2017-05-10 15:14:00

Yaani, asiyekuwa na mwana aeleke jiwe! Fatima kumekucha!


Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto watatu wa Fatima yaani Francis, Yacinta Marto na Lucia dos Santos kati ya tarehe 13 Mei hadi tarehe 13 Oktoba 1917 yanapambwa kwa namna ya pekee na taarifa kwamba, Wenyeheri Francis na Yacinta Marto, waliotangazwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako tarehe 13 Mei 2000 wakati Kanisa lilipokuwa linaadhimisha Jubilei kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo, wamo kwenye orodha ya watakatifu watakaotangazwa hivi karibuni na Kanisa baada ya Baba Mtakatifu Francisko kuridhia hatua ya mchakato wao hivi karibuni. Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kushiriki katika kilele cha maadhimisho haya huko Fatima, Ureno kuanzia tarehe 12 hadi 13 Mei 2017. Kauli mbiu inayoongoza hija hii ni “Papa Francisko mjini Fatima 2017 pamoja na Bikira Maria kama mahujaji wa matumaini na amani”.

Ikumbukwe kwamba, ujumbe wa Bikira Maria wa Fatima unafumbatwa kwa namna ya pekee kabisa katika mwaliko wa toba na wongofu wa ndani; maisha ya sala na tafakari ya Rozari ambayo kimsingi ni muhtasari wa historia nzima ya ukombozi wa mwanadamu; ni ujumbe wa matumaini yanayoonesha kwamba, daima Mwenyezi Mungu yuko kati pamoja na watu wake. Hii ni hija ya imani na mshikamano kati ya watu wa Mataifa. Miaka kumi iliyopita, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alisikika akisema, ujumbe wa Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima ni kati ya matukio makuu yaliyotikisa na kuimarisha Ibada kwa Bikira Maria wa Fatima.

Ibada hii ikapewa kipaumbele cha pekee na Mtakatifu Yohane Paulo II, ambaye mwanzoni kabisa mwa utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro akakumbana na jaribio la kutaka kumuua kwa kupigwa risasi kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Hii ilikuwa ni tarehe 13 Mei 1981. Mtakatifu Yohane Paulo II anaamini kabisa kwamba, aliweza kusalimika na kifo kutokana na ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Fatima, kama ambavyo ilikuwa imeelezewa katika Siri ya tatu ya Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima na kutangazwa na Sr. Lucia kunako mwaka 1944. Papa Yohane Paulo II akachukua ile risasi na kuiweka kwenye Sanamu ya Bikira Maria wa Fatima, nchini Ureno.

Ujumbe wa Bikira Maria kwa watoto watatu wa Fatima ulikuwa ni mwaliko wa kuuweka wakfu ulimwengu wote chini ya ulinzi na tunza ya Moyo Safi wa Bikira Maria, Ibada iliyoadhimishwa kunako tarehe 25 Machi 1984. Kardinali Joseph Ratzinger wakati huo akiwa ni Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa alichapisha siri zote za Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima na kufafanua siri hii kwa ufundi mkubwa wa kitaalimungu ili kuonesha na kushuhudia utakatifu wa maisha ya Yohane Paulo II na utume wa Kanisa ulimwenguni. Akawakumbusha walimwengu kwamba, matukio mbali mbali yanayoendelea kutendeka duniani yako chini ya dhamana ya walimwengu na kwamba, watu wamepewa baraka ya kujenga dunia inayojikita katika haki, umoja,upendo na udugu.

Watoto watatu wa Fatima walimtambua Bikira Mari wa Fatima kuwa ni Malkia wa Rozari aliyekuwa amejaa neema na baraka, akang’ara kama mwanga wa jua, huku akiwataka watoto hao tarehe 13 Mei 1917 kusali na kutafakari Rozari Takatifu, muhtasari wa kazi kubwa ya ukombozi iliyofanywa kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. Bikira Maria akawaonesha watoto wa watatu wa Fatima dhambi na madhara yake katika maisha ya mwanadamu duniani, changamoto na mwaliko ukawa ni kutubu na kumwongokea Mungu; kuvumilia kwa saburi mateso na mahangaiko ya dunia. Waamini wanapaswa kusali kwa ajili ya kuombea roho za watu walioko toharani, kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji kama anavyokaza kusema Mtakatifu Paulo, Mtume na mwalimu wa mataifa. Hii ni hija ya Kanisa inayojikita katika mshikamano wa dhati na binadamu wote wanaotakiwa kutubu na kumwongokea Mungu, ili watu hawa waweze kupata maisha na uzima wa milele. Itakumbukwa kwamba, hiki kilikuwa ni kipindi cha mahangaiko baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia.

Mkazo ukawa ni kwa ajili ya kuombea amani na usalama kwani Kanisa lilikuwa linakabiliwa na vitisho, dhuluma na nyanyaso kutoka kwa Urussi. Lakini, kwa bahati mbaya, toba na wongofu wa ndani haukufanyika kama alivyokuwa ameagiza Bikira Maria wa Fatima, haki, amani, upendo na mshikamano vikatoweka na mara ikafumuka tena Vita ya Pili ya Dunia. Ujumbe wa Bikira Maria kwa watoto wa Fatima unasimikwa katika toba, wongofu wa ndani, sala, matumaini na mshikamano unaooneshwa katika maisha na utume wa Kanisa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.