2017-05-09 10:44:00

Jitahidini kuwa wachamungu na raia wema kwa nchi zenu!


Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini, hivi karibuni ameongoza ujumbe wa Vatican kwenye kongamano lililoandaliwa na Taasisi ya Elimu ya Mfalme wa Morocco huko Rabat. Ujumbe wa Morocco uliongozwa na Abdeljalil Lahjomri, Katibu wa kudumu wa Taasisi ya Elimu ya Mfalme wa Morocco. Washiriki wa kongamano hili wamepembua kwa kina na mapana maana ya kuwa waamini na raia katika ulimwengu ambao unakabiliwa na mabadiliko makubwa, mintarafu dini ya Kiislam na Kikristo. Baada ya kusikiliza hoja zilizowasilishwa na wawezeshaji mbali mbali katika kongamano, wajumbe, wakaamua kutoa tamko lao la pamoja!

Kwa pamoja wanakazia umuhimu wa kutenganisha masuala ya maisha ya kidini na uongozi wa kisiasa, ili kuepuka uwezekano wa siasa au dini kutumiwa kwa ajili ya mafao ya watu binafsi. Waamini wanapaswa kutambua kwamba, wanayo imani yao, lakini pia wanawajibika kama raia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kwamba, kimsingi hakuna misigano kati ya kuwa ni mwamini na raia! Jambo la msingi ni waamini kuhakikisha kwamba, kweli wanakuwa ni raia wema na wachamungu. Waamini wawe ni mashuhuda wa tunu msingi za maisha ya kiroho na utu wema kwa kukazia: unyofu wa moyo, uaminifu, upendo; mafao, ustawi na maendeleo ya wengi, daima wakionesha upendo na mshikamano na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Jamii, inahitaji raia ambao ni waaminifu, wanaojitahidi kuishi maadili mema; kwa kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ili kujipatia riziki yao ya siku bila kushawishika kutafuta njia ya mkato inayowatumbukiza wengi katika rushwa, ufisadi na wizi wa mali ya umma. Kuna haja ya kuendeleza mchakato wa majadiliano kati ya Waislam na Wakristo; majadiliano ambayo yanajichimbia kwa namna ya pekee katika uhalisia wa maisha ya kila siku.

Taasisi za kidini nazo zitekeleze nyajibu zake kwa kushirikiana katika kuwahudumia maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Huduma hii iwe ni makini, inayotekelezwa katika hali ya unyenyekevu, hekima, huruma na mapendo ya dhati, ili kujenga na kuimarisha amani, usalama, ustawi na maendeleo ya wengi! Wajumbe kwa namna ya pekee, wanamshukuru na kumpongeza Mfalme Mohammad VI wa Morocco na watu wake kwa fadhila na ukarimu aliouonesha kwa wajumbe wa mkutano huu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.