Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Maisha Ya Kanisa Afrika

Shemasi Charles Kato Rubaza ni "Jembe" jipya kutoka Jimbo la Geita!

Shemasi Charles Kato Rubaza ni "jembe" jipya kutoka Jimbo Katoliki la Geita, aliyepewa Daraja ya Ushemasi, tarehe 13 Mei 2017.

16/05/2017 11:39

Mimi ninaitwa Shemasi Charles Kato Rubaza nilizaliwa kunako tarehe 22.01.1985 katika kijiji cha Rubya huko jimboni Bukoba, kwa wazazi ANDREW KATO na SELINA BAKAGORWAKI. Nilisoma katika Shule ya Msingi Rubya Wasichana ambayo baadaye ilibadilishwa jina na kuitwa Rubya A, nilianza shule ya msingi mnamo mwaka 1994-2000. Mwaka 2001-2002 nilijiunga na Shule ya Upili ya Masaka, na mwaka 2003 nilijiunga na Shule ya Upili ya Crane iliyoko Kitintale Kampala ambako niliitimu masomo ya Kidato cha IV mwaka 2005. Na mwaka 2006 nilijiunga na Seminari ndogo ya Kisubi ya Jimbo Kuu la Kampala kwa masomo ya Kidato cha Tano na Sita na kuhitimu mnamo mwaka 2007.

Mwaka 2008 niliomba na kuitwa rasmi na Askofu Damian Dallu wa Jimbo Katoliki Geita kwa wakati huo na kuanza malezi kwa ajili ya maandalizi ya kwenda Seminari Kuu. Na mwezi wa Julai mwaka 2008 nilijiunga na Seminari Kuu ya Mt. Augustino iliyoko katika jimbo Kuu la Songea kwa masomo ya Falsafa kwa miaka mitatu yaani kati ya mwaka 2008-2011, niliendelea katika Seminari hiyo hiyo kwa masomo ya Taalimungu kwa mwaka mmoja (2012) na mwaka 2013 nitumwa na Baba Askofu Damian Dallu kuja hapa Roma kuendelea na masomo ya Taalimungu na niliihitimu masomo hayo mwaka 2015. Baada ya kuhitimu masomo ya Taalimungu nilianza masomo ya Uzamivu katika Sheria za Kanisa 2015 na nategemea kumaliza mwezi Juni,  mwaka 2017, tayari kurejea Jimboni Geita kwa ajili ya kuwahudumia watu wa Mungu kwa ari na moyo mkuu!

Ninamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya wito wa upadre ambao naweza kusema nilianza kusikia sauti katika miaka ya awali ya maisha yangu na hasa wakati nikisoma katekesi katika Parokia ya Rubya, na baadaye kama mtumikiaji wa Ibada ya Misa Takatifu Altareni. Nilivutwa sana na moyo wa Ibada. Ninawashukuru sana Mapadre wa Parokia ya Rubya hii mbegu iliyo ndani yangu, walitusisitiza daima kusikiliza vema sauti ya Mungu ili kuweza kuitofautisha na sauti zingine. Walinisaidia sana kuitambua sauti ya Mungu na kuifuata. Walezi wangu katika seminari ndogo na kubwa wote walinisaidia kuendela kuitambua na kuifuata sauti ya Mungu. 

Hii ndiyo changamoto inayotolewa pia na Baba Mtakatifu Francisko anayetukumbusha kwamba, wito wa Kikristo ni mwaliko wa kutoka katika ubinafsi, tayari kujizatiti kusikiliza sauti ya Mwenyezi Mungu anayeita daima. Jumuiya ya Kikristo ni mahali muafaka pa kuibua, kukuza na kushuhidia wito wa Kikristo, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani!

Namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa zawadi hii ya wito wa Upadre, na mnamo tarehe 13.05.2017 nimepewa Daraja ya Ushemasi wa mpito katika Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa kuwekewa mikono na Kardinali Ferdinand Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, akisaidiana na Askofu mkuu Hon Tai Fai, Katibu mkuu wa Baraza pamoja na Askofu mkuu Protase Rugambwa, Rais wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa na Katibu mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu.

Ninamshukuru Baba Askofu Flavian Matindi Kassala wa Jimbo Katoliki Geita, Tanzania kwa kunitia moyo kusonga mbele katika maisha na utume wangu ili siku moja niweze kuwa ni Kristofa yaani chombo kinachombeba Kristo kwa wengine! Mimi naweza kusema wito wowote katika Kanisa Takatifu ni zawadi kutoka kwa Mungu na anayeitika wito huo kwa hiyari, upendo, imani na unyenyekevu anaunganika na Mungu kuutangaza na kuushuhudia upendo wa Mungu kwa watu wote maana “Mungu ni upendo” Rej.  1Yn 4:8.

Ni mimi Shemasi Charles Kato Rubaza

Kutoka Jimbo Katoliki la Geita. 

16/05/2017 11:39