Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Maisha Ya Kanisa Afrika

Shemasi Mkwizu, Jimbo Katoliki Same anasimulia cheche za wito wake!

Shemasi Jonathan Wilfred Mkwizu kutoka Jimbo Katoliki la Same, Tanzania ni kati ya Mashemasi 18 waliopewa Daraja la Shemasi, tarehe 14 Mei 2017 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. - OSS_ROM

16/05/2017 10:56

Mimi ni Shemasi Jonathan, mtoto wa mzee Wilfred Mkwizu na Mama Hediel Emmeanuel   kutoka jimbo la same Tanzania. Mnamo tarehe 26/03/1987, mimi pamoja na pacha wangu tumezaliwa huku tukishika nafasi ya saba katika familia yetu yenye watoto kumi. Nimeanza masomo yangu ya darasa la kwanza mwaka 1994 huku nikihitimu masomo ya sekondari mwaka 2004 katika shule ya sekondari ya kata ya chanjagaa. Baada ya masomo mengine nimeendelea na masomo ya kidato cha tano na sita katika shule ya sekondari ya Kiriki iliyoko chini ya Baraza Kuu la Waislam Tanzania, BAKWATA.

Huku nikiendelea na sala na malezi ya wito wangu, kwa msaada wa mapadre, wazazi wangu na marafiki zangu hatimaye, nilipokelewa kwenye  Kituo cha Malezi huko Dido ambako nililelewa na kulea waseminari wadogo kwa miezi kumi. Na hatimaye, kuanzia mwaka 2009 - 2012 nihitimu masomo yangu ya Falsafa katika Seminari Kuu ya Ntungamo, Jimbo Katoliki Bukoba. Na mwaka huo huo mwezi wa Julai, Askofu Rogath Kimaryo wa Jimbo Katoliki la Same alinituma Roma, Italia kwa masomo ya Taalimungu kuanzia mwaka huo 2012 hadi mwaka 2015 ambako nilipata nafasi ya kurudi nyumbani kwa muda kidogo kabla ya kutumwa tena kwa masomo ya juu zaidi katika Sheria za Kanisa (Canon Law) masomo ambayo naendelea kumalizia.

Wakati huu napenda kumshukuru Mungu kwa kunijalia kupokea Daraja la Ushemasi wa mpito hapo tarehe 13/05/2017 katika Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican  kwa kuwekewa mikono na Kardinali Ferdinand Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, akisaidiana na Askofu mkuu Hon Tai Fai, Katibu mkuu wa Baraza pamoja na Askofu mkuu Protase Rugambwa, Rais wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa na Katibu mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu kutoka Tanzania. 

Ninapenda kumshukuru Mungu  kwa baraka na nafasi hii,  Mhashamu Baba Askofu Rogath Kimaryo wa Jimbo Katoliki  la Same, walezi wangu wa seminari ya kipapa Urbaniana ninakolelewa, Maprofesa wa chuo kikuu cha kipapa Urbaniana, mapadre wetu wa jimbo, watawa, kaka zangu mafrate wa jimbo la same, mfrate rafiki zangu tuliokua pamoja Ntungamo, na wale tulioko nao huku Roma, wana darasa wote na wote wenye mapenzi mema, bila kuwasahau kwa nafasi ya upendeleo wazazi wangu, ndugu zangu na wote walionisaidia na wanaondelea kunisaidia kuijongea Altare ya Bwana. Mungu awabariki na unganeni nami katika sala yangu hii ya kutaka kukaa nyumbani mwa Bwana siku zote za maisha yangu (Zab 27:4) Amina.

Na Shemasi Mkwizu Jonathan Wilfred.

Kutoka Jimbo Katoliki la Same, Tanzania.

16/05/2017 10:56