2017-05-08 14:53:00

Papa Francisko: Imani inapaswa kukua, kukomaa, kuenea na kushuhudiwa!


Mwamini anapaswa kujiangalia kwa makini ili asitumbukie katika dhambi kwa kupingana na Roho Mtakatifu, bali ajitahidi kuwa wazi mbele ya Mwenyezi Mungu anayeendelea kumshangaza katika hija ya maisha yake hapa duniani. Mtume Petro alikumbana na maono kabla ya kukubali mwaliko wa kwenda Yafa ili kukutana na Jumuiya ya kwanza iliyokuwa imemwongokea Mungu, ikabahatika kusikia Habari Njema ya Wokovu ikitangazwa kwao na Mtakatifu Petro na hatimaye, wakabatizwa kwa Roho Mtakatifu.

Ni kweli kwamba, kuna baadhi ya waamini waliokuwa na wasi wasi kuhusu mwelekeo huu mpya wa Kanisa kwa wapagani kama inavyosimuliwa kwenye Kitabu cha Matendo ya Mitume! Roho Mtakatifu akaendelea kutenda kazi na miujiza kati ya waamini. Hii inaonesha kwamba, Mwenyezi Mungu daima yuko kati na anatembea pamoja na watu wake. Daima anaendelea kuwashangaza kwa matendo yake kwa sababu ni: hai, anaishi kati ya watu wake; anatembea kati nyoyo zao; ni Mungu ambaye yuko ndani ya Kanisa lake na daima anaongozana nalo! Roho Mtakatifu ni zawadi ya Baba anayeendelea kuwashangaza walimwengu; ndiye aliyeumba dunia na anaendelea kuumba mapya na hivi ndivyo Mwenyezi Mungu anavyowashangaza watu wake!

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika Ibada ya Misa Takatifu, Jumatatu, 8 Mei 2017 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican. Mshangao huu wa Mungu unaweza kusababisha magumu na changamoto kubwa katika maisha ya kiroho kama ilivyotokea kwa Mtakatifu Petro, aliyeshutumiwa kwa kushikamana na wapagani waliopokea Neno la Mungu na kubatizwa kwa Roho Mtakatifu. Kitendo hiki kilionekana kuwa ni kashfa kubwa kwa Petro, Mwamba wa Kanisa ambaye alikuwa amekabidhiwa madaraka ya kuliongoza Kanisa!

Lakini Mtume Petro alijitahidi kuangalia mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu na kuamua kufanya maamuzi magumu na yenye ujasiri, ili kuendelea kushangazwa na Mwenyezi Mungu, kiasi hata cha Mitume wakaamua kufanya Mtaguso mkuu wa kwanza ili kutekeleza mpango wa Mungu uliokuwa mbele yao! Tangu mwanzo, kumekuwepo na dhambi ya kutaka kupingana na Roho Mtakatifu na hivi ndivyo walivyotaka Petro kukaa kimya na kumgeuzia Mungu kisogo, lakini Mzaburi anawaonya watu wasifanye mioyo yao migumu kama ilivyokuwa kwa baba zao.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumsikiliza kwa makini, kumtii na kufuasa Kristo Mchungaji mwema. Jitihada hizi zinapaswa kuelekezwa hata kwa wale kondoo ambao si wa kundi hili, ili kondoo wote siku moja waweze kuwa chini ya mchungaji mmoja. Hawa ndio wapagani waliodhaniwa kwamba, wamelaaniwa na Mwenyezi Mungu na hata pale walipofanikiwa kubatizwa kwa maji na Roho Mtakatifu, bado walitengwa na kuchukuliwa kuwa ni waamini wa daraja la pili. Hizi ni dalili za kujifungia katika ubinafsi na kwa kushindana na Roho Mtakatifu. Hii ni tabia mbaya inayofifisha uhuru, furaha na uaminifu kwa Roho Mtakatifu anayetenda ili kulipeleka Kanisa mbele. Ili kufahamu kweli kwamba, hii ni kazi ya Roho Mtakatifu na wala si malimwengu kuna haja ya kuwa na kipaji cha mang’amuzi, kama walivyofanya Mitume kwa kukutana na kuadhimisha Mtaguso wa kwanza wa Yerusalemu, uliowawezesha kusonga mbele kwa imani na matumaini.

Wakristo wanapaswa kuwa na kipaji cha kung’amua ambacho kimsingi ni zawadi ya Roho Mtakatifu. Imani inapaswa kukua, kupanuka na kukomaa kama anavyosema Mtakatifu Vincent wa Lerino. Ukweli wa maisha na utume wa Kanisa vinasonga mbele, kwa kukua na kuimarishwa kwa kusoma alama za nyakati ili kuwa kuwa na nguvu kadiri ya muda unavyosonga mbele. Inawezekana kukosea njia, lakini waamini wamwombe Mwenyezi Mungu neema ya kutokubali kushindwa na kujikalia kitako, katika ubaridi na ugumu wa mioyo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.