2017-05-04 10:44:00

Papa Francisko kutoa Daraja Takatifu ya Upadre kwa Mashemasi 10


Siku ya 54 ya Kuombea Miito Duniani inayoadhimishwa na Mama Kanisa tarehe 7 Mei, 2017 inaongozwa na kauli mbiu “Tukisukumwa na Roho Mtakatifu kwa ajili ya utume”.  Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa ajili ya maadhimisho haya anakumbusha kwamba, wito wa Kikristo ni mwaliko wa kutoka katika ubinafsi, tayari kujizatiti kusikiliza kwa makini sauti ya Mwenyezi Mungu anayeita daima na umuhimu wa Jumuiya ya Kikristo kama mahali maalum pa kuibua, kukuza na kushuhudia wito.

Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu kwa mwaka huu 2017 anapenda kukazia mwelekeo wa Kimisionari katika wito wa Kikristo! Hawa ni wale ambao wamesikiliza sauti ya Mungu, wakajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kumfuasa Kristo na kwamba, wanatambua ndani mwao kuwa; wanayo dhamana na wajibu wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa jirani zao kwa njia ya: Uinjilishaji na huduma ya upendo; kwa njia ya Neno na Sakramenti za Kanisa. Kanisa linaadhimisha Siku ya Kuombea Miito Duniani kama pia sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana itakayotimua vumbi mjini Vatican mwezi Oktoba 2018 kwa kuongozwa na kauli mbiu mbiu “Vijana, imani na mang’amuzi ya miito”.

Baba Mtakatifu, Jumapili ya Nne ya Kipindi cha Pasaka, Maarufu kama Jumapili ya Kristo Mchungaji mwema, anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuanzia saa 4: 00 kwa saa za Ulaya. Katiba Ibada hii ya Misa Takatifu, atatoa pia Daraja Takatifu ya Upadre kwa Mashemasi kumi kutoka Seminari kuu ya Kipapa ya Jimbo kuu la Roma pamoja na Seminari ya kimissionari ya Jimbo kuu la Roma, maarufu kama “Redemptoris Mater”. Ibada hii ya Misa Takatifu itatanguliwa na mkesha wa sala na Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuombea Miito itakayoadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano, Ijumaa usiku, tarehe 5 Mei 2017. Mashemasi sita wanatoka Jimbo kuu la Roma na wengine waliobakia wanatoka kwenye Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume. Mashemasi watakaopadrishwa na Baba Mtakatifu Francisko kutoka Jimbo kuu la Roma ni pamoja na: Andreas Biancucci,  Dario Loi, Mattia Pica, Gabriele Vecchione Rolando Francesco Rizzuto pamoja na Alfonso Torre Elias. Mashemasi wengine ni pamoja na: Andrea Bonfanti Octavio Angel Jimenez Bello, David Behbud Mustafayev pamoja na Aniello Nappo.

Baba Mtakatifu anapenda kuwahimiza waamini kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya wito wa Kipadre na maisha ya kuwekwa wakfu. Watu wa Mungu wanapaswa kuongozwa na watumishi wa Mungu wanaoyamimina maisha yao kwa ajili huduma ya Injili, changamoto na mwaliko kwa waamini na vyama vyote vya kitume, kujizatiti katika sala ili kumwomba Mwenyezi Mungu aweze kupeleka watenda kazi: wema, watakatifu na wachapakazi katika shamba lake. Wafanyakazi ambao wameshibana vyema na Injili, tayari kujisadaka kwa ajili ya Injili ya huruma na mapendo kwa jirani zao; kwa kukazia utu, furaha na upendo katika huduma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.