2017-05-08 07:20:00

Cheche za Mapambazuko Mapya ya Ubinadamu zawashwa nchini Misri!


Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki katika mahojiano maalum na Gazeti la L’Osservatore Romano anasema, hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Misri iliyoongozwa na kauli mbiu “Papa wa amani nchini Misri” iliyohitimishwa hivi karibuni ni “cheche mpya za Mapambazuko ya ubinadamu” yanayojikita katika majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kudumisha: utu, heshima, ustawi na maendeleo ya wengi. Ni mapambazuko ya ubinadamu yanayopania kuendeleza: haki msingi za binadamu, amani na maridhiano kati ya watu!

Ni mchakato unaopania kuhakikisha kwamba, mwanadamu anakuwa ni kitovu cha maendeleo kwa watu kujipatia elimu bora na makini itakayowawezesha kupambana vyema na changamoto za maisha na hatimaye, Misri iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Watu wote wapate fursa na haki sawa katika huduma ya afya ili kupambana na magonjwa yanayodhalilisha na kunyanyasa utu na heshima ya binadamu. Wazee na maskini wanapaswa kuangaliwa kwa jicho la huruma na upendo kwani hawa kimsingi ndicho kipimo cha ufanisi wa huduma makini kwa binadamu. Itakumbukwa kwamba, kazi ni utimilifu wa utu na heshima ya binadamu; kazi inawawezesha watu kutekeleza vyema dhamana na majukumu yao ya kifamilia, kijamii na kitaifa, kumbe, kuna haja ya kuwa na sera na mikakati makini ya uchumi shiriki ili kwamba, watu wengi zaidi waweze kupata fursa za ajira, lakini zaidi ajira miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, jeuri na matumaini ya jamii husika!

Kardinali Leonardo Sandri anakaza kusema, cheche za “Mapambazuko ya ubinadamu mpya” nchini Misri baada ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko ni kutaka kukuza na kudumisha utu na heshima ya binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Hija hii ilijikita katika misingi ya shughuli za kitume, majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kujenga madaraja ya watu kukutana, kujadiliana katika ukweli na uwazi, ili kwa pamoja kushiriki katika ujenzi wa umoja na mshikamano wa kitaifa, licha ya tofauti na changamoto mbali mbali zinazoweza kujitokeza katika hija ya maisha ya pamoja kama taifa! Ni matumaini ya Kanisa kwamba, hija hii ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Misri itazaa matunda yanayokusudiwa huko Mashariki ya kati kwa kujenga na kudumisha misingi ya majadiliano ya kidini na kiekumene, ili amani, ustawi na maendeleo endelevu yaweze kujikita na kustawi katika maisha ya watu hawa ambao kwa miaka mingi wanaelemewa na vita, mashambulizi ya kigaidi, nyanyaso na dhuluma kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake!

Kardinali Sandri anasema, maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwa Jumuiya ya waamini wa Kanisa Katoliki nchini Misri, iliyohudhuriwa na bahari ya waamini, ilikuwa ni nafasi ya pekee ya kuonesha na kushuhudia umoja, upendo na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Imekuwa ni nafasi kwa Baba Mtakatifu kuwatia shime katika ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake; imani inayomwilishwa katika ushuhuda wa Injili ya upendo. Waamini wameonesha ibada na moyo wa sala; watoto wakashuhudia kuwa kweli wao ni watoto wa Misri, lakini pia ni waamini wa Kanisa Katoliki kutokana na mavazi yao yaliyokuwa yanapendeza na kuvutia hisia za wengi. Waamini wameonesha kwamba, licha ya changamoto na matatizo mbali mbali wanayokabiliana nayo katika hija ya maisha yao ya kiroho, bado wana imani na matumaini kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!

Kardinali Sandri anakaza kusema, kwa miaka ya hivi karibuni Wakristo nchini Misri wamekumbana na vistisho na mashambulizi ya kigaidi ambayo yamepelekea watu kadhaa kupoteza maisha na mali zao, hali ambayo pia inahatarisha mshikamano wa kitaifa; mafungamano ya kijamii na uhuru wa kuabudu ambao ni msingi wa haki zote za binadamu. Hata hivyo, Kanisa Katoliki bado lina nafasi ya pekee katika umwilishaji wa Injili ya upendo katika huduma ya elimu, afya, ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu.

Katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Mashariki ya Kati, iliyoitishwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, kunako mwaka 2010, kwa namna ya pekee, aliwahimiza waamini kujenga na kudumisha umoja na ushuhuda kama kielelezo cha imani na uzalendo kwa nchi zao. Mkazo ulikuwa ni watu wote kuheshimu utawala wa sheria, demokrasia na uhuru wa kuabudu, kila raia akipewa haki zake msingi na kutekeleza wajibu na dhamana yake kama raia! Raia wema ni dhana iliyochimbiwa mkwara na viongozi wa Kanisa huko Mashariki ya kati kutokana na kukithiri kwa vitendo vya kigaidi na misimamo mikali inayohatarisha: usalama, amani na haki msingi za binadamu!

Kanisa Katoliki kwa kushirikiana na wadau mbali mbali anasema Kardinali Sandri, limeendelea kuwa mstari wa mbele katika hutoaji wa huduma makini katika sekta ya elimu, afya, ustawi na maendeleo ya wengi kama chachu muhimu sana ya kupambana na umaskini wa hali na kipato; magonjwa na ujinga. Lengo ni kukuza na kudumisha utu, heshima, ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu wote, ambao kweli wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Huu ndio ujumbe ambao Baba Mtakatifu amewaachia viongozi wa Serikali, wanasiasa na wanadiplomasia wakati wa hija yake ya kitume nchini Misri. Ni matumaini ya Kanisa kwamba, ujumbe huu utaweza kuzaa matunda kwa wakati wake!

Kardinali Leonardo Sandri anakaza kusema, Misri ni nchi yenye utamaduni na utajiri mkubwa wa urithi wa mambo ya kale. Ni nchi ambayo ilibahatika kuwa ni makao ya Mababa wa imani. Hapa ni mahali ambapo Pasaka ya kwanza ya Wayahudi ilitendeka, Mwenyezi Mungu alipowakomboa watu wake kutoka utumwani Misri kwa nguvu na mkono wa ajabu, akawavusha salama kwenye Bahari ya Shamu. Mwenyezi Mungu akaweka Agano la Kale na Waisraeli pale Mlimani Sinai na hatimaye kuwapatia Amri Kumi, ambazo ni dira,  mwongozo na utambulisho wao kama Taifa teule la Mungu. Hii ni historia inayofumbata wito, changamoto ya utakatifu wa maisha na utekelezaji wa mpango wa Mungu katika maisha ya binadamu. Hata leo hii, Misri bado inayo nafasi kubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi katika Jumuiya ya Kimataifa, ikiwa kama: ulinzi, usalama, amani na haki msingi za binadamu vitapewa kipaumbele cha pekee. Amani na usalama ni mambo yanayopaswa kuvaliwa njuga nchini Misri.

Kardinali Leonardo Sandri anasema, hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Misri imeimarisha uhusiano wa kidugu kati ya viongozi wa Makanisa ya Kikristo nchini Misri, kiasi kwamba, baada ya vuta nikuvute, kinzani na misigano ya kiekumene, hatimaye, Baba Mtakatifu Francisko, Papa Tawadros II pamoja na Patriaki Ibrahim Sedrak waliweza kukaa na hatimaye, kutoa Tamko la Pamoja huko Misri; wamekazia uekumene wa sala na maisha ya kiroho; uekumene wa damu na huduma makini kwa wananchi wote wa Misri. Mshikamano miongoni mwa Wakristo wakati wa raha na shida umeimarishwa zaidi na hasa kwa kukumbuka kwamba, kwa pamoja wanao urithi mkubwa ulioachwa na Mababa wa Jangwani katika maisha ya kiroho na liturujia, cheche za ushuhuda na utakatifu wa maisha ya Kikristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.