2017-05-12 12:33:00

Mwenyeheri John Sullivan: Shuhuda wa wongofu wa kikristo na Kitawa


Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu, Jumamosi, tarehe 13 Mei 2017, Kanisa linapoadhimisha kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Fatima, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, atamtangaza Mtumishi wa Mungu Padre John Sullivan, SJ., kuwa Mwenyeheri. Ibada hii inaadhimishwa nchini Ireland. Padre John Sullivan, Myesuit aliishi kati ya Mwaka 1861 hadi Mwaka 1933 akabahatika kuaga dunia katika hali ya utakatifu wa maisha!

Kardinali Angelo Amato anasema, jambo la msingi katika maisha ya mwamini ni toba na wongofu wa ndani. Mwenyeheri John Sullivan alibahatika kupata wongofu wa ndani, tarehe 21 Desemba 1896 alipohama Kanisa Anglikani na kuingia katika Kanisa Katoliki na tarehe 7 Septemba 1900 akapata wongofu awamu ya pili kwa kuingia katika Shirika la Wayesuit kama Mnovisi na baada ya masomo na majiundo yake ya kitawa, kunako tarehe 28 Julai 1907 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Wongofu awamu ya pili ulikuwa ni msaada wa neema ya Mungu iliyofanya kazi ndani mwake, kiasi hata cha kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha umwilishaji wa tunu msingi za maisha ya Kikristo!

Mwenyeheri John Sullivan alikuwa ni mfano bora wa kuigwa katika maisha ya kitawa, kwani alijitahidi kuishi kikamilifu mashauri ya Kiinjili, hasa nadhiri ya ufukara na utii, akawa maskini kati ya maskini kwa kujitahidi kumwilisha nadhiri ya ufukara katika maisha na utume wake, ingawa alibahatika kuzaliwa katika familia iliyokuwa inajiweza kiuchumi! Daima alifarijika na kile ambacho alipatiwa katika maisha na utume wake kama mtawa! Hakupenda kubandukana na Msalaba, kielelezo makini cha huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu.

Alijitahidi kukamilisha mateso ya Kristo Yesu katika maisha yake, akaiga mfano bora wa maisha na utume wa Mtakatifu Inyasi wa Loyola kwa kumchagua Kristo fukara kati ya maskini badala ya kukimbilia utajiri na malimwengu; alikubali kuteseka kwa ajili ya Kristo badala ya kupambwa na sifa na heshima za walimwengu! Akakubali kuwa mjinga kwa ajili ya Kristo Yesu, hata kama alitambua kwamba alikuwa na hekima na busara. Katika ufukara alibahatika pia kuonesha na kushuhudia utii kwa Kristo na Kanisa lake; Utii kwa viongozi wake wa Shirika! Alionesha upendo wa hali ya juu kwa Shirika la Wayesuit na Katiba yake.

Kardinali Angelo Amato anasema, Mwenyeheri John Sullivan kwa hakika alikuwa ni shuhuda na mfano bora wa kuigwa katika umwilishaji wa nadhiri za kitawa katika maisha yake kiasi cha kufumbatwa katika unyenyekevu wa hali ya juu. Alikuwa ni msomi na wakili, mtu mwenye uzoefu na mkomavu katika maisha; lakini akajichanganya na kuchanganyika na vijana waliokuwa wanapevuka kwa wakati ule, wakiwa na umri kati ya miaka 17 hadi 20. Akaonesha unyenyekevu wa hali ya juu katika utekelezaji wa dhamana na majukumu aliyokabidhiwa na Shirika; akapokea shutuma na kejeli za maisha kwa uvumilivu mkuu; akaonesha ukweli wa maisha na unyofu wa moyo. Hata pale alipotishiwa maisha katika utume, aliomba msamaha, kiasi cha kuwashangaza hata wale waliomtishia wakidhani kwamba, ni mtu aliyekuwa anatafuta sifa na “ujiko” katika utume!

Kardinali Angelo Amato anahitimisha mahojiano haya maalum kwa kusema, leo hii Kanisa linawahitaji waamini walei, mapadre na watawa watakatifu! Mwenyeheri John Sullivan anawaalika waamini wote kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu ili kuambata mambo matakatifu. Ni changamoto ya kuondokana na ubinafsi kwa kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo, jambo muhimu sana katika maisha ya Kikristo! Injili ya upendo ni ngazi ya kupandia kwenda mbinguni!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.