2017-05-08 15:13:00

Papa Francisko: Wenyeheri wapya ni mashuhuda wa Injili ya upendo!


Baba Mtakatifu Fracisko mara baada ya Sala ya Malkia wa mbingu, Jumapili tarehe 7 Mei 2017 aliyaelekeza mawazo yake nchini Hispania ambako, Jumamosi, tarehe 6 Mei 2017, Kardinali Angelo Amato kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko alimtangaza Antonio Arribas Hortiguela na watawa wenzake sita kutoka Shirika la Moyo Mtakatifu wa Yesu kuwa wenyeheri. Watawa hawa wamekuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake, akawajalia zawadi ya ujasiri, kiasi hata cha kusadaka maisha yao kama wafuasi amini wa Kristo. Mashuhuda hawa wa imani waliuwawa kutokana na chuki za kiimani, wakati wa madhulumu ya kiimani nchini Hispania.

Baba Mtakatifu anasema, Mwenyeheri Antonio Arribas Hortiguela na watawa wenzake waliokubali kupokea upendo wa Mungu, wakaonesha uaminifu kwa wito wao; wawe ni mfano bora wa kuigwa ndani ya Kanisa kwa kuamsha kiu ya ushuhuda wa nguvu ya Injili ya upendo. Hawa walikuwa ni watawa vijana wabichi kabisa wakiwa na umri kati ya miaka 20 na 28, lakini tayari wakajisadaka kwa ajili ya Injili ya upendo kwa Kristo na Kanisa lake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.