2017-05-20 11:30:00

Ijumaa ya huruma ya Mungu: Papa atembelea familia na kubariki nyumba!


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma imekuwa ni fursa makini kwa waamini kumwilisha matendo ya huruma kiroho ambayo kimsingi ni ushauri kwa wenye shaka, kuwafundisha wajinga, kuwaonya wakosefu; kuwafariji wenye huzuni; kusamehe makosa; kuvumilia wasumbufu pamoja na kuwaombea walio hai na wafu. Imekuwa ni nafasi ya kujenga umoja na mshikamano na wale wote wanaojisikia kuwa mbali na Kanisa au kusukumizwa pembezoni mwa maisha na utume wa Kanisa!

Matendo ya huruma kimwili ni: kuwalisha wenye njaa, kuwanywesha wenye kiu; kuwavika walio uchi; kuwakaribisha wageni, kuwatembelea wagonjwa na wafungwa pamoja na kuwazika wafu! Wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Baba Mtakatifu Francisko alijianzishia “Ijumaa ya huruma ya Mungu” muda muafaka wa kutenda tendo la huruma: kiroho na kimwili; utaratibu ambao anaendelea kuutekeleza pale anapopata nafasi!

Ijumaa, tarehe 19 Mei 2017, Baba Mtakatifu Francisko alitembelea Parokia ya “Stella Maris” moja ya Parokia sita zilizoko eneo la Ostia, nje kidogo ya Roma na kukutana na familia zinazoishi katika maeneo haya. Baba Mtakatifu amesalimiana na wanafamilia hawa pamoja na kubariki nyumba zao kama sehemu ya utamaduni wa kipindi cha Pasaka kwa Jimbo kuu la Roma, huku akiwa ameambatana na Padre Plinio Poncina, Paroko wa Parokia ya “Stella Maris”. Waamini wa Parokia hii, walishikwa na mshangao mkubwa walipokutana uso kwa uso na Baba Mtakatifu Francisko aliyekwenda kubariki nyumba zao kama Paroko. Baba Mtakatifu amewaachia zawadi ya Rozari kwa kila familia alimobahatika kupita na kubariki nyumba yao. Waamini wamefurahia sana tukio hili ambalo kwa hakika, limeaacha chapa ya kudumu katika akili na nyoyo za waamini wao! Baba Mtakatifu anasema huruma ya Mungu ni hija ya maisha inayopaswa kumwilishwa kila siku, kwani hapa duniani mwanadamu ni hujaji anayepaswa kuwa kweli ni chombo na shuhuda wa huruma ya Mungu kwa jirani zake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.