2017-05-15 13:30:00

Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima ni daraja la huruma ya Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu Jumamosi, tarehe 13 Mei 2017, kama kilele cha Jubilei ya Miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima, alipata chakula cha pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki la Ureno pamoja viongozi wote waliokuwa kwenye msafara wake. Katika hotuba yake, Kardinali Manuel Clemente, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Lisbon, Ureno amemsifu na kumshukuru Baba Mtakatifu Francisko anayeendelea kujielekeza zaidi kama chombo na shuhuda wa huruma ya Mungu kwa waja wake; mafundisho makuu ya Kanisa yanayopata mwangwi pia katika tukio la Bikira Maria kuwatokea Watoto wa Fatima, miaka 100 iliyopita.

Watoto wa Fatima yaani: Mtakatifu Francisko Marto na Mtakatifu Yacinta Marto pamoja na Mtumishi wa Mungu Sr. Lucia dos Santos, walikuwa wanakazia upendo kwa Mungu na jirani ili kuwaokoa watu waliokuwa wanaelemewa na matatizo ya maisha ya kiroho na kimwili! Bikira Maria wa Fatima akawahimiza watoto hawa kufanya toba na malipizi ya dhambi, kwa ajili ya wongofu wa walimwengu. Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima, yamekuwa ni mahali ambapo machozi ya watoto wa Mungu yamegeuzwa kuwa ni kisima cha matumaini ili kuvuka vita na machafuko kwa kujikita katika amani; amana inayobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu na Moyo Safi wa Bikira Maria usiokuwa na doa.

Ni kutokana na mwelekeo, mafundisho na changamoto mamboleo kwamba, Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima na uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko pamoja na mafundisho yake, yanapata umuhimu wa pekee ndani ya Kanisa na katika maisha ya familia ya Mungu ndani na nje ya Ureno. Familia ya Mungu nchini Ureno inamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko aliyeamua kufanya hija ya kiroho na kuungana na mahujaji wengine wote kutoka sehemu mbali mbali za dunia kwa ajili ya kuadhimisha kilele cha Jubilei ya Miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima.

Baba Mtakatifu kwa uwepo na ukimya wake, ameonesha umuhimu wa sala na tafakari katika maisha ya waamini. Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima katika kipindi cha miaka 100 iliyopita yamekuwa ni mahali pa sala kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro na nia zake kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Uwepo wa Khalifa wa Mtakatifu Petro kati pamoja na mahujaji wengine ni changamoto ya kukumbuka kwamba, upendo wa Mungu umefunuliwa kwa njia ya Kristo Yesu, ukamwilishwa kwake Bikira Maria na sasa unashuhudiwa na Kanisa na kwa namna ya pekee na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Katika kipindi cha miaka 100 iliyopita, kumekuwepo na uhusiano wa pekee kati ya Madhabahu ya Bikira Maria na Mapapa wa Kanisa. Kunako mwaka 1917 Papa Benedikto wa kumi na tano alitembelea Madhabahu ya Fatima, akimwomba Bikira Maria wa Fatima kuwaokoa walimwengu dhidi ya vita ambayo haikuwa na miguu wala kichwa! Alikwenda kuombea toba na wongofu wa ndani, kiini cha ujumbe wa Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima. Papa Pio XI na Pio XII; Yohane XXIII, Mtumishi wa Mungu Papa Paulo VI, Yohane Paulo II, Benedikto XVI na sasa funga kazi katika kilele cha Jubilei ya Miaka 100 amekuwa ni Papa Francisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.