2017-04-30 12:10:00

Tamko la Pamoja kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Papa Tawadros II


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Misri, Ijumaa tarehe 28 Aprili 2017 alikutana na kuzungumza na Papa Tawadros II wa Kanisa la Kikoptik Misri na baadaye kuweka sahihi katika Tamko la pamoja kama sehemu ya mchakato unaopania kujenga na kuimarisha majadiliano ya kiekumene katika sala na maisha ya kiroho; katika ushuhuda na huduma, daima wakimshukuru Roho Mtakatifu anayewawezesha kukutana ili kumtolea Mwenyezi Mungu sifa na shukrani kwa ushuhuda wa umoja na udugu unaofumbatwa katika maisha ya Mtakatifu Petro na Mwinjili Marko. Makanisa haya mawili yanaendelea kukuza na kudumisha urafiki, imani na upendo kwa Kristo Yesu. Misri ni nchi iliyo barikiwa, yenye tamaduni za kale na dini mbali mbali na kwa namna ya pekee dini ya Kiislam. Misri ni mahali ambapo Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ilipata hifadhi; Misri ni nchi ya mashuhuda wa imani na watakatifu wa Kanisa.

Viongozi hawa katika tamko lao la pamoja wanasema, kulikuwepo na umoja kamili kati ya Makanisa haya mawili na kushuhudiwa katika Mitaguso mbali mbali ya Kiekumene kama ule Mtaguso wa Nicea ulioadhimishwa kunako mwaka 325 na hapo Kanisa likatambua mchango wa Mtakatifu Athanasi kama mlinzi wa imani. Umoja huu ukashuhudiwa kwa njia ya sala, liturujia, ibada kwa watakatifu na mashuhuda wa imani; katika huduma makini ya maendeleo endelevu ya watu na katika kukua na kupanuka kwa Umonaki, daima kwa kufuata ushuhuda wa maisha ya Mtakatifu Anthoni Mkuu. Kutokana na sababu hizi msingi ndiyo maana Makanisa haya mawili yanataka kurejesha tena umoja kamili, juhudi ambazo zimekuzwa na kuimarishwa katika miaka ya hivi karibuni, ili kujenga umoja katika utofauti chini ya usimamizi wa Roho Mtakatifu.

Viongozi hawa wanakumbuka kwa heshima tukio lililowakutanisha Mwenyeheri Paulo VI na Papa Amba Shenouda III kunako mwaka 1973 kwa kukumbatiana na kupeana busu la kidugu na huo ukawa ni mwanzo wa kuandika historia ya majadiliano ya kiekumene iliyopelekea kuundwa kwa Tume mchanganyiko wa Taalimungu kati ya Makanisa haya mawili, ili kuendeleza majadiliano ya kitaalimungu kwa kuwa na mwelekeo mpana zaidi. Makanisa haya yanasadiki na kuungama imani katika “Mungu mmoja, Fumbo la Utatu Mtakatifu; Umungu wa Kristo, Mwana pekee wa Mungu aliyezaliwa bila kuumbwa, ni Mungu kweli na Mtu kweli. Maisha ya Kimungu yanapata chimbuko na kurutubishwa zaidi kwa njia ya Sakramenti Saba za Kanisa na Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu, Mama wa mwanga kweli, “Theotokos”.

Mkutano kati ya Papa Tawadros II na Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2013 umeimarisha na kudumisha urafiki na udugu kati ya Makanisa haya mawili pamoja na kutambua kwamba, kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, wakristo wote wanafanyika kuwa ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa, changamoto ya kuendelea kushirikiana na kushikamana katika umoja, ili kukua na kukomaa katika upendo na upatanisho. Wakuu hawa wa Makanisa wameamua kufuata nyayo za watangulizi wao katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, ili kudumisha ari na moyo mkuu wa kumfuasa Kristo Yesu, uliooneshwa kwa namna ya pekee kwa njia ya upendo kwa Kristo Yesu, Mchungaji mwema, changamoto ni kujichotea nguvu kutoka kwa Mwenyezi Mungu ili hatimaye, kupata umoja na upendo kamili hususana katika: maisha ya sala kwa kutambua na kuthamini yale mambo msingi yanayowaunganisha Wakristo kuliko yale yanayowagawa na kuwasambaratisha, lengo ni kutekeleza agizo la Kristo Yesu, ili wote wawe wamoja.

Huu ni uekumene wa sala utakaowawezesha kuwa na sala za pamoja sanjari na maadhimisho ya Fumbo la Pasaka na Ekaristi Takatifu kwa pamoja kwa kuimarisha mambo msingi ambayo tayari yanayaunganisha Makanisa haya mawili. Ni uekumene unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha matakatifu; utakatifu wa maisha ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; utakatifu wa maisha na utume wa ndoa na familia pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Wakristo wanahamasishwa kushuhudia kwa pamoja tunu msingi za Kiinjili mintarafu Mapokeo ya Makanisa haya mawili; kuendelea kujifunza utajiri mkubwa unaofumbatwa katika maisha ya Mababa wa Kanisa kutoka Mashariki na Magharibi.

Makanisa haya yaangalie uwezekano wa kuwa na mpango mkakati wa shughuli za kichungaji hasa katika Katekesi makini ili kutajirishana amana inayobubujika kutoka kwa wamonaki na watawa. Wakristo wawe ni mashuhuda wa upatanisho na matumaini kwa familia ya Mungu nchini Misri, kwa kusimama kidete kulinda na kutetea matunda ya haki na amani sanjari na kutambua kwamba, binadamu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Makanisa haya mawili yanataka kujizatiti katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi nchini Misri, kwa kushiriki kikamilifu katika maisha ya kijamii; kwa kuheshimu uhuru wa kidini, uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidhamiri unaofumbatwa katika utu na heshima ya binadamu na kwamba hii ni haki msingi ambayo kamwe haiwezi kuondoshwa na awaye yote!

Makanisa haya yameamua kudumisha moyo wa sala ili kuwakumbuka na kuwaombea Wakristo wanaouwawa, wanaonyanyaswa na kudhulumiwa sehemu mbali mbali za dunia kwa vile tu wao ni Wakristo! Uekumene wa damu unawaunganisha Wakristo wote na kuwahamasisha kujikita katika njia ya amani na upatanisho. Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu kwa ajili ya upendo kwa binadamu wote ni kiini cha majadiliano ya kiekumene ili kuweza kufikia umoja kamili. Damu ya mashuhuda wa imani kwa Kanisa la mwanzo ilikuwa ni mbegu ya Ukristo; damu ya mashuhuda wa imani wa nyakati hizi, iwe kweli ni mbegu ya umoja wa Wakristo na chombo cha mshikamano na amani duniani. Makanisa haya yataendelea kumtii Roho Mtakatifu anayelitakatifuza Kanisa na kuliongoza katika umoja kamili ambao uliombwa na Kristo mwenyewe.

Viongozi hawa wanakiri kwa pamoja Ubatizo mmoja kwa maondoleo ya dhambi; utii kwa Maandiko Matakatifu na Imani ambayo imeungamwa na Mababa wa Kanisa katika Mitaguso ya Kiuekumene ya: Nicea, Costantinopoli na Efeso na kwamba, wanaendelea kujiaminisha chini ya ulinzi na uongozi wa Roho Mtakatifu, ili siku moja waweze kuwa na umoja katika Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa, daima wakijitahidi kufuata Mafundisho ya Mtakatifu Paulo Mtume kwa kudumisha umoja na amani; matumaini, imani na ubatizo mmoja. Wanamtambua Mungu mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.