2017-05-16 09:29:00

Papa Francisko kutembelea Ikulu ya Italia tarehe 10 Juni 2017


Dr. Greg Burke, Msemaji mkuu wa Vatican katika taarifa yake kwa vyombo vya habari anasema kwamba, Baba Mtakatifu Francisko tarehe 10 Juni 2017 atatembelea rasmi Ikulu ya Italia, ili kukutana na kuzungumza na Rais Sergio Mattarella wa Italia, kama kielelezo cha shukrani kwa ziara ambayo Rais Mattarella aliifanya mjini Vatican tarehe 18 Aprili 2015. Hii itakuwa ni fursa kwa viongozi hawa wawili kuendelea kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Italia. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko tarehe 14 Novemba 2013 alikwenda kumtembelea wakati huo Rais Giorgio Napolitano. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alitembelea Ikulu ya Italia kunako tarehe 4 Oktoba 2008.

Kuna uhusiano mwema kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Rais Sergio Mattarella ambaye amekuwa akimpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu! Baba Mtakatifu amekuwa ni sauti ya maskini, wakimbizi na wahamiaji; vijana wasiokuwa na fursa za ajira. Ameendelea kusimamia kanuni maadili na utu wema kwa kukemea kwa nguvu zake zote saratani ya rushwa na ufisadi wa mali ya umma.

Rais Sergio Mattarella alipomtembelea Baba Mtakatifu Francisko tarehe 18 Aprili 2015 walijadili pamoja na mambo mengine: changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji Barani Ulaya; ukosefu wa fursa za ajira; mauaji ya kimbari ya Waarmeni, hali iliyokuwa imesababisha mtikisiko wa kidiplomasia kati ya Uturuki na Vatican. Walikazia umuhimu wa kanuni maadili na hali jamii bila kusahau nafasi ya waamini walei katika mustakabali wa maisha na utume wa Kanisa na jamii katika ujumla wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.