2017-05-08 09:50:00

Msiba wa Kitaifa; Wanafunzi 32, walimu 2 na dreva 1 wapoteza maisha!


Taarifa iliyotolewa na kamanda wa polisi mkoani Arusha, Kaskazini mwa Tanzania imesema kuwa, jumla ya wanafunzi 32 pamoja na walimu wao na dreva walipoteza maisha hapo hapo katika ajali iliyotokea wilani Karatu kando ya Mto Marera Jumamosi 6 Mei 2017 . Wanafunzi na walimu hao walipata ajali hiyo wakati wanaenda kwenye shule iitwayo Tumaini kwa ajili ya kufanya mitihani wa ujirani mwema baada ya gari walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kutumbukia bondeni kwenye eneo la Rhotia wilayani Karatu. Habari za awali zilikuwa zimesema ni watoto wanne pekee ndio walionusurika katika ajali hiyo ingawa hali zao  zilikuwa mahututi na kwamba kuna uwezekano idadi ya vifo ikaongezeka. Kufuatia tukio hilo, Rais John Pombe Magufuli wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania alimtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Mrisho Gambo na kueleza kuwa ajali hiyo imezima ndoto za watoto waliokuwa wakijiandaa kulitumikia Taifa na imesababisha uchungu, huzuni na masikitiko makubwa kwa familia za marehemu na taifa kwa ujumla.

Taaarifa kutoka Vyombo vya habari pia vinasema ,Jumatatu tarehe 8 Mei 2017, Ibada na dua za kuaga miili ya marehemu hao inafanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha. Jumapili 7 Mei 2017, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na ujumbe wake walipokelewa katika uwanja wa ndege wa Arusha  na Mkuu wa mkoa wa Arusha Mhe Mrisho Gambo pamoja na viongozi wengine wa mkoa huo. Kuwasili kwake ni kuongoza  wananchi wa mkoa wa Arusha na mikoa ya jirani katika kuaga miili ya wanafunzi,walimu wawili pamoja na dereva mmoja wa shule ya Lucky Vicent iliyopo mjini Arusha .

Aidha ripoti zaidi zinasema ,simanzi na majonzi yametanda katika mji wa Arusha wa kaskazini mwa Tanzania kutokana na msiba huo mkubwa. Viongozi mbalimbali wameendelea kutuma salamu zao za rambirambi kufuatia ajali hiyo mbaya. Ikumbukwe kuwa, Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo hukumbwa na ajali za barabarani mara kwa mara na kupelekea mamia ya watu kupoteza maisha kila mwaka katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.Uchunguzi unaonesha kuwa,asilimia kubwa ya ajali hizo chanzo chake ni mwendo wa kasi!

Sr Angela Rwezaula 
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.