2017-05-08 11:17:00

Yesu ni mchungaji mwema na mlango wa wokovu wa binadamu!


Yesu ni Mchungaji mwema na Mlango wa maisha ya uzima wa milele kwani kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake amemkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na wote wamefanyika kuwa ni kondoo wake. Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 7 Mei 2017, wakati wa tafakari yake ya Sala ya Malkia wa Mbingu, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Hii ni Jumapili ya Kristo Mchungaji mwema, Siku ya 54 ya Kuombea Miito Duniani ambayo kwa mwaka huu, imeongozwa na kauli mbiu “Tukisukumwa na Roho Mtakatifu kwa ajili ya utume”.

Baba Mtakatifu amekazia mwelekeo wa kimissionari katika wito wa Kikristo na ametoa Daraja Takatifu ya Upadre kwa Mashemasi 10 kutoka ndani na nje ya Jimbo kuu la Roma! Mapadre wapya wanne kutoka Jimbo kuu la Roma, wameshirikiana na Baba Mtakatifu Francisko kutoa baraka baada ya Sala ya Malkia Mbingu, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, uliokuwa umefurika kwa umati mkubwa wa watu kutoka ndani na nje ya Italia! Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, Kristo Yesu ni Mchungaji mwema, anayewapenda na kuwajali kondoo wake; anawafahamu na kuwaita kwa majina; wanaifuata sauti yake, ili kuwapeleka kwenye malisho ya majani mabichi. Anaonya kwamba, kuna wachungaji wengine ni wevi na wanyang’anyi na hao wameruka ukuta ili kuwatafuna na kuwararua kondoo. Ndiyo maana Yesu anasema kwamba, Yeye ni Mlango wa Wokovu wa binadamu kwani ameyamimina maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Yesu ni kiongozi anayetumia madaraka yake kwa ajili ya huduma makini;  anayeamuru kwa kujisadaka mwenyewe. Ni kiongozi anayethaminiwa na kupendwa na kondoo wake, kiasi kwamba, wako tayari kuisikiliza sauti yake na watapelekwa kwenye malisho bora zaidi. Ni kondoo wanaomtii na kujiaminisha kwake kwani: anashuhudia kuwa ni rafiki mwema na mwenye nguvu; mpole na mwenye kuonesha dira na mwongozo wa kufuata; ni kiongozi anayewalinda, anayewafariji; anayeganga na kuwaponya wale waliovunjika moyo!

Huyu ndiye Kristo Mchungaji mwema na mlango wa wokovu, utambulisho ambao pengine umefunikwa na uvuli wa giza katika maisha ya kiroho na upendo, kiasi cha Wakristo kushindwa kuonesha ule uhusiano mwema kati yao kama kondoo na Kristo Mchungaji mwema. Baba Mtakatifu anasikitika kusema, kwamba, wakati mwingine, waamini wamekuwa wadadisi sana kuhusu mambo ya imani, kiasi hata cha kushindwa kuisikia ile sauti ya Kristo Yesu, Mchungaji mwema, inayowaita na kuwapatia hamasa. Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa wale wanafunzi wa Emau, waliokuwa wanaandamana na Yesu njiani, wakasikia moto wa mapendo ukiwaka ndani mwao, wakati Yesu Kristo Mfufuka alipokuwa anazungumza pamoja nao njiani. Jambo la msingi kwa waamini wa nyakati hizi ni kujiuliza ikiwa kama kweli wanajisikia kupendwa na kuthaminiwa na Kristo Yesu katika maisha yao; kwa kuwa tayari kuisikiliza sauti yake bila kuchanganyikiwa na “hekima ya mambo ya duniani”, bali wakaze nia yao njema ya kumfuasa Kristo Mfufuka, kiongozi makini na anayetoa maana kamili ya maisha.

Katika maadhimisho ya Siku ya Kuombea Miito Duniani, hasa miito ya Kipadre, Baba Mtakatifu anawaalika waamini, kumwomba Bikira Maria aweze kuwasindikiza Mapadre wapya 10 waliopewa Daraja Takatifu ya Upadre katika maisha na utume wao. Awasaidie wale wote walioitwa na Kristo Yesu, wawe tayari kuitikia na kumfuasa kwa ukarimu, ari na moyo mkuu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.