2017-05-11 14:34:00

Imani na kanuni maadili vinafahamika vyema katika hija ya kiroho!


Familia ya Mungu daima imekuwa katika hija ya ukomavu wa imani unaofumbatwa katika historia ya wokovu tangu katika Agano la Kale na utimilifu wake umefikiwa katika Agano Jipya kwa njia ya Kristo Yesu. Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, ameendelea kujifunua mbele ya watu wake katika historia na maisha ya mwanadamu. Ni historia inayojikita kwa Waisraeli waliokombolewa kutoka utumwani, akawaongoza Jangwani kwa muda wa miaka arobaini ili kuelekea katika utimilifu wa nyakati. Ni hija ambayo iliwajumuisha watakatifu na wadhambi, hadi pale Mwenyezi Mungu alipowaletea Waisraeli Mwokozi, ndiye Kristo Yesu kutoka katika uzao wa Daudi, Mwana wa Yese aliyeupendeza moyo wa Mungu na kutekeleza mapenzi yake.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 11 Mei 2017 katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kristo Yesu baada ya kuhitimisha kazi ya ukombozi kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, akawapelekea Roho Mtakatifu ili kuwakumbusha yale mambo msingi yaliyofundishwa na Yesu; kufahamu ujumbe uliokuwa unafumbatwa katika Mafundisho haya sanjari na kuliendeleza Kanisa. Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, Kanisa ni Jumuiya ya waamini watakatifu na wadhambi; Kanisa linatembea kati ya neema na dhambi, lakini linasimamiwa na kuongozwa na Roho Mtakatifu.

Baba Mtakatifu anasema, kuna wakati katika historia ya mwanadamu utumwa na adhabu ya kifo vilikuwa vinakubalika mbele ya jamii. Lakini, kwa njia ya safari ya imani katika Kristo Yesu, kwa kuongozwa na Amri za Mungu na Kanuni maadili, sasa mambo ya utumwa na adhabu ya kifo ni dhambi ya mauti. Utumwa na mifumo yake yote hata katika ulimwengu mamboleo ni uhalifu dhidi ya utu na heshima ya binadamu. Katika mfumo wa utumwa, binadamu anageuzwa kuwa ni bidhaa inayoweza kuuzwa na kununuliwa sokoni!

Baba Mtakatifu anawaangalisha waamini kwamba, hata leo hii, bado kuna utumwa mamboleo na adhabu ya kifo inayokwenda kinyume kabisa cha Injili ya uhai! Hija ya imani, inawasaidia waamini kujizatiti katika kanuni maadili, imani na utu wema. Kuna watakatifu wanaofahamika mbele ya Mama Kanisa, lakini pia kuna watakatifu waliojificha, lakini wanafahamika mbele ya Mwenyezi Mungu peke yake. Hawa ndio wanaolisaidia Kanisa kusonga mbele, hadi pale Kristo Yesu, atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu na wala Ufalme wake hautakuwa na mwisho!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Mwenyezi Mungu amependa watu wake waweze kumfahamu kwa kutembea, ili kamwe wasigeuke kuwa watumwa na kutopea katika imani, mapendo na matumaini. Lakini, ikumbukwe kwamba, kila mtu ana ukamilifu wa nyakati zake. Hapa kuna haja ya kuwakumbuka: mitume na wahubiri wa kwanza kwanza waliojisadaka ili kuhakikisha kwamba, Mwenyezi Mungu anafahamika na kupendwa na watu wake, daima wakiwa katika safari ya maisha ya kiroho. Yesu Kristo alimtuma Roho Mtakatifu ili kuwasaidia waamini kuendelea kutembea katika maisha ya kiroho, kielelezo makini cha huruma ya Mungu kwa binadamu.

Huu ndio mwelekeo wa utimilifu wa nyakati kwa kila mtu binafsi. Jambo la msingi hapa ni kujiuliza na kuangalia ikiwa kama kweli ahadi za Mungu zimefumbatwa katika hija ya maisha ya watu wake na kama Kanisa bado linaendeleza mchakato wa hija ya maisha ya kiroho, ili hatimaye, kuweza kukutana na Kristo Yesu. Jambo la msingi kwa waamini  ni kuona aibu ya dhambi wanazotenda, wawe na ujasiri wa kutubu na kuomba msamaha, ili kujiweka tayari kukutana na Kristo Yesu, uso kwa uso wakati utakapowadia. Waamini wajitahidi kuchunguza dhamiri zao na hatimaye, kuungama dhambi zao vyema, ili kuambata huruma ya Mungu katika maisha yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.