2017-05-13 15:09:00

Papa Francisko: Dumisheni Ibada safi kwa Bikira Maria!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya sala ya kuwakabidhi walimwengu wote chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Fatima, Ijumaa tarehe 12 Mei 2017 katika mkesha wa kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima, akiwa kwenye Kikanisa cha Bikira Maria wa Fatima, alibariki mishumaa na hatimaye, akawasha mshumaa wake kwenye Mshumaa wa Pasaka, akatoa salam zake na baadaye kuongoza Ibada ya Rozari Takatifu, ambayo kimsingi ni muhtasari wa historia nzima ya kazi ya ukombozi.

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru waamini na mahujaji wote kwa mapokezi makubwa kwake kama hujaji wa matumaini na amani; amewahakikishia wote aliokabidhiwa kwake na Kristo Yesu anawabeba katika “sakafu ya moyo wake”. Anapenda kuwakabidhi wote kwa Yesu, lakini zaidi wale wenye shida na mahangaiko makubwa. Bikira Maria Mama wa faraja awaombee baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu wale: wasiopendwa; waliotengwa na kusukumiziwa pembezoni mwa jamii; wale wote wanaopokwa matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi; yatima na wale wote walionyimwa haki zao msingi! Amewaombea baraka ya Mwenyezi Mungu iliyomwilishwa katika Kristo Yesu, iweze kuwalinda; Mwenyezi Mungu aweze kuwaangazia nuru za uso wake na kuwafadhili; awainulie uso wake na kuwapatia amani.

Baba Mtakatifu anasema, baraka hii imepata utimilifu wake ndani ya Bikira Maria aliyebahatika kuwa ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili; Uso wa huruma ya Baba wa milele ambao waamini wanautafakari katika Matendo ya Rozari Takatifu na kwamba, kwa njia ya Kristo Yesu na Bikira Maria, waamini wanaweza kuendelea kubaki wakiwa ndani ya Mwenyezi Mungu. Ili kuwa Wakristo, kweli, waamini hawana budi kuwa na Ibada kwa Bikira Maria, kwa kutambua mambo msingi yanayounganisha maisha ya Bikira Maria na Kristo Yesu. Kwa kusali Rozari Takatifu, Injili ya Kristo inaendelea kutangazwa na kumwilishwa katika maisha, watu, familia na katika ulimwengu mzima!

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kufanya hija pamoja na Bikira Maria, Mwalimu mkuu katika maisha ya kiroho, aliyethubutu kumfuasa Kristo katika Njia ya Msalaba, akabarikiwa kwa kuwa aliamini! Anawaonya waamini kutomkimbilia Bikira Maria kwa kutaka awafanyie miujiza ya “chapuchapu”, kwani Bikira Maria wa Injili anayeheshimiwa na Kanisa ni yule anayeangalia mambo msingi, anayewaombea watoto wake huruma ya Mungu ili hatimaye, kukutana na Hakimu mwenye haki, yaani Mwana kondoo wa Mungu aliyechinjwa kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu!

Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo anasema Baba Mtakatifu, mwaliko kwa waamini kukimbilia huruma ya Mungu badala ya kuogopa hukumu yake kwa kutambua kwamba, huruma ya Mungu kamwe haiwezi kuondoa haki! Yesu aliteswa na kufa Msalabani ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la utumwa wa dhambi na mauti. Kwa njia ya imani inayowaunganisha katika Msalaba wa Kristo, wamekombolea na hivyo kuwekwa huru, kumbe hakuna sababu ya kuwa na woga, bali kukimbilia na kuambata upendo wake. Bikira Maria ni kielelezo cha mapinduzi ya wema na upendo wa Mungu kwa binadamu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Bikira Maria anaonesha kwamba unyenyekevu na upole si fadhila ya wanyonge bali ni fadhila ya watu wenye nguvu ambao hawana sababu ya kuwatendea wengine ubaya ili kuonekana kuwa ni watu wa maana sana. Mwingiliano wa haki na upole, wa taamuli na kujali mahitaji ya wengine ndiyo inayolifanya Kanisa limtazame Bikira Maria kama mfano bora wa uinjilishaji. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini wote kuiga mfano wa Bikira Maria, ili waweze kuwa ni alama na Sakramenti ya huruma ya Mungu anayesamehe yote! Kwa kushikamana na Bikira Maria, wote wanaweza kuimba huruma ya Mungu kwani ni huruma ambayo amewakirimia watakatifu na watu wake waaminifu imeweza kuwafikia wengine wote. Kwa njia ya kiburi cha binadamu na uchu wa malimwengu, binadamu ameshindwa kutimiza hamu ya moyo wake! Njia pekee ya kuweza kuinuka tena ni kwa njia ya Bikira Maria kumshika mkono na kumfunika kwa joho ili kumweka pembeni wa Moyo wake usiokuwa na doa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.