2017-05-12 11:53:00

Kiini cha Siri ya Fatima: huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na Radio Vatican wakati huu Baba Mtakatifu Francisko anapofanya hija ya 19 ya Kitume kwenye madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima, nchini Ureno, kuanzia tarehe 12 hadi 13 Mei 2017 anasema, hakuna tena siri ya Fatima iliyofichwa na ambayo haijafichuliwa. Ujumbe wa Bikira Maria unafumbatwa katika: sala, toba, wongofu wa ndani, amani na mshikamano kati ya watu. Itakumbukwa kwamba, hija hii inaongozwa na kauli mbiu “Papa Francisko mjini Fatima 2017 pamoja na Bikira Maria kama mahujaji wa matumaini na amani”.

Baba Mtakatifu anafanya hija hii kuonesha upendo na ibada yake kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu, ndiyo maana daima anaanza na kuhitimisha hija zake za kitume kwa maombezi na tunza ya Bikira Maria, Mama ambaye uzoefu na mang’amuzi yake ni chachu ya imani, matumaini na mapendo kwa watu wa Mungu kama inavyojidhihirisha katika utenzi wake wa “Magnificat”. Bikira Maria wa Fatima, miaka 100 iliyopita aliwatokea Watoto wa Fatima na wala hakujionesha kwa wenye nguvu, bali akawakweza wanyonge na kuwainua juu kama “mlingoti wa bendera”. Bikira Maria akawaangalia kwa jicho la upendo, hawa wadogo na wanaohesabiwa kuwa wanyonge, ili kuwapatia ujumbe makini kwa walimwengu kuhusu umuhimu wa toba, wongofu wa ndani na amani duniani!

Kardinali Parolin anasema, hiki kilikuwa ni kipindi cha Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, yaani ilikuwa ni “patashika nguo kuchanika”! Hapa kilichokuwa kinatawala katika mwaka 1917 ni vita, chuki, uhasama na kulipizana kisasi. Papa Benedikto wa kumi na tano akasema, hii ilikuwa ni Vita isiyokuwa na “kichwa wala miguu”. Bikira Maria wa Fatima akajitokeza na kuanza kuwasha moto wa upendo, toba na msamaha; sadaka na majitoleo kwa wenye shida na mahangaiko mbali mbali. Mkazo ukawa ni tunu msingi za maisha ya Kiinjili na kiutu dhidi ya kuporomoka kwa utu wema, upendo na mshikamano kati ya watu wa Mataifa. 

Mwaliko kwa Familia ya Mungu nchini Ureno na dunia katika ujumla wake, wakati huu ni kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ni mwaliko wa kumwilisha tunu msingi za Kiinjili katika uhalisia wa maisha ya watu kama kielelezo makini cha imani tendaji katika maisha ya watu! Amani, utulivu, upendo na mshikamano ndiyo mkazo unaotolewa na Mama Kanisa wakati huu wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima.

Kardinali Parolin anakaza kusema, ujumbe wa Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima, ulikuwa ni toba na wongofu wa ndani, kwa kuwataka waamini kuchuchumilia utakatifu wa maisha! Madhabahu ni mahali muafaka pa toba na wongofu wa ndani; ni mahali pa kuonja huruma na upendo wa Mungu kwani kwa kawaida madhabahu ni “kiliniki ya magonjwa ya maisha ya kiroho”! Kwa kutambua kwamba, hakuna lisilowezekana mbele ya Mwenyezi Mungu. Madhabahu yanakuwa ni mahali pa waamini kukua na kukomaa  katika maisha ya kiroho, tayari kujibu kwa ujasiri kama alivyofanya Bikira Maria kwa kusema, “Tazama mimi ni mtumishi wa Bwana, nitendewe kama ulivyonena”! Hapa mwamini anajiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu na kumwalika kutembea pamoja naye katika hija ya maisha yake ya kiroho, tayari kushiriki katika mchakato wa kuleta mageuzi katika maisha ya walimwengu kwa njia ya chachu ya Injili ya upendo, wema na huruma ya Mungu kwa waja wake. Kila kitu kinawezekana kwa mwamini anayekimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria.

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kunako mwaka 2010 wakati wa hija yake ya kitume kwenye Madhabahu ya Bikira Maria alisikika akisema, utume wa kinabii uliotolewa kwa Watoto wa Fatima bado ni endelevu! Huu ni ujumbe wa Pasaka unaojikita katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, kiini cha imani ya Kanisa! Kristo bado ni hai na anatembea pamoja na Kanisa lake. Hakuna tena siri nyingine kutoka Fatima, kwani kiini cha ujumbe wa Bikira Maria ilikuwa ni imani ya Kanisa Katoliki; kwa kuwa na maana na uelewa mpya wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!

Kardinali Parolin anakaza kusema, hija ya maisha ya waamini, daima inaongozwa na kuimarishwa na tunu msingi za Kiinjili. Kanisa linahamasishwa na Bikira Maria kuendelea kuwa ni shuhuda na chombo cha toba, wongofu wa ndani, haki, amani na mshikamano kati ya watu! Kanisa  litaendelea kusoma alama za nyakati na kuzifafanua kwa mwanga wa Injili; kuzima kiu na kujibu matamanio halali ya watu wa nyakati hizi, dhamana na changamoto iliyovaliwa njuga na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Mwenyezi Mungu amemwokoa mwanadamu kutoka katika kongwa la utumwa wa kihistoria na kumwonesha matumaini mapya yanayofumbatwa katika Injili ya upendo, haki na amani. Huu ndio ujumbe wa kinabii unaotolewa na Mama Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha hija hii ya kichungaji kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima kwa kuwatangaza Wenyeheri Francis na Yacinta Marto kuwa ni watakatifu. Huu ni mwaliko kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuiga mfano wa unyofu wa Watoto wa Fatima, ili kuzama katika tunu msingi za Kiinjili kwa njia ya Moyo Safi wa Bikira Maria usiokuwa na doa! Huu ni moyo ambao ni chemchemi ya upendo na huruma ya Mungu kwa binadamu. Kanisa linatambua ujasiri huu unaobubujika kutoka katika ukweli wa Fumbo la Msalaba, kuwa ni kiini cha utakatifu wa Francis na Yacinta Marto!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.