2017-05-10 12:10:00

Ujumbe wa B. Maria wa Fatima: Sala, Toba na Wongofu wa ndani!


Kardinali Giovanni Battista Re katika tafakari yake kuhusu maadhimisho ya Jubilei ya miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima: Francis, Yacinta Marto na Lucia dos Santos, tarehe 13 Mei 1917 na kujitambulisha kuwa ni Bikira Maria wa Rozari Takatifu aliwakabidhi watoto hawa ujumbe wa matumaini kwa binadamu wote, akiwataka wajizatiti katika kupambana na ubaya, kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia imani kwa Kristo na Kanisa lake. Ikumbukwe kwamba, matukio ya Bikira Maria kuwatokea watu mbali mbali si sehemu ya ufunuo wa imani ya Kanisa kama inavyofundishwa katika Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa!

Matukio haya yanachukuliwa kuwa ni ufunuo binafsi wa Mama wa Mungu kwa baadhi ya watu. Kanisa limekuwa makini sana kuhusu matukio kama haya, lakini pia pale ambapo limejiridhisha, limeruhusu waamini kufanya Ibada na hija kwa Bikira Maria kama ilivyo kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima, huko Ureno, yakabahatika kutembelewa na Mapapa wanne katika kipindi cha miaka 100 iliyopita! Matukio haya ni muhimu kwani yanawasaidia waamini kutambua utashi na mpango wa Mungu katika maisha yao! Daima wanahamasishwa kumpenda Mwenyezi Mungu na kuishi vyema Ukristo wao kwa kuzingatia Amri kumi za Mungu ambazo ni kanuni msingi za maisha, maadili na utu wema.

Kardinali Giovanni Battista Re anasema, ujumbe wa Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima unaweza kufupishwa kwa maneno makuu matatu: Sala, Toba na Wongofu wa ndani! Sala ni majadiliano ya kina kati ya mwamini na Muumba wake; majadiliano yanayomwongoza mwamini kuelekea katika maisha ya uzima wa milele. Waamini wanachangamotishwa na Mama Kanisa kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu kwa kuwa na mwelekeo mpya katika maisha yao. Bikira Maria wa Fatima anawaalika waamini kuchuchumilia utakatifu na kuendelea kusali kwa ajili ya toba na wongofu wa ndani; kwa kujiweka wakfu kwa Moyo wake usiokuwa na doa! Bikira Maria anawaalika waamini kusali Rozari Takatifu ili kuombea amani duniani! Hii ni cangamoto endelevu hata kwa watu wanaoishi katika ulimwengu mamboleo!

Ujumbe wa Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima unafumbatwa kwa kiasi kikubwa katika Injili, kiasi kwamba, Fatima inakuwa ni shule ya imani na ushuhuda wa maisha ya Kikristo, na Bikira Maria ndiye Mwalimu wake mkuu! Anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa na imani kwa Kristo Yesu na kamwe wasikatishwe tamaa na Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia; majanga katika maisha ya watu; tawala za kifashisti na kikomunisti, tawala ambazo zimedhalilisha haki msingi, utu na heshima ya binadamu; kiasi hata cha kutaka kumng’oa Mungu katika maisha na vipaumbele vya waamini. Kilio cha waamini kilikuwa ni kumwomba Mwenyezi Mungu asimame mwenyewe na kujitetea!

Ujumbe wa Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima ulijikita zaidi katika Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia na Vita Kuu ya Pili ya Dunia; vita ambavyo vimesababisha madhara makubwa kwa maisha ya watu sehemu mbali mbali za dunia. Siri zote za Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima zikafunuliwa hadharani kunako Mwaka 2000 kwa kuonesha madhara makubwa yaliyosababishwa na Urussi kwa wakati ule kwa kupandikiza “ndago” za Ukanimungu; dhuluma, nyanyaso na mauaji ya kikatili dhidi ya Wakristo! Katika kipindi hiki cha utawala wa giza na chuki dhidi ya imani ya Kikristo, hapa kukaibuka makundi ya Wakristo waliosimama imara kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Jeuri ya maisha yao ya kiroho!

Mtakatifu Yohane Paulo II, kunako tarehe 13 Mei 1981 akiwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican akapigwa risasi katika jaribio la kutaka kumuua na kumfutilia mbali kutoka katika uso wa dunia! Lakini akasalimika na kwamba, huu ni muujiza wa pekee kabisa aliotendewa na Bikira Maria wa Fatima. Akaamuru hata ile Siri ya Tatu ya Fatima iwekwe hadharani! Ni siri ambayo ilionesha kwamba kulikuwa na mapambano makubwa dhidi ya Kanisa. Mtakatifu Yohane Paulo II akachukua risasi iliyotoka mwilini mwake na kuiweka kwenye taji ya nyota kumi na mbili zinazopamba kichwa cha Bikira Maria wa Fatima. Tarehe 25 Machi 1984 Mtakatifu Yohane Paulo II akauweka ulimwengu na kwa namna ya pekee kabisa, Urussi chini ya ulinzi na tunza ya Moyo Safi wa Bikira Maria.

Kardinali Giovanni Battista Re anasema, Ujumbe wa Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima ni endelevu hata kwa watu wa nyakati hizi kwani unafumbatwa katika Injili ya Kristo na Kanisa lake; Unahimiza Ibada kwa Bikira Maria, Toba, Wongofu wa ndani, Utakatifu wa maisha na umuhimu wa kusali Rozari Takatifu ili kuombea amani duniani. Waamini watambue daima kwamba, hata katika shida na mahangaiko yao, Mwenyezi Mungu daima yuko pamoja nao hadi utimilifu wa dahali! Bikira Maria anataka kuwaachia watoto wake, ujumbe wa matumaini, wokovu, amani na kwamba, Mwenyezi Mungu apewe kipaumbele cha kwanza katika maisha ya mwanadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.