2017-05-12 12:10:00

Fatima: Shindeni dhambi na ubaya wa moyo kwa toba na wongofu wa ndani


Familia ya Mungu nchini Ureno inapenda kumwimbilia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani, kwa neema na baraka za uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko kati yao, wakati huu Kanisa linapoadhimisha kilele cha Jubilei ya Miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima: Francis, Yacinta Marto na Lucia, dos Santos. Baba Mtakatifu hujaji wa matumaini na amani, anasindikizwa na Kanisa zima katika maadhimisho ya Jubilei hii ambayo ni muhimu sana kwa familia ya Mungu ndani na nje ya Ureno. Hili ni tukio la kanisa la kiulimwengu anasema, Askofu Antonio Marto, wa Jimbo Katoliki Leiria-Fatima nchini Ureno.

Familia ya Mungu nchini Ureno inampongeza Baba Mtakatifu kwa Ibada yake kwa Bikira Maria na kwa namna ya pekee wakati huu, anapowatangaza Wenyeheri Francis na Yacinta Marto kuwa watakatifu, tarehe 13 Mei 2017, kama alivyowatokea Bikira Maria wa Fatima, miaka 100 iliyopita. Hawa walikuwa ni watoto wachungaji, lakini Bikira Maria akawatumia kuwa ni chombo cha kufikishia ujumbe wake wa amani, toba, sala, upendo na mshikamano kwa watu wa Mataifa.

Ni mwaliko wa kufanya hija ya imani, matumaini na mapendo, kwa kufuata nyayo za Watoto wa Fatima, ili kutangaza na kushuhudia Injili ya amani dhidi ya utamaduni wa kifo, uliosababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao kutokana na Vita Kuu ya Kwanza na ya Pili ya Dunia. Kanisa linawakumbuka watoto wake wote walioteseka kutokana na dhuluma na nyanyaso za kidini huko Russia na katika nchi za Kikomunisti kiasi kwamba, damu ya mashuhuda hawa wa imani, imekuwa ni chemchemi ya Ukristo thabiti huko Ulaya ya Mashariki. Waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, wanahimizwa na Mama Kanisa kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya amani duniani.

Kamwe wasikatishwe tamaa na ubaya watu na kuona kana kwamba, hii ni sehemu ya maisha ya binadamu! Inawezekana kabisa kushinda dhambi na ubaya wa moyo kwa njia ya toba na wongofu wa ndani; kwa sala na malipizi ya dhambi. Hii ni changamoto ya kusimama kidete kutangaza Injili ya amani, haki msingi za binadamu; kwa kukuza na kudumisha majadiliano katika ukweli na haki; sanjari na kuendeleza upatanisho, ili kuendeleza kazi ya ukombozi wa mwanadamu. Hii ndiyo dhamana ambayo Mwenyezi Mungu anapenda kuwapatia walimwengu katika nyakati hizi.

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, kunako mwaka 2010 aliwataka waamini kushinda dhambi na ubaya wa moyo kwa kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, kwa kutimiza malipizi ya dhambi; kwa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa upendo. Papa Francisko bado anawaonya walimwengu kwamba, hata leo hii bado dunia inakabiliwa na vitisho vya utamaduni na hofu ya kifo kutokana na vita, nyanyaso, dhuluma na ukosefu wa haki msingi za binadamu, sehemu mbali mbali za dunia. Kuna haja kwa walimwengu kushikamana ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu; kujisadaka kwa ajili ya huduma makini kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi badala ya kujenga kuta za utengano na ubaguzi. Mwishoni mwa ujumbe wa Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima unasema, hatimaye, Moyo Safi wa Bikira Maria utashinda na amani itaweza kurejeshwa tena duniani, tafsiri makini iliyotolewa na Papa Mstaafu Benedikto XVI, kwani Bikira Maria ni kielelezo makini cha huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Upendo utashinda mantiki ya vita na kinzani, kwani ujumbe wa Fatima unafumbatwa katika matumaini na amani duniani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.