2017-05-19 14:08:00

Wananchi tumieni vyema ardhi kama chombo cha uzalishaji na huduma!


Baraza la Maaskofu Katoliki Msumbiji, CEM, linawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema nchini humo kuhakikisha kwamba, wanajikita kikamilifu katika kulinda, kutunza na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote. Haya yamo kwenye Waraka wa kichungaji uliotolewa na Baraza la Maaskofu unaoongozwa na kauli mbiu “Uzao wako nitawapa nchi hii”. Waraka huu ni mwendelezo wa tafakari juu ya Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Ardhi ni chombo cha uzalishaji na huduma kinachopaswa kutumiwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wote wa Msumbiji.

Baraza la Maaskofu Katoliki Msumbiji linasikitika kusema kwamba, tangu mwaka 2000 hadi mwaka 2013, kiasi cha ekari 56 milioni zimeuzwa kwa wageni pamoja na makampuni ya kigeni yanayotafuta maeneo makubwa kwa ajili ya kuwekeza katika sekta ya kilimo ili kukidhi mahitaji ya malighafi ya nishati katika nchi zilizoendelea zaidi duniani. Mashamba haya yameanza kutumika kwa ajili ya kilimo cha nishati uoto hali ambayo imewafanya wawekezaji hawa kuyapata kisogo matatizo na changamoto za wakulima mahalia.

Baraza la Maaskofu Katoliki Msumbiji linakaza kusema, hapa kuna haja ya kuwa na sera, mipango na mifumo ya maendeleo endelevu ya kilimo inayozingatia ukweli na uwazi; ustawi na maendeleo ya wengi, badala ya kujikita katika uchumi unaotafuta faida kubwa, wakati mamilioni ya watu wakiteseka kwa baa la njaa na ukosefu wa uhakika wa usalama chakula nchini Msumbiji. Wananchi wa Msumbiji wana haki ya kumiliki na kuendeleza ardhi kama sehemu muhimu sana ya mtaji katika mchakato wa maendeleo yao. Lakini, tabia ya wananchi kuanza kuuza maeneo makubwa makubwa ya ardhi kwa wawezekaji wa ndani na nje ni hatari katika sera za kilimo ambacho kimsingi ni uti wa mgongo kwa wananchi wengi wa Msumbiji.

Kutokana na maeneo makubwa ya ardhi kupokwa na makampuni makubwa makubwa, kwa sasa  kumeanza kujitokeza kinzani, migogoro na mipasuko ya kijamii kati ya wawekezaji na wananchi ambao wamejikuta hawana tena mahali ya kilimo kwa ajili ya mahitaji yao binafsi na familia zao. Maaskofu wanasema katika Waraka wao wa kichungaji kwamba, kuna haja ya kuwa na uwiano bora zaidi wa uhusiaho na maendeleo kati ya wananchi na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, kwa kuwa na sera za uchumi shirikishi, zinazotoa fursa kwa wananchi kuendelea kufaidika na rasilimali ardhi. Kwa bahati mbaya, Sheria ya ardhi inapindishwa kwa makusudi na wahusika, hali inayopelekea kuwatumbukiza wananchi wengi katika dimbwi la umaskini wa hali na kipato!

Maaskofu wanaendelea kufafanua kwamba, sera na mikakati ya uchumi mamboleo nchini humo ni hatari sana, kwani watu wamegeuzwa kuwa ni walaji wa kupindukia na kwamba, kumekuwepo na kasi kubwa ya kuchuma rasilimali na utajiri wa nchi, ambao kwa bahati mbaya unaishia mikononi mwa baadhi ya matajiri, huku “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi” wakiendelea kuteseka kwa hali ngumu ya uchumi. Maaskofu wanakumbusha kwamba, kilimo ni uti wa magongo wa uchumi wa Msumbiji. Hii inatokana na ukweli kwamba, takribani ya asilimia 70% ya wananchi wote wa Msumbiji wanaishi vijijini. Kumbe, hapa kuna haja ya kuwa na sera makini zinazoheshimu na kuzingatia ekolojia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ikumbukwe kwamba, maji ni sehemu ya haki msingi za binadamu, kumbe kuna haja ya kuhakikisha kwamba, wananchi wengi wa Msumbiji wanapata maji safi na salama, ili kukuza na kudumisha afya bora.

Uvunaji mkubwa wa misitu unaendelea kusababisha madhara makubwa ya tabianchi. Baraza la Maaskofu Katoliki linawataka wawekezaji na wadau mbali mbali wa shughuli za uzalishahji na utoaji wa huduma, kujenga na kudumisha moyo wa upendo na mshimamano wa kidugu unaosimamiwa na kuongozwa na kanuni auini. Lengo ni kuhakikisha kwamba, rasilimali ya nchi iwe ni kwa ajili ya huduma na matumaini ya wananchi wote wa Msumbiji. Uchumi wa nchi hauna budi kusimikwa katika kanuni maadili na utu wema; haki na usawa ili kweli shughuli uzalishaji na huduma ziweze kuwanufaisha wengi.

Baraza la Maaskofu Katoliki Msumbiji katika Waraka wake linaitaka familia ya Mungu nchini humo kuondokana na kishawishi cha uchu wa mali, madaraka na utajiri wa haraka haraka ambao una madhara makubwa kwa ustawi wa watu na maendeleo yao. Sera na mikakati ya kiuchumi haina budi kuzingatia: utu na heshima ya binadamu; haki zake msingi pamoja na kuendelea kuimarisha uchumi mahalia. Wananchi wa Msumbiji hawana budi kuondokana na ukataji ovyo wa miti ili kutoa hifadhi kwa maliasili ya dunia.

Vijana wa kizazi kipya wanapaswa kufundwa kuhusu umuhimu wa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote sanjari na kukazia tunu msingi za maisha ya Kiinjili na utu wema. Lengo ni kuweza kujenga jamii inayosmikwa katika haki, usawa, umoja na udugu. Maaskofu wanawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika maisha na utume kwa Jamii wanamoishi kwa kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa; kwa kuondokana na ukabila usiokuwa na mvuto wala mashiko!

Kanisa nchini Msumbiji litaendelea kujielekeza kutoa mafunzo ya Mafundisho Jamii ya Kanisa ili kila mwamini aweze kutambua, kuthamini na kutekeleza wajibu wake barabara! Mapadre na watawa wawe mstari wa mbele kusimamia misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu! Wawe mstari wa mbele kukemea uwovu, dhuluma na nyanyaso dhidi ya wakulima na wafanyakazi na wawe mstari wa mbele kuchukua hatua pasi na kuchelewa. Wanafunzi wafundwe juu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, tayari kusimama kidete kuzuia uchafuzi wa mazingira unaoendelea kusababisha madhara makubwa kwa watu na mali zao.

Vijana wa kizazi kipya wawe makini kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya Kikristo na Kiafrika na kamwe wasikubali kuwa kama “dodoki” linalokusanya takataka kutoka kila upande wa dunia. Wanasiasa Wakristo na wapenda amani, ustawi na maendeleo ya wengi wanahamasishwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Msumbiji kuhakikisha kwamba, wanajifunza Mafundisho Jamii ya Kanisa na kuyamwilisha katika maisha na vipaumbele vyao. Wasimame kidete kupambana na rushwa, wizi na ufisadi wa mali ya umma.

Msumbiji inapojiandaa kuadhimisha Jubilei ya miaka 50 tangu ilipojiapatia uhuru wake toka kwa Mreno hapo mwaka 2025, Baraza la Maaskofu Katoliki Msumbiji linaiomba Serikali ya Msumbiji kuandaa sera na mikakati makini ya Mapinduzi ya Kilimo nchini humo. Wanasiasa wawe na ujasiri wa kurekebisha makosa na kasoro ili kweli Msumbiji iweze kuwa ni mahali bora zaidi pa kuishi. Familia ya Mungu nchini Msumbiji kweli iwe ni chombo na shuhuda wa misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Mwishoni, Baraza la Maaskofu Katoliki Msumbiji linaiweka familia yote ya Mungu nchini humo chini ya ulinzi na tuna ya Bikira Maria, Mama wa huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.