2017-05-23 10:29:00

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia: Vijana, Uchungaji na Uchaguzi mkuu


Kardinali Angelo Bagnasco, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia anayeng’atuka kutoka madarakani baada ya kumaliza muda wake wa uongozi, amemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa sera na mikakati yake ya shughuli za kichungaji: kwa kuambatana, kuongozana na kufuatilia maisha ya familia ya Mungu nchini Italia kwa moyo wa umoja. Hiki ni kipindi mtambuka chenye changamoto, matatizo, fursa na matarajio yake.

Anasema kama Maaskofu hawatakubali kubwagwa chini na mikingamo wala malalamiko yasiyokuwa na tija wala mashiko, kwani wanatambua kwamba, wanatekeleza dhamana na utume ambao unabubujika kutokana na kukutana na Yesu Kristo, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Yeye ni sura ya Kanisa; ni sura ya Jumuiya yenye moyo unaowaka mapendo na huruma anayepata ukuu na utimilifu wake katika huduma ya ukarimu na unyenyekevu!

Maaskofu wanampongeza Baba Mtakatifu ambaye ameendelea kuwa ni shuhuda wa ujasiri wa kitume, njia makini ya kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili katika tamaduni na jamii ya watu mamboleo, ili kweli mwanga wa Kristo uweze kuwaangaza  watu wote! Maadhimisho ya Mkutano mkuu wa 70 wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia unapenda kutoa kipaumbele cha pekee mwelekeo wa shughuli za kichungaji katika kipindi cha miaka kumi ijayo pamoja na maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana itakayofanyika mwezi Oktoba, 2018.

Maaskofu wanataka kujibu maswali, kuwasikiliza na kuwasindikiza vijana wa kizazi kipya katika maisha yao, kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa jamii iliyo bora zaidi; kwa kujikita katika elimu na ushuhuda makini. Kukutana na vijana kunawasaidia Maaskofu kutoa kipaumbele cha pekee kwa Mwenyezi Mungu, ili hatimaye, waweze kufikiri na kutenda katika uhuru unaobubujika kutokana na ukweli! Mkutano mkuu una dhamana ya kuchagua Rais mpya wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia na mwishoni, anamshukuru Baba Mtakatifu kwa kumwamini na kumpatia dhamana ya kuliongoza Baraza la Maaskofu Katoliki Italia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.