2017-05-17 14:54:00

TAKUKURU sasa kuwachezesha "Sindimba" wafanyabiashara ya "Kangomba"


Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) itafuatiIia na kubana wezi ndani ya Tasnia ya Korosho ili mkulima apate stahili yake. Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Velentino Mlowola, amesema kuna wizi na udanganyifu mwingi ndani ta Tasnia ya Korosho na hivyo wakati umefika sasa wa wabaya wote kupelekwa mbele ya sheria.  Alikuwa akizungumza hivi karibuni kwenye Mkutano Mkuu wa Wadau wa Tasnia ya Korosho, uliofanyika kwa siku mbili mjini Dodoma ukifunguliwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na kuendeshwa na Mwenyekiti wa Wadau, mzee Hemed Mkali.

“Nimekuzwa na uchumi wa Korosho. Mengine nitakayoyasema hapa nayajua kwa sababu hiyo, si kwa sababu ya kuyasoma vitabuni tu. Tasnia ya Korosho ni miongoni mwa sekta muhimu sana katika uchumi wa Taifa letu. Korosho ndilo zao kuu la biashara katika Mikoa ya Kusini mwa Tanzania. Lakini sekta hii inakabiliwa na changamoto kadhaa zinazokwaza maendeleo ya sekta yenyewe na uchumi wa wananchi wanaozalisha Korosho na pia Mapato ya Serikali ambayo hutumika kugharamia maendeleo ya wananchi na usalama wao. Changamoto zinazoathiri sekta ya Korosho zinahitaji kuingiliwa kati na Serikali ili wananchi wanaozalisha Korosho wapate stahili zao na hivyo kukuza uchumi wao binafsi na wa nchi kwa ujumla.

“Kuna malalamiko mengi kutoka kwa wakulima ambayo mengine   yanasababishwa na ukosefu wa uadilifu na kuwapo kwa rushwa. Migogoro ni mingi kwenye vyama vya Msingi na Vikuu na inadidimiza dhana nzima ya Ushirika. Na wakulima kutolipwa au kupunjwa fedha za mauzo ya Korosho baada ya Korosho zote kuuzwa minadani. “Kuwapo wa mlolongo wa kodi nyingi zinazotozwa kwenye mauzo ya Korosho mfano; makato ya usambazaji wa fedha na kinachoitwa  Kikosi kazi. Ugumu wa upatikanaji wa pembejeo kwa wakati na huduma za Ugani kutosambaa kwa wakulima wengi,” alisema.

Alisema TAKUKURU imeorodhesha makosa 24, baadhi ya makosa hayo yakiathiri kwa kiwango kikubwa maendeleo ya sekta ya Korosho. “Tunayachunguza katika kutekeleza jukumu letu la kusimamia Sheria katika Sekta. Kuna  mianya mingi ya rushwa kwenye Korosho kama ununuzi wa Korosho kwa njia za vichochoroni maarufu kwa jina la “Kangomba” dhidi ya mfumo rasmi uliowekwa. Viongozi wa Serikali za Mitaa kutojihusisha na jukumu lao la kusimamia taratibu za kiserikali zinazodhibiti ubadhirifu, (wanaporuhusu biashara ya “Kangomba” kufanyika kwenye maeneo wanayoyaongoza kuna uwezekano mkubwa wanafanya hivyo kutokana na kuwapo rushwa) na baadhi ya viongozi wa Serikali na vyama vya Ushirika kuingiza siasa kwenye zao la Korosho na kusababisha athari kubwa kwa wakulima na wanachama.

Akifungua Mkutano huo Waziri Mkuu  Majaliwa alisema Serikali ya awamu ya tano italilinda zao la Korosho kwa kufa na kupona.  Naye Waziri Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dk. Charles Tizeba alisema kuanzia msimu huu dawa ya wadudu ya sulphur itatolewa bure kwa wakulima na kwamba Serikali pia iko mbioni kugawa bure magunia na vifungashio vya zao la Korosho. Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho (CBT) ambayo ndiyo iliyoandaa mkutano huo uliohudhuriwa na washiriki wapatao 600, Hassan Jarufu, amesema tayari wadau wamekutana kupanga namna ya kusambaza pembejeo hizo kwa kutumia Kamati za Pembejeo za Mikoa, Wilaya na Vijiji.  Amesema pia kwamba Bodi ya Korosho itagawa bure kwa wakulima pembejeo za dawa zilizobaki katika msimu uliopita badala ya kuziharibu kwa kuwa zoezi hilo la kuzitekeza ni la gharama kubwa.

Na Bodi ya Korosho Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.