2017-05-11 07:40:00

B. Maria wa Fatima: bado kuna haja ya toba, wongofu na amani duniani!


Mama Kanisa anapoadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima yaani: Francis, Yacinta Marto na Lucia dos Santos aliwahimiza kwa namna ya pekee kabisa kusali Rozari Takatifu ambayo kimsingi ni muhtasari wa historia nzima ya kazi ya ukombozi. Bikira Maria aliwataka Watoto wa Fatima kuombea toba na wongofu wa ndani sanjari na amani duniani! Baba Mtakatifu Francisko, anatarajia kuhitimisha maadhimisho haya kwa kuwatangaza Wenyeheri Francis na Yacinta Marto kuwa Watakatifu katika hija yake kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima inayoongozwa na kauli mbiu “Papa Francisko mjini Fatima pamoja na Bikira Maria kama mahujaji wa matumaini na amani”.

Baba Mtakatifu katika hija yake kwenye Madhabahu ya Fatima anaongozana na Kardinali Josè Saraiva Martins, Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu. Kardinali Martins, hivi karibuni alimwakilisha Baba Mtakatifu Francisko katika Kongamano la Bikira Maria Kimataifa lililofanyika kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima, Mwezi Septemba 2016 kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima.

Katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, ujumbe wa Bikira Maria bado ni hai sana kwa watu wa nyakati hizi. Ni ujumbe unaokazia umuhimu wa imani inayopaswa kumwilishwa katika matendo. Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima aligusia umuhimu wa imani katika maisha ya waamini, changamoto kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanapyaisha imani yao kwa Kristo na Kanisa lake kwa njia ya: Sakramenti za Kanisa, Tafakari makini ya Neno la Mungu, Katekesi pamoja na kuhakikisha kwamba, imani hii inamwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo cha imani tendaji! Changamoto katika ulimwengu mamboleo anasema Kardinali Josè Saraiva Martins ni kutopea na utepetevu wa imani, tabia ambayo inataka kumfanya mwanadamu kumweka Mwenyezi Mungu pembezoni kabisa mwa maisha na vipaumbele vyake!

Ujumbe wa pili kutoka kwa Bikira Maria wa Fatima ni toba na wongofu wa ndani. Anawaalika waamini kumwongokea Mwenyezi Mungu pamoja na jirani zao, ili kujenga na kudumisha umoja, upendo, mshikamano na udugu. Lengo kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko ni kujenga madaraja ya watu kukutana, ili kufahamiana na hatimaye, kusaidiana katika hija ya maisha, kwani wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Watu wote wanapaswa kujisikia kuwa ni sehemu ya Familia ya Mungu duniani licha ya tofauti zao msingi! Ujumbe wa tatu ambao Bikira Maria wa Fatima anapenda kukazia hata kwa watu wa nyakati hizi ni kuombea amani duniani! Hii ni changamoto ambayo imefanyiwa kazi na Mapapa wengi katika kipindi cha Miaka 100 iliyopita, lakini kwa namna ya pekee kabisa wakati wa uongozi wa Yohane Paulo II na kwa sasa Baba Mtakatifu Francisko kutokana na hatari ya uwepo wa Vita Kuu ya tatu ya Dunia inayopiganwa sehemu mbali mbali za dunia pamoja na hatari iliyopo ya kufumuka kwa mashambulizi ya silaha za kinyuklia, baada ya Mataifa makubwa duniani yanayomiliki, kutengeneza na kufanya majaribio ya silaha hizi, ili “kutunishana misuri” lakini kwa hofu na hatari ya familia ya Mungu duniani!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, dunia mamboleo haina uwezo wa kustahimili kishindo cha athari za mashambulizi ya kinyuklia duniani! Kumbe, majadilano, diplomasia na suluhu ya amani ni njia muafaka ya changamoto na vitisho vya mashambulizi na vita duniani! Kardinali Josè Saraiva Martins, Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu anasema, Bikira Maria bado anaendelea kuwahimiza waamini katika ulimwengu mamboleo kusali Rozari Takatifu, sala ya waamini wa kawaida, muhtasari wa historia nzima ya ukombozi inayofumbatwa katika maisha na utume wa Kristo Yesu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.