Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Maisha Ya Kanisa Afrika

Mashemasi wapya! Kazeni buti ndo kwanza kumekucha!

Askofu mkuu Rugambwa: Mashemasi wapya jiandaeni vyema kupokea Daraja ya Upadre kwa kujikita katika huduma makini na utakatifu wa maisha!

16/05/2017 14:46

Askofu mkuu Protase Rugambwa Rais wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa na Katibu mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, Jumapili tarehe 14 Mei 2017 amewapongeza Mashemasi wapya wawili Shemasi Charles Kato Rubaza kutoka Jimbo Katoliki la Geita na Shemasi Jonathan Wilfred Mkwizu kutoka Jimbo Katoliki la Same, Tanzania kwa hatua kubwa waliyofikia katika malezi na majiundo yao, kiasi cha kupewa Daraja ya Ushemasi wa mpito. Askofu mkuu Rugambwa, amechukua nafasi hii kuwashukuru na kuwapongeza, wazazi, walezi na wafadhili mbali mbali wanaosaidia kufanikisha majiundo ya Majandokasisi wanaojiandaa kwa ajili ya kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani zao sehemu mbali mbali za Tanzania.

Askofu mkuu Protase Rugambwa amemshukuru Mwenyezi Mungu anayependakiza mbegu ya miito mitakatifu katika maisha ya waja wake, kiasi cha kumea, kukua na kukomaa katika Daraja ya Ushemasi na hatimaye, Daraja Takatifu ya Upadre. Amewataka Mashemasi wapya kwa kuitikia wito huu na waendelee kujizatiti katika malezi, maisha na ushuhuda wao, tayari kuelekea katika Daraja ya Upadre ni kujisadaka kwa ajili ya huduma ya kufundisha, kutakatifuza na kuwaongoza watu wa Mungu nchini Tanzania kadiri ya majimbo yao! Askofu mkuu Protase Rugambwa amewashukuru na kuwapongeza wazazi, walezi, ndugu na jamaa walioshiriki katika hafla ya kumshukuru Mungu na kuwapongeza Mashemasi wapya. Kwa namna ya pekee, amewapongeza watanzania wanaoishi Roma kwa kuonesha umoja, upendo na mshikamano katika matukio mbali mbali, jambo ambalo ni la kujivunia sana hasa wanapokuwa ughaibuni!

Itakumbukwa kwamba katika kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima, akawahimiza waamini kusali, kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, tayari kuchuchumilia na kuambata utakatifu wa maisha, Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, Jumamosi, tarehe 13 Mei 2017 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na kutoa Daraja la Ushemasi wa mpito kwa Majandokasisi 18 kutoka katika nchi za kimissionari zinazosimamiwa na kuratibiwa na Baraza lake.

Jumuiya ya watanzania wanaoishi mjini Roma, Jumapili tarehe 14 Mei 2017 iliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu ili kumshukuru Mungu kwa zawadi ya Daraja la Ushemasi wa mpito kwa mashemasi hawa wawili kutoka Tanzania. Ibada hii iliongozwa na Padre Elias Masolwa, Makamu Askofu Jimbo Katoliki Geita na mahubiri kutolewa na Padre Apolinari Moris Mshighwa kutoka Jimbo Katoliki la Same. Amewatia moyo Mashemasi wapya na kuwataka kushikamana na Kristo Yesu katika maisha na utume wao, ili kuweza kukabiliana na matatizo, magumu na changamoto za maisha na utume wa Kipadre kama ilivyokuwa kwa Mashemasi wa Kanisa la mwanzo. Yesu mwenyewe anawaambia wafuasi wake wasifadhaike mioyoni mwao, bali waendelee kuwa na imani na matumaini kwake kwani Yeye ni: Njia, Ukweli na Uzima. Wakumbuke kwamba, hata Mitume katika Kanisa la mwanzo walionja manung’unuko na migawanyiko, lakini wakabaki imara na thabiti katika Neno na Sakramenti za Kanisa.

Mashemasi wapya waboreshe maisha yao kwa kuambatana na kushikamana na Kristo Yesu katika: Sala, Tafakari na Maadhimisho ya Mafumbo Matakatifu ya Kanisa kadiri ya dhamana na nafasi zao. Daima watambue kwamba, msingi wa maisha na wito wa Kipadre ni Kristo mwenyewe, jiwe kuu la msingi ambalo wanapaswa kujijenga juu yake kwa njia ya huduma na utakatifu wa maisha! Padre Apolinari Moris Mshighwa amewataka Mashemasi kujenga na kudumisha umoja na mshikamano na Kristo Yesu ambaye ni: Njia, Ukweli na Uzima, ili aweze kukamilisha kile ambacho Mwenyezi Mungu amekianzisha ndani mwao, yaani maisha na wito wa Kipadre.

Baada ya adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu na Mashemasi wakahudumia Altareni kwa mara ya kwanza, kulifuatia halfla ya kukata na shoka iliyoandaliwa na Jumuiya ya watanzania wanaoishi mjini Roma! Kati ya maajabu yaliyowaacha wengi wakiwa na midomo wazi ni “Pilau ya Kande” kutoka Same iliyoandaliwa na kupikwa kwa ufundi mkubwa na hasa ukitambua kwamba, sherehe hii imeadhimishwa ughaibuni! Kwa familia ya Mungu kutoka Jimbo Katoliki la Same, kilikuwa ni kicheko kwenda mbele!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 

16/05/2017 14:46