2017-05-09 15:16:00

Jubilei ya Miaka 100 ya B. Maria wa Fatima: mkazo: Uinjilishaji mpya!


Kanisa linaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima, yaani Francis, Yacinta Marto na Lucia dos Santos. Baba Mtakatifu Francisko kwa heshima ya Bikira Maria, ameamua kuwatangaza Wenyeheri Francis na Yacinta Marto kuwa watakatifu wakati wa hija yake ya kitume nchini Ureno kuanzia tarehe 12- 13 Mei 2017. Hija hii inaongozwa na kauli mbiu “Papa Francisko mjini Fatima 2017 pamoja na Bikira Maria kama mahujaji wa matumaini na amani”. Ujumbe wa Bikira Maria kwa watoto hawa ulikuwa ni toba, wongofu wa ndani na matumaini kwa binadamu kwa kutambua kwamba, kweli Mwenyezi Mungu anasikia kilio chao na kukijibu kwa wakati wake.

Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania, limeandika ujumbe wa matumaini kwa Familia ya Mungu nchini humo, ukiwataka wamjifunze Yesu kupitia shule ya Bikira Maria, ili kuwa na upendeleo wa pekee kwa maskini, wanyonge na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; wadhambi na wale wanaotengwa kutokana na sababu mbali mbali za maisha; wagonjwa na watu wanaoteseka: kiroho, kimwili, kimaadili na kiutu bila kuwasahau wale waliovunjika na kupondeka moyo! Maaskofu wanasema, wote hawa wanahitaji ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Fatima, ili hatimaye, aweze kuyafikisha maombi yao mbele ya Mwanaye Mpendwa, Yesu Kristo!

Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania linapenda kujikabidhi tena kwa ulinzi na tunza ya Bikira Maria, kwa sala aliyotumia Baba Mtakatifu Francisko tarehe 13 Oktoba 2013 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Maaskofu wanawaalika waamimini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuungana pamoja na Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake ya kiroho huko Fatima, nchini Ureno kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima. Ibada kwa Bikira Maria wa Fatima imejikita katika moyo wa waamini wa kawaida kabisa, kiasi hata cha kuleta mvuto kwa viongozi wakuu wa Kanisa, kwa kuona jinsi ambavyo watu walimkimbilia Bikira Maria katika imani na matumaini katika shida na mahangaiko yao.

Wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima, Mwenyeheri Paulo VI alikwenda kuhiji huko. Lakini, Mtakatifu Yohane Paulo II alikuwa na uhusiano na ibada ya pekee kabisa kwa Bikira Maria wa Fatima katika maisha na utume wake, kiasi cha kujikabidhi kwa huyu Mama. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alitembelea madhabahu haya kunako mwaka 2010. Huyu ndiye aliyefafanua kuhusu siri za Fatima na kuziweka hadharani. Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania linawaalika watu wa Mungu nchini humo kusoma ujumbe wa Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima katika mwanga wa historia ya ukombozi. 

Ujumbe huu uwe ni changamoto na mwaliko wa kuzama zaidi katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaojikita katika toba, wongofu wa ndani na ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo! Lugha aliyotumia Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima ilikuwa ni lugha ya upendo inayoeleweka na kufahamika na wengi, changamoto na mwaliko kwa waamini ni kuwa kweli vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao. Toba na wongofu wa ndani pamoja na maisha ya sala ni mambo msingi ambayo yalikaziwa sana na Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima, yaani: Francis, Yacinta Marto na Lucia dos Santos.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.