2017-05-22 16:21:00

Papa Francisko: Imarisheni vyama vya kitume ili kukoleza imani!


Baba Mtakatifu Francisko alipotembelea Parokia ya Mtakatifu Pier Damiani, Jimbo kuu la Roma, Jumapili tarehe 21 Mei 2017 alipata nafasi ya kukutana na kuzungumza na wazazi wa watoto waliobatizwa hivi karibuni Parokiani hapo. Baba Mtakatifu amewakumbusha kwamba, watoto ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu wanaopaswa kuhudumiwa, kupewa malezi na elimu bora. Wasisahau kuwasindikiza, ili hatimaye, waweze kuwa ni watu wenye furaha! Baba Mtakatifu alipata nafasi pia ya kuzungumza na wanachama wa Ukatekumeni Mpya, kilichoanzishwa takribani miaka 30 iliyopita. Baadhi ya wanajumuiya wake, walitumwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, miaka minane iliyopita ili kusaidia mchakato wa Uinjilishaji mpya. Chama hiki cha kitume kimekuwa na mafanikio makubwa kiasi kwamba, hata idadi ya waamini wanaoshiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa imeongezeka maradufu. Kwa njia ya ushuhuda wa imani, waamini waweweza kukabiliana na changamoto za maisha; wamesaidiwa kuimarisha miito yao yao ndani ya Kanisa!

Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza viongozi wa Kanisa wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma makini kwa familia ya Mungu waliyokabidhiwa na Mama Kanisa. Jumuiya inayosimikwa katika imani, matumaini na mapendo thabiti inakuwa ni chemchemi ya miito mitakatifu, ari na mwamko wa kimissionari. Hii inatokana na ukweli kwamba, neema ya utume inabubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo, inayowakirimia nguvu ya kuwa kweli ni wamissionari. Waamini walei wanahamasishwa kuwa kweli ni wamissionari kwa watu wanaowazunguka kwa kuwasikiliza na kuwapatia huduma: kiroho na kimwili; ushuhuda wenye mvuto na mashiko; chachu ya Uinjilishaji mpya inayokolezwa na Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa.

Waamini walei wawe mstari wa mbele katika kutangaza na kushuhudia Injili; wawe wasikivu kwa Roho Mtakatifu, ili kuruhusu mbegu ya Neno la Mungu iweze kuingia na kuzama katika akili na nyoyo zao! Hapa kinachohitajika ni ushuhuda na wala si wongofu wa shuruti! Kanisa linaweza kukua na kukomaa kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko na wala si kwa njia ya shuruti kama ambavyo aliwahi kusema, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI. Ushuhuda wa Kanisa unafumbatwa katika huduma makini kwa maskini wa kiroho na kimwili.

Katika safari ya maisha ya kiroho, kuna nyakati ambazo mwamini anapata mtikisiko katika maisha na imani yake, lakini wakimtegemea Mwenyezi Mungu wanaweza kuibuka kidedea na kuwa na ujasiri zaidi. Pale waamini wanapokabiliwa na changamoto za maisha na imani, wawe na ujasiri wa kuomba msaada na ushauri kutoka kwa jirani zao. Wakristo ndio waliopewa dhamana ya kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo na wala si malaika, kwani wao dhamana na wajibu wao ni kumsifu, kumtukuza na kumwabudu Mwenyezi Mungu! Amewataka kuwasaidia na kuwaendeleza watoto wao katika  maisha ya kiroho na utu wema, kwani wao ni jeuri na matumaini ya Kanisa la Kristo! Wajitahidi kuwafunda ili hatimaye, waweze kuwa ni wakristo watakatifu na raia wema zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.