2017-05-16 15:06:00

Nani kama mama?


Msikilizaji mpendwa, Jumuiya ya Kimataifa Jumapili iliyopita, tarehe 14 Mei 2017 imeadhimisha Siku ya Mama Duniani. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, aliwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kusali katika ukimya ili kuwakumbuka na kuwaombea mama zao ambao bado wako hapa duniani, na wale ambao wamekwisha kutangulia mbele ya haki, kwa kukumbuka wema na ukarimu wao; kwa ujasiri na upendo wao uliowawezesha kusimama kidete kulinda na kudumisha Injili ya uhai!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, dunia bila mama ni ulimwengu usiokuwa na utu kwani akina Mama ni mashuhuda wa tunu msingi za maisha na utu wa binadamu! Wanawake wanashiriki kikamilifu katika kazi ya uumbaji, dhamana kubwa sana ambayo wanawake wanashirikishwa katika maisha na utume wao! Kumbe, wanawake wawe mstari wa mbele dhidi ya utamaduni wa kifo! Maadhimisho haya yamekuwa ni fursa ya kutambua na kuenzi tena na tena dhamana na wito wa wanawake ndani ya Kanisa na Jamii katika ujumla wao!

Akina Mama hata katika shida, magumu na changamoto za maisha yao, daima wameweza kuonesha: huruma, ukarimu, upendo na faraja kwa watoto wao. Akina Mama wamekuwa ni walimu na makatekista wa kwanza katika kurithisha imani, matumaini na mapendo kwa watoto wao. Hii inatokana na ukweli kwamba,  wanawake ndio wanaokaa na watoto wao kwa muda mrefu! Kanisa ni mama mwema na mpendelevu; anayewajali na kuwatunza watoto wake. Siku ya Mama Duniani, imekuwa ni siku ya kusherehekea Injili ya uhai; sadaka, majitoleo pamoja na ukimya unaooneshwa na wanawake katika maisha yao ya kila siku!

Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa awe ni mfano bora wa kuigwa katika Sala, tafakari ya matendo makuu ya Mungu katika maisha ya mwanadamu, lakini zaidi, tayari kujisadaka kwa ajili ya kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha. Bikira Maria alikuwa ni Mama mwenye imani, matumaini na mapendo makuu; aliyempokea Mwana wa Mungu, akawa ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili; akamsindikiza katika maisha na utume wake; akafanya naye safari katika Njia ya Msalaba, kiasi cha kusimama chini ya Msalaba. Tangu wakati huo, amekuwa ni Mama wa Kanisa na Mama wa wote. Basi Bikira Maria awe ni mfano bora wa kuigwa, jamii inapoendelea kuwaenzi akina mama wote duniani. Msikilizaji, Basi kwa maelezo haya nimefikishwa mwisho wa ujumbe huu.  Nawaageni na kuwatakia kila la kheri.

Na Pauline Mkondya,

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.