Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Vatican \ Hotuba

Kardinali Sandri mkazo: Umoja wa Kanisa na ukarimu kwa maskini!

Kardinali Leonardo Sandri amehitimisha ziara yake ya kikazi nchini Australia kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki, amekazia umoja, upendo, mshikamano na huduma kwa maskini, wakimbizi na wahamiaji. - AFP

18/05/2017 07:30

Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki  katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwake, ametumia fursa hii kutembelea Makanisa ya Mashariki yaliyoko nchini Australia ili kukuza na kudumisha majadiliano ya kiekumene; kushirikishana sera mikakati, changamoto na vikwazo vinavyowakabili waamini wa Makanisa ya Mashariki walioko ughaibuni!

Hii ni fursa makini ya kukuza na kudumisha ari na moyo wa kimissionari tayari kuendeleza mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Imekuwa ni nafasi ya kutembelea kwa namna ya pekee, Australia kuanzia tarehe 11 hadi 15 Mei 2017 na huko amekutana, amesali na kuzugumza na waamini, viongozi wa Makanisa na Serikali ya Australia. Amewapongeza wote kwa upendo na mshikamano wanaoendelea kuonesha kwa ajili ya kuwapokea na kuwakirimia wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi huko ughaibuni. Amewatakia wananchi wote wa Australia amani, ustawi, mafao na maendeleo ya wengi.

Ametembelea shule, vyuo na taasisi zinazomilikiwa na kuendeshwa na Makanisa ya Mashariki kwa ajili ya kutoa elimu bora na makini kwa wote, ili hatimaye, vijana hawa wa kizazi kipya waweze kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Wazazi na walezi wametakiwa kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana na wajibu wao ili kuwarithisha watoto wao tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili. Amekazia umuhimu wa vijana kushiriki katika Ibadan a Liturujia takatifu ili kukua na kukomaa kiroho.

Kardinali Leonardo Sandri katika safari yake ya kikazi nchini Australia amekua akiandamana na Askofu mkuu Adolfo Tito Yllana, Balozi wa Vatican nchini Australia. Wameungana na Baba Mtakatifu Francisko  kiroho, katika kuadhimisha kilele cha Jubilei ya Miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima. Amewaweka waamini na watu wote wenye mapenzi mema nchini Australia chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Fatima. Amewataka watawa  kujenda na kudumisha uhusiano wa karibu zaidi na Kristo Yesu, kila mtu akijitahidi kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara! 

Wamewakumbuka Wakristo wanaoteseka kutokana na vita, nyanyaso na madhulumu huko Mashariki ya Kati ili kamwe wasikate tamaa, bali wanendelee kumtegemea Mungu katika maisha yao. Kwa namna ya pekee, waamini wanahamasishwa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu na furaha ya Injili kwa watu wa mataifa! Wakristo kati ya watu wa Mataifa wawe ni mwanga na chumvi ya walimwengu, kwa kuchota uhai wao kutoka kwa Roho Mtakatifu.

Kwa upande wake Askofu mkuu Adolfo Tito Yllana, amewataka waamini kuendelea kuwa ni mashuhuda wa Furaha ya Injili; tunu msingi za maisha ya Kikristo kwa kutambua kwamba, wanapaswa kuwa ni chumvi ya ulimwengu na mwanga wa mataifa. Kwa sasa ni raia wa Australia, lakini makini katika utambulisho wao unaofumbatwa katika Mapokeo ya Makanisa ya Mashariki; lakini kwa pamoja wanaunda Kanisa moja, takatifu, katoliki na la mitume! Waendelee kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake sanjari na kuonesha mshikamano wa dhati na Wakristo wenzao wanaoteseka kwa vita na madhulumu ya kidini kutokana na misimamo mikali ya kiimani huko Mashariki ya Kati. Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki amehitimisha hija yake nchini Australia kwa kuwashukuru na kuwapongeza viongozi wa Serikali ya Australia kwa huduma makini inayotoa kwa wakimbizi na wahamiaji walioko nchini mwao. Amevipongeza na kuvishuruku vyombo vya habari vilivyomwezesha kuwafikia waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kwa wingi zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

18/05/2017 07:30