2017-05-15 13:39:00

Mashemasi ni wahudumu wa Neno na Injili ya huduma kwa maskini!


Mama Kanisa anafundisha kwamba, Mashemasi hushiriki kwa namna ya pekee utume na neema ya Kristo. Sakramenti ya Daraja Takatifu huwapa chapa ya kudumu na hivyo kufananishwa na Yesu Kristo aliyejifanya “Shemasi”, yaani Mtumishi wa wote! Mashemasi ni wasaidizi wakuu wa Maaskofu na Mapadre katika maadhimisho ya Mafumbo ya Mungu na kwa namna ya pekee, Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Mashemasi ni wahudumu wa Neno la Mungu kwa kutangaza na kuhubiri Injili; kwa kusimamia na kubariki ndoa; kwa kuongoza mazishi na hasa zaidi kwa kujitoa kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya huduma ya upendo kwa niaba ya Kanisa!

Katika kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima, akawahimiza waamini kusali, kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kuchuchumilia na kuambata utakatifu wa maisha, Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, Jumamosi, tarehe 13 Mei 2017 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na kutoa Daraja la Ushemasi wa mpito kwa Majandokasisi 18 kutoka katika nchi za kimissionari zinazosimamiwa na kuratibiwa na Baraza lake.

Familia ya Mungu Barani Afrika, imebahatika kutoa Mashemasi 11 na wawili kati yao ni Shemasi Rubaza Kato Charles kutoka Jimbo Katoliki la Geita na Shemasi Mkwizu Jonathan Wilfred wa Jimbo Katoliki la Same, Tanzania. Wengine ni: Ciza Gabriel kutoka Burundi; Cyebwa Thèodore, DRC; Irene Augustine, Nigeria; Madvamuse Hubert Wedzerai kutoka Zimbabwe; Malila Bakang Morris kutoka Botswana na Mba Basil Ikechukwu kutoka Nigeria. Wengine ni: Mukendi Tshiabola Dieudonnè, DRC; Ndolo ndolo Parfair Bienvenu kutoka Congo Brazzavile na mwishoni ni Shemasi Yeboah Joseph kutoka Ghana.

Kardinali Filoni katika wosia wake kwa Mashemasi wapya amewakumbusha kwamba, kama ilivyokuwa kwa Kanisa la Mwanzo, wameandaliwa vyema: kiutu, kiakili, kiroho na kichungaji ili waweze kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu katika maisha ya watu wanaowazunguka. Mashemasi wapya watambue kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya upendo inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, yanayotekelezwa na Mama Kanisa kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Kardinali Filoni amewataka Mashemasi wapya kuhakikisha kwamba, wanautumia vyema muda waliopewa na Mama Kanisa katika masomo na majiundo yao, tayari kurejea katika Makanisa yao Mahalia, ili kusaidia kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu katika ukamilifu wa Daraja Takatifu ya Upadre. Mashemasi wamekumbushwa kwamba, ndugu zao katika Makanisa mahalia wanatamani siku moja kuwaona wakiwahudumia huko nyumbani kwao! Ibada hii, imehudhuriwa na baadhi ya wazazi na walezi wa Mashemasi hawa wapya kutoka sehemu mbali mbali za dunia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.