2017-05-20 15:00:00

Siku kuu ya Bikira Maria Msaada wa Wakristo: Siku ya Kuombea China


Siku kuu ya Bikira Maria msaada wa Wakristo inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 24 Mei, ilianzishwa na Papa Pio wa VII kunako mwaka 1815. Huu ulikuwa ni mwaliko kwa waamini kujiaminisha mbele ya Bikira Maria msaada wa Wakristo, ili awasaidie kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Kunako mwaka 2001 Bikira Maria alitangazwa kuwa ni Mama na msimamizi wa Familia ya Mungu nchini China.

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kunako mwaka 2007 akatangaza tarehe 24 Mei ya kila Mwaka kuwa ni Siku ya Kuombea China. Tangu wakati, Kanisa zima linakimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria kwa ajili ya familia ya Mungu nchini China; siku ambayo China pia inaadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria wa Sheshan. Kutokana na mwaliko huu, Askofu mkuu Ludwig Schick kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuungana na Kanisa zima, ili kuombea familia ya Mungu nchini China.

Anasema, majadiliano kati ya China na Vatican yanaendelea vyema,  ili kuhakikisha kwamba, umoja wa Kanisa la Kristo chini ya Khalifa wa Mtakatifu Petro unadumishwa pamoja na Sheria za Kanisa kuhusu uteuzi wa Maaskofu Mahalia kufuata kwa ukamilifu, kwani ndiye aliyepewa dhamana hii kisheria. Kwa njia hii, hata Kanisa Katoliki nchini China linaweza kuendeleza mahusiano na Makanisa mengine mahalia sehemu mbali mbali za dunia.

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, kunako mwaka 2008, alisali na kumwomba Bikira Maria msaada wa Wakristo, msimamizi wa China na Bara la Asia katika ujumla wake kuwainua wale wote ambao wanaendelea kujisadaka usiku na mchana kwa kuamini, kutumaini na kupenda, ili wawe na ujasiri wa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu mbele ya walimwengu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.