2017-05-15 09:08:00

Miaka 100 ya kutokea Maria sala zimetiririka kama maji ya mto !


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, Jumapili tarehe 14 Mei 2017 amekumbusha juu ya ziara yake ya kitume huko Fatima tarehe 12-13 Mei 2017 na kusema kwamba, leo hii kuna haja kusali  na kutubu, ili  vita hasa vya Mashariki ya Kati viweze kusitishwa, mahali ambapo watu wachache wanapata misukosuko na ubaguzi. Aidha anamshukuru Bwana aliyemwezesha kwenda na  kusimama chini ya miguu ya Bikira Maria kama muhujaji wa matumaini na amani. Anamshukuru kwa moyo wote Askofu wa Leiria-Fatima, viongozi wa Serikali kwa namna ya pekee Rais wa Ureno na wote walioshiriki kujitoa ili kufanikisha ziara na sikukuu hiyo ya Fatima.

Baba Makatifu kabla ya sala ya Malkia wa Mbingu, asubuhi kama kawaida anaporudi katika ziara yake, amekuwa na utamaduni wa kwenda katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Maria Mkuu mjini Roma  kushukuru ambapo amepeleka waridi jeupe na kubaki kimya kwa tafakari mbele ya picha ya mama Maria Mkuu. Kwa upande wa  ziara yake ya Fatima, ameweka mwanga wa utakatifu wa Francis na Jacinta na kusema, siyo kufikiria tu mfululizo wa matukio ya kutokewa kwao, bali ni kutazama ule  uaminifu mkubwa walio uonesha pia bahati ya kuweza kumwona Bikira Maria. Aidha  kwa njia ya kuwatangaza watakatifu hao Baba Mtakatifu alitaka kutoa wito kwa  Kanisa  zima kujikita katika  shughuli ya ulinzi wa watoto. Maana amesema, huko Fatima ni miaka 100 sala zinaendelea kama maji yatiririkayo katika mto,watu wakisali sana  kuomba ulinzi wa Mama Maria kwa ajili ya dunia. Huo ni mfano wa sala ya  Francis na Yacinta Marto walio kuwa wakisali ili vita vya kwanza vya dunia viweze kuisha na hivyo hata leo hii bado vipo anasema Baba Mtakatifu.

Hata leo kuna haja ya sala na kutubu pia kwa ajili ya kuomba neema ya uongofu , kusali kwasababu vita viweze kuisha  ambavyo vimetawanyika kila upande duniani, kusali  kwa ajili ya kuisha  migogoro isiyo kuwa na maana, mikubwa au midogo  ya kifamilia na misukosuko inayoathiri sura ya ubinadamu.  Kwa njia hiyo Baba Mtakatifu Francisko anamkabidhi Maria wa Amani watu wengi wanaosumbuliwa na migogoro ya kivita kwa namna ya pekee katika nchi za mashariki ya Kati. Anasisitiza, watu wengi wasio kuwa na hatia wanajaribiwa, wakristo na waislam na hata madhehebu madogo kama Yazidi yanayokabiliwa na misukosuko na kubaguliwa. Kwa kutoa mshikamano wake, anawasindikiza kwa sala, wakati huo huo akiwashukuru watu wote wenye mapenzi mema kujikita katika shghuli za mahitaji ya kibinadamu. Anawatia  moyo jumuiya zote hizoili waweze kuombea katika njia ya mazungumzo na mapatano ya urafiki kijamii, kujenga heshima ya baadaye , usalama na amani ili vita viweze kuishilia mbali.

Aidha Baba Mtakatifu Francisko amekumbuka kuwa Jumamosi 13 Mei 2017  Huko Dublin, Ireland alitangazwa Mwenye heri Padre John Sullivan, Myesuit ambaye alikuwa ni baba wa maskini na wanaoteseka. Na katika salam zake kwa namna ya pekee wamewageukia waanzilishi wa viti visivyo na watoto wadogo vilivyokuwa vimewekwa katika uwanja wa Mtakatifu Petro , kama ishara ya maisha ya kuadhimisha siku ya Mama duniani kote, ametoa wito kwamba maisha ya jamii yetu endelevu yanahitaji juhudi za  kila mmoja na zaidi taasisi zote kuwa makini katika kujikita kwa dhati kwenye masuala ya umama. Na mwisho ametoa wito kwa mahujaji na waamini 25,000 waliokuwa uwanja wa Mtakatifu Petro Mjini Vatican kusali  kitambo kila mmoja akimwombea  mama binafsi.

Ikumbukwe kwamba:Siku ya mama duniani huadhimishwa katika siku tofauti kulingana na nchi na nchi. Nchi nyingi hata hivyo huiadhimishwa siku hiyo kila Jumapili ya pili ya mwezi wa tano. Kwa mwaka huu siku hiyo imeadhimishwa tarehe 14 Mei 2017 ambayo ni sherehe za kumshukuru mama wa familia, pamoja na umama, uzazi wanaopitia na mchango mkubwa wa mama katika jamii.

 

Sr Angela Rwezaula
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.
 
 
 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.