2017-05-09 14:39:00

Hija ya mshikamano wa upendo na waamini wa Makanisa ya Mashariki


Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki kuanzia tarehe 6 hadi 15 Mei 2017 anafanya ziara ya kichungaji nchini Australia ambayo itamwezesha kukutana na kuzungumza na viongozi mbali mbali wa Makanisa ya Mashariki sanjari na kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa pamoja nao! Akiwa mjini Sydney, Kardinali Sandri amekutana na kuzungumza na wakimbizi pamoja na wahamiaji kutoka Siria na Iraq wanaohudumiwa na Makanisa ya Mashariki huko Australia.

Amesikiliza shuhuda mbali mbali ambazo zimetolewa na wakimbizi hawa akiwemo Askofu mkuu Amel Shamon Nona, ambaye hadi mwaka 2014 alikuwa amepewa dhamana ya kuwaongoza, kuwafundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu huko Mosul, Iraq. Kutokana na nyanyaso na madhulumu ya kidini, leo hii amejikuta yuko uhamishoni. Ni matumaini yake kwamba, iko siku, wahamiaji na wakimbizi kutoka Siria na Iraq wataweza kurejea tena nchini mwao na kuishi kwa amani, utulivu na maridhiano; tayari kuanza mapambazuko ya utu mpya unaosimikwa katika majadiliano ya kidini na kiekumene kwa ajili ya: haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi!

Kardinali Sandri, aliwasili nchini Australia, Jumamosi tarehe 6 Mei 2017 na kupokelewa na Askofu mkuu Adolfo Tito Yllana, Balozi wa Vatican nchini Australia pamoja na viongozi wengine wa Makanisa ya Mashariki yaliyoko nchini Australia. Jumapili asubuhi, ameadhimisha Liturujia Takatifu katika Kanisa la Bikira Maria Mama Yetu wa Lebanon. Askofu Antoine Charnel Tarabay wa Jimbo la Maron, Sydney, amemshukuru na kumpongeza Kardinali Sandri kwa jitihada zake za kutembelea na kuimarisha Jumuiya za Makanisa ya Mashariki.

Kardinali Sandri, Jumatatu tarehe 8 Mei 2017 kwenye Kanisa kuu la Canberra ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake. Katika mahubiri yake, amekazia umuhimu wa kuendelea kumwilisha na kuimarisha Mapokeo na tamaduni zao njema hata wakati huu wakiwa ugenini, kama walivyofanya watakatifu kama vile: Marone, Charbel na Rafka. Ni watakatifu waliokita maisha yao ya kiroho katika Mapokeo ya Makanisa ya Mashariki, wakawa ni chachu na mfano bora wa kuigwa na watu waliokuwa wanawazunguka.

Kardinali Sandri amekazia umuhimu wa kudumisha majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam pamoja na kuimarisha uekumene wa huduma ya upendo miongoni mwa Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema, daima wakijitahidi kushuhudia nguvu ya upendo wa Kikristo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Msalaba. Ushiriki mkamilifu wa waamini katika Mafumbo ya Kanisa, uwawezeshe kupata neema na baraka inayoboresha maisha yao ya kiroho, tayari kujisadaka katika huduma ya upendo kwa jirani, kielelezo makini cha imani tendaji!

Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumkumbuka na kumwombea Khalifa wa Mtakatifu Petro ni kutaka kuimarisha upendo na mshikamano wa dhati na Baba Mtakatifu ambaye amepewa dhamana na Kristo Yesu ya kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo. Imekuwa ni fursa ya kuwakumbuka Mapapa waliowahi kutembelea nchini Australia kama vile: Mwenyeheri Paulo VI aliyetembelea nchini humo kunako mwaka 1970; Mtakatifu Yohane Paulo II akatembelea Australia mwaka 1986 na baadaye mwaka 1995. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alitembelea nchini humo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2008.

Daima viongozi wakuu wa Kanisa wamekuwa wakikazia umuhimu wa Kanisa kuendelea kujikita katika mchakato wa kutafuta na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Ushirikiano na mshikamano unaofumbatwa katika kanuni auni pamoja na kuhakikisha kwamba, waamini walei wanatekeleza dhamana na wajibu wao barabara. Ni dhamana pia inayopaswa kutekeleza na wanadiplomasia wanaoziwakilisha nchi zao sehemu mbali mbali za dunia. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa na Baba Mtakatifu kuwa ni madaraja na wajenzi wa amani dunia sanjari na kuwa ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.

Kwa namna ya pekee, wamemwombea Baba Mtakatifu Francisko anapojiandaa kwa ajili ya hija yake ya kitume huko Fatima, nchini Ureno, ili kushiriki katika kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima sanjari na kuwatangaza wenyeheri Francis na Yacinta Marto kuwa ni Watakatifu. Kardinali Leonardo Sandri amehitimisha mahubiri yake kwa kuwaalika waamini kuombea amani, toba na wongofu wa ndani, ili dunia iweze kuishi katika hali ya utulivu na amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.