2017-05-22 14:23:00

Mkutano mkuu ni muda wa: umoja, kusikilizana, kung'amua na ushuhuda


Shirika la Watawa wa “Divin Maestro” kuanzia tarehe 10 Aprili hadi tarehe 28 Mei 2017 linaadhimisha mkutano mkuu wa tisa wa Shirika unaoongozwa na kauli mbiu “Divai mpya kwenye viriba vipya”. Wajumbe tayari wamemchagua Sr. Micaela Monetti kuwa Mama mkuu wa Shirika. Baba Mtakatifu Francisko amekutana na kuzungumza na wajumbe wa mkutano huu, Jumatatu, tarehe 22 Mei 2019 na kukazia umuhimu wa kujenga na kudumisha umoja; kujitahidi kusoma alama za nyakati; kujenga utamaduni wa kusikiliza; kung’amua ili hatimaye waweze kuwa ni manabii wa furaha na matumaini!

Ili kujenga umoja, watawa hawa hawana budi kuwa wazi kwa Roho Mtakatifu anayewawezesha kujenga umoja katika utofauti na kutembea katika umoja kwa kuthamini tofauti msingi zinazotokana na utume wao katika nchi na tamaduni mbali mbali; ili kuweza kupokea na kuwajibika wa zawadi zilizomo katika maisha yao kwa kukazia: ukarimu; kukosoana kidugu; kuwaheshimu na kuwathamini watawa wanyonge; kwa kukuza na kudumisha ari na moyo wa maisha ya kijumuiya; kwa kuondokana na kinzani na mipasuko ya kijumuiya; wivu na majungu! Watawa wawe na ujasiri wa kuambiana ukweli katika upendo!

Matunda ya umoja wa familia ya Wapaulini yanasimikwa katika msingi wa Don Giacomo Alberione; utume wa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kwa watu wa nyakati hizi mintarafu huduma ya Kiliturujia na kwa Wakleri. Familia hii inajikita katika karama moja kwa ajili ya Uinjilishaji, kila upande ukiendelea kuwa aminifu kwa utambulisho wake, changamoto ni kuendeleza majadiliano na karama za mashirika mengine ili kuondokana na kishawishi cha kutaka kujitafuta wenyewe! Matunda ya umoja yawakumbatie walimwengu wote, kwani Mwenyezi Mungu ni Bwana wa hisitoria na imani ya watu wake; imani inayotenda kazi katika historia, tayari kujibu kilio cha wale wanaotumaini sadaka na majitoleo yao kama watawa!

Baba Mtakatifu anasema, maadhimisho ya Mkutano mkuu ni muda wa kusoma alama za nyakati; kusikilizana kwa makini; kupembua kwa kina na mapana; kuondokana na maamuzi mbele; ni wakati wa kutoka katika ubinafsi ili kuonja ukarimu wa wanashirika wengine; kwa kuwa na akili na moyo wazi, tayari kutembea kwa pamoja kuelekea katika ukweli kamili, utakaowaweka wote huru! Ni wakati muafaka wa kusikiliza; kushirikishana maisha ya kidugu ndani ya jumuiya, ili kutoa na kupokea kutoka kwa wengine, tayari kukua na kukomaa kwa pamoja. Ni wakati wa kukabiliana na changamoto mamboleo zinazojibiwa kwa kujikita katika uaminifu wenye ubunifu na tafiti makini; kwa kusikiliza na kushirikishana, ili kutoa maana halisi ya maisha kwa wanashirika na wale wote wanaokutana nao katika huduma yao!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, ili kuweza kufikia azma hii, kuna haja ya kufanya mang’amuzi, ili kutambua kile ambazo Roho Mtakatifu anakitaka kutoka kwao na kile ambacho wanapaswa kukiacha kwa kuundwa ili kujiunda katika mang’amuzi binafsi na yale ya kijumuiya. Maadhimisho ya Mkutano mkuu ni wakati muafaka wa kujipyaisha na kujiweka chini ya Roho Mtakatifu ili kushiriki utume na unabii wa Kristo, kwa kuonesha upendo kwa Mungu na binadamu; kwa kuwa ni sauti ya Mungu dhidi dhambi na mabaya.

Watawa wanapaswa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya unabii wa furaha inayobubujika kutoka katika undani wao kwa vile wamekutana na Kristo Yesu katika Sala, tafakari ya Neno, katika maisha ya kidugu ndani ya jumuiya; kwa kuwapokea, kuwasaidia na kuwakumbatia maskini; ni furaha inayobubujika kutoka katika undani wao kwa kutambua kwamba, wanapendwa kwa sababu wanapendwa na kusamehewa, changamoto kubwa kwa watu wanaoishi katika ulimwengu mamboleo! Huu ni ushuhuda wa utimilifu wa maisha unaojikita katika furaha; uzuri wa kuishi Injili na kumfuasa Kristo; tayari kutoka kifua mbele kwenda pembezoni mwa jamii kushiriki katika furaha ya Kanisa linaloinjilisha, kwa kutambua kwamba, Yesu ni Habari Njema kwa wote inayofukuzia mbali saratani ya kukata na kukatishwa tamaa.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka watawa kuwa kweli ni manabii na mashuhuda wa matumaini yanayowawajibisha kwani wanaitwa kuwa tayari siku zote kumjibu kila mtu anayewaulizia kuhusu tumaini lililoko ndani mwao! Matumaini ambayo kamwe hayamdanganyi mtu, wala kujikita katika idadi au mafanikio yaliyopatikana kutokana na utume. Matumaini ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya Kikristo kuelekea katika uzima wa milele na kwamba, Kristo Yesu ni tumaini la Wakristo, kumbe, watawa wanaweza kuwa ni manabii wa matumaini, changamoto na mwaliko wa kukuza na kuimarisha wito na maisha yao ya kitawa, ili kuwaamsha walimwengu na kuyaangazia yale yajayo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.