo, upendo, imani na huduma kwa watu! Hapa Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu kuangalia hali halisi ya watu wanaowahudumia, ili hatimaye, waweze kuambata mambo msingi ya imani, upendo kwa Mungu na huduma inayotolewa kwa moyo wa furaha na bashasha ili kudumisha umoja na mshikamano na Kristo Yesu nyota ya alfajiri isiyotambua machweo ya jua! Kanisa la Sardi lilikuwa na jina kubwa na mwonekano mzuri wa mambo ya nje, kishawishi ambacho kinaweza kuwavuta hata Maaskofu na kusahau mambo msingi yanayojikita katika ukarimu, utii na uaminifu unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha kwa kuepuka: majivuno, kiburi na uasi na badala yake kujenga urafiki na watu wadogo pamoja na kushirikiana na watu wenye shida; ili kudumisha upendo, kwa kujifunza hekima na busara ya maskini na kufumbata huruma ya Mungu, ili kushiriki katika kutunga kitabu cha maisha.

Baba Mtakatifu anakaza kusema,  kama ilivyokuwa kwa Kanisa la Filadelfia, Maaskofu pia wanapaswa kuwa na subira, tayari kujiachilia katika ukweli pasi na woga wala wasiwasi, ili waweze kuwa ni nguzo thabiti katika sadaka na utume; kwa kujenga na kudumisha ujirani mwema katika hali ya unyenyekevu; kwa kujenga madaraja ya watu kukutana katika tamaduni mbali mbali kwa ajili ya mafao ya wengi, ili kuwa ni washiriki wa Yerusalemu mpya. Kanisa la Laodikia lilikuwa halina msimamo, changamoto ni kuwa wafuasi amini wa Kristo Yesu alijisadaka maisha yake kwa ajili ya kumwokoa mwanadamu; analaani dhambi, lakini anampatia haki mdhambi, mwaliko hapa ni kuchuchumilia neema ya Mungu pasi na kumezwa na malimwengu, kwa kumruhusu Mungu kukaa pamoja nao, ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, udugu na amani! Mwenyezi Mungu anapenda kuwakemea watu wake, ili waweze kutubu, kuongoka na kumrudia tena. Imani, upendo na matumaini yawe ni nyenzo, dira na mwongozo katika hija ya maisha yao, daima wakijiaminisha kwa Roho Mtakatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.