2017-05-13 14:23:00

Papa: Igeni mfano wa watakatifu Francis Marto na Yacinta Marto!


Katika maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Fatima, sanjari na kilele cha Jubilei ya Miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima, Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 13 Mei 2017 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima na kuwatangaza Wenyeheri Francis na Yacinta Marto kuwa watakatifu. Ibada hii ya Misa Takatifu imehudhuriwa na bahari ya watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia!

Maandiko Matakatifu yanamwonesha Bikira Maria kuwa ni yule Mwanamke aliyevikwa jua, na mwezi ulikuwa chini ya miguu yake. Pale chini ya Msalaba, Yesu alimkabidhi Mama yake mpendwa kwa yule mwanafunzi aliyempenda. Watoto wa Fatima katika ushuhuda wao wanakiri kwamba, Bikira Maria alikuwa ni mwanamke mzuri sana, kiasi kwamba, Mtakatifu Yacinta akashindwa kuhifadhi siri ya uzuri wa Bikira Maria na kuamua kumshirikisha mama yake kwamba, wamemwona Bikira Maria. Ujio wa Bikira Maria ilikuwa ni fursa na mwaliko wa kuchuchumilia utakatifu wa maisha, tayari kuingia mbinguni!

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake amesema, kwamba, katika maisha ya mwanadamu kuna matukio ambayo yanaendelea kumkufuru Mungu pamoja na viumbe wake! Bikira Maria amewatokea Watoto wa Fatima ili kuwakumbusha walimwengu kwamba, mwanga wa uwepo wa Mungu upo na unawaandama watu wake, mwelekeo ulioneshwa pia na Watoto wa Fatima waliotokewa na Bikira Maria. Madhabahu ya Fatima ni kielelezo cha mwanga wa Mungu unaowafunika waja wake, pengine kuliko hata sehemu yoyote ile ya dunia; ni mahali ambapo watu wanakimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria, kama ambavyo waamini wanasali katika ile “Salve Regina” yaani “Salam Malkia”.

Baba Mtakatifu anawakumbusha mahujaji kwamba wanaye Mama, wamwendee na kumkimbilia katika matumaini kwa kumwegemea Kristo Yesu, ili kupata neema na haki katika utimilifu wa maisha katika Yeye. Kristo aliyepaa mbinguni, ameutukuza ubinadamu wake uliomwilishwa katika tumbo la Bikira Maria. Kwa njia hii, Yesu anakuwa ni tumaini la waja wake, changamoto ni kuendelea kuwa ni watu wa matumaini hadi dakika ya mwisho! Ni matumaini haya ambayo yamewajumuisha watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia ili kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kipindi cha miaka 100 iliyopita, tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima.

Waamini mbele ya macho yao wana mifano ya watakatifu Francis  Marto na Yacinta Marto, walioingizwa kwenye mwanga wa kumwabudu Mwenyezi Mungu, akawa ni nguvu ya kuweza kuvuka kinzani na mahangaiko ya ndani. Uwepo wa Mungu katika maisha, ukawa ni chachu ya kudumu katika sala kwa ajili ya toba, wongofu wa ndani na malipizi ya dhambi za walimwengu; wakatamani daima kubaki karibu na “Yesu aliyejificha” kwenye Tabernakulo. Katika mwanga huu, Mtumishi wa Mungu Sr. Lucia dos Santos aliona mahangaiko ya umati mkubwa wa watu wakiteseka kwa baa la njaa, Khalifa wa Mtakatifu Petro akiwa mbele ya Moyo Safi wa Maria akisali, huku akiwa amezungukwa na umati mkubwa wa watu! Baba Mtakatifu anawashukuru ndugu zake katika Kristo kwa kumsindikiza katika hija ya matumaini na amani katika Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima. Amekuja kuwakabidhi watoto wa Kanisa na walimwengu wote kwa Bikira Maria, ili aweze kuwahifadhi, kuwapatia matumaini na amani wanaoitamani ndani mwao.

Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu anapenda kumkabidhi Bikira Maria wagonjwa na walemavu; wafungwa na watu wasiokuwa na ajira; maskini na wale waliotengwa. Anawaalika kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwasikiliza na kuwapatia msaada wa daima. Watambue kwamba, wameumbwa kwa ajili ya kuwa ni matumaini kwa wengine, changamoto na mwaliko wa kushirikiana na kushikamana! Sadaka na ukarimu utawezesha maisha kusonga mbele na kuzaa matunda yanayokusudiwa. Pale waamini wanapokutana na Msalaba, watambue kwamba, tayari mbele yao amepita Kristo Yesu, aliyejinyenyekesha hata kifo cha Msalaba ili aweze kuwakomboa na kuwaokoa kutoka katika giza la ubaya na kuwapeleka katika mwanga wa maisha. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawaalika waamini kutafakari Uso wa kweli wa Kristo Mkombozi wa dunia, Uso unaong’aa katika Kipindi cha Pasaka, ili kugundua uso wa Kanisa la Kristo linalojikita katika azma ya umissionari, ukarimu, huru, aminifu na maskini wa vitu lakini mwingi wa utajiri wa upendo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.