2017-05-12 18:31:00

Huduma katika utumishi!


Jumapili ya Nne ya Kipindi cha Pasaka, tulialikwa na mama kanisa kuomba na kusali kwa ajili ya miito mitakatifu. Katika neno la Mugu dominika hii ya leo tunasikia habari juu ya haja ya ushuhuda kati ya mitume na wahudumu katika kutumikia, tunasikia pia mwaliko wa Petro wa kumwendea Bwana na haja ya kina Tomaso na Filipo ya kuoneshwa Baba na kuoneshwa njia. Dhamira hii inayotuongoza ya utumishi iko wazi zaidi katika somo la kwanza, yaani huduma katika utumishi. Katika somo la pili, Mtume Petro anawahimiza waliobatizwa waende wakafanye kazi ya Bwana,  wamwendee yeye, yaani ubatizo waliopokea uwe sababu ya utumishi. Katika somo la Injili tunamsikia Yesu akisema aniaminiye atafanya kazi niifanyayo mimi na anasema anamtukuza Baba kwa kazi azifanyazo kwa ajili ya watu wa Mungu.

Ndugu wapendwa, sote twajua jinsi ilivyo vigumu kuamini na swali linalofuata ni hili – Je, inawezekana? Ila jambo moja na la faraja ni kwamba tunatambua kuwa Mungu hadanganyi wala hadanganyiki. Kuhusu ufuasi na kuamini, Mtume Paulo katika Gal. 5:1,13-18 anatukumbusha kuwa ni roho ya Kristo inayotuita tuwe huru na ndiyo roho inayotuwezesha kutoa jibu katika huo ufuasi. Wito wa ufuasi hautegemei kusikia sauti ya roho zetu bali twaitwa kusikiliza sauti ya roho yake Kristo.

Shida ya mwanadamu ni kwamba anataka uhakika wa kila jambo afanyalo. Pia anataka aishi na Mungu kimkataba na kama ni makubaliano ya malipo basi hicho kiasi cha fedha kiandikwe mara moja. Ahadi ya Mungu hakika ni zaidi ya kile tunachotaka kionekane. Binadamu anataka kusawazisha maagano yake na Mungu kama anavyosawazisha na mwanadamu mwenzake. Tabia mojawapo ya mwanadamu ni kudai toka kwa mwenzake kile ambacho hata yeye mwenyewe hawezi kukitoa. Tukumbuke kuwa ahadi ya Yesu ni tofauti na anasema wazi niko kwa Baba na Baba ndani yake – mimi ndimi njia na ukweli na uzima na mtu haji kwa Baba ila kwa njia yake.

Leo hii tunaalikwa kuwa na imani katika ahadi hii. Tunaalikwa kutofautisha ahadi na agano kati yetu na kati ya Mungu. Aidha tukumbuke kuwa hakuna ahadi na ushuhuda wa kweli zaidi ya ule wa Mungu kuja kwetu (umwilisho) na kukaa kwetu, nasi tukapata wokovu na uzima wa milele. Mt. Agustino anasema hakuna kikubwa zaidi ya huruma ya Mungu, kwayo tunapata msamaha na upatanisho naye na hivyo hakuna haja ya kupiga kelele, tuishi hilo.

Ndiyo maana leo Yesu anasema msiogope, nyumbani kwa Baba kuna makao tele. Hapa ulimwenguni siyo makao yetu. Inaonekana mitume wanapata wasiwasi kwamba huyu mfufuka akiondoka hali itakuwaje. Na Yesu anasema msifadhaike, mwaminini Mungu, niaminini na mimi pia.  Hatuna budi leo kujiuliza juu ya uimara wa imani yetu. Je, sisi tunaamini au tumejishikamanisha zaidi katika ahadi zipi? Za kibinadamu au za kimungu? Au kila mtu anajiamini peke yake tu? Huu mwaliko wa Yesu anayesema aniaminiye atafanya kazi zangu una nafasi gani katika maisha ya mwamwini?

Bila shaka hata sisi leo tuna hicho kishawishi cha kutaka kumshika Yesu kwa mikono yetu au kumwona kwa namna tunayotaka sisi. Mahangaiko ya watu mbalimbali hasa wale wanaohama dhehebu hili au lile na namna mbalimbali za maombi huthibitsha hali hiyo. Sisi tunaacha kuishi mwaliko halisi wa Kristo na tunataka mtu atakayesema Yesu huyu hapa sasa zaidi ya alivyosema tayari kwamba nipo kati yenu. Tukumbuke kuwa kwa fumbo la umwilisho, Yesu tayari yupo kati yetu. Na kuna watu walioishi, wanaoishi na watakaoishi ushuhuda huo.

Wakati wa maziko ya Baba Mtakatifu Yohane Paulo II yalisikika maneno kama haya ya ushuhuda hai toka waombolezaji wakisema mtakatifu haraka, yaani afanywe mtakatifu haraka na kama wanasema hivyo ina maana kuwa wanatambua na kukubali uwepo wa Mungu aliye hai. Wengine walisikika wakisema wewe uliyependa na kuiishi mbingu hapa duniani tusalimie Mungu. Haya ni maneno mazito ya ushuhuda. Wanamtuma mtu wao ambaye aliishi mbingu amsalimie Mungu wanayemwamini. Kama nasi tukiishi maisha ya ushuhuda basi tutakuwa tumezima kiu ya kina Filipo na Toma ambao bado wapo wengi kati yetu. Katika sehemu ya sala ya mwanzao ya ibada ya leo tunasali – utusikilize kwa wema sisi wanao, ili katika kumwamini Kristo, tupate uhuru wa kweli na urithi wa milele. Na hii iwe sala yetu ya leo.

Tumsifu Yesu Kristo.

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.