2017-05-06 14:16:00

Uswiss na Vatican kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 6 Mei 2017 amekutana na kuzungumza na Bi Doris Leuthard, Rais wa Shirikisho la Uswiss ambaye baadaye amekutana na kuzungumza pia na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican. Papa Francisko na mgeni wake katika mazungumzo yao ya faragha wamgusia huduma msingi inayotolewa na Kikosi cha Ulinzi na Usalama kutoka Uswiss, maarufu kama “Swiss Guards” ambao wamekula kiapo cha utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, Jumamosi, tarehe 6 Mei 2017 pamoja na kukutana na Baba Mtakatifu Francisko.

Viongozi hawa wawili wameonesha nia ya kutaka kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, sanjari na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na Kanisa Katoliki nchini Uswiss. Baadaye, viongozi hawa wawili wamejielekeza zaidi kwa tema mahususi hasa kwa kuangalia mustakabali wa Bara la Ulaya kwa siku za usoni; changamoto ya wakimbizi na wahamiaji; ukosefu wa fursa za ajira miongoni mwa vijana wa kizazi kipya; mapambano dhidi ya vitendo vya kigaidi pamoja na changamoto ya kusimama kidete kulinda, kutetea na kuendeleza mazingira nyumba ya wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.