2017-04-29 14:55:00

Familia ya Mungu Misri inampongeza Papa Francisko mjumbe wa amani


Patriaki Ibrahim Isaac Sedrack wa Kanisa la Wakoptik wa Alexandria nchini Misri mara baada ya Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 29 Aprili 2017 wakati wa hija yake ya kitume nchini Misri, iliyokuwa inaongozwa na kauli mbiu “Papa wa amani nchini Misri”, ametumia nafasi hii kumshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kufika nchini mwao, Misri inayopenda amani, amani ambayo inayopaswa kuimarishwa zaidi huko Mashariki ya Kati na ulimwenguni kote!

Huu ni ushuhuda kwamba, Misri ni mahali pa majadiliano ya kidini na kitamaduni kwa watu mbali mbali. Hapa ni chimbuko la dini duniani, mahali ambapo pamekuwa ni makazi ya Mababa wa imani na kimbilio la Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu! Kwa hakika Misri ni nchi ya amani! Uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko ni ushuhuda kwamba, yeye ni mjumbe na mpenda amani; mambo yanayojionesha katika maisha na utume wake! Kwa hakika ni kiongozi anayetaka kupandikiza mbegu ya amani sehemu mbali mbali za dunia.

Patriaki Ibrahim Isaac Sedrack, anampongeza Baba Mtakatifu kwa kumchagua Mtakatifu Francisko kuwa msimamizi wake, kiasi cha kujitahidi kufuata nyayo zake na kubahatika kutembelea nchini Misri, takribani miaka mia nane iliyopita. Baba Mtakatifu ameamua kuiga mfano wa Mtakatifu Francisko aliyekuwa fukara na mpenda mazingira. Kwa maisha na utume kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, Baba Mtakatifu Francisko amejitahidi kuwaimarisha ndugu zake katika mambo msingi yanayomwendeleza mwanadamu: kiroho na kimwili; kiutu na kijamii.

Bado watu wanaendelea kumwilisha ujumbe wa huruma ya Mungu katika maisha na vipaumbele vyao. Huu ni ujumbe wa nguvu ambao Mwenyezi Mungu anautoa kwa ajili ya binadamu wote, akiwataka kujipatanisha naye. Kanisa Katoliki la Kikoptik nchini Misri limeuishi Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa njia ya sala na tafakari ya Neno la Mungu ambayo imemwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Viongozi wa Kanisa wanaounda Sinodi ya Kanisa la Katoliki la Kikoptik wanapenda kuonesha umoja na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro; ili kuunganisha taalimungu kutoka Mashariki na Magharibi, ili kutajirisha na kuboresha imani na liturujia ili kushuhudia Kanisa Katoliki ambalo liko wazi kwa walimwengu, Kanisa ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa katika ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu nchini Misri, hususan katika sekta ya elimu na afya; malezi na maendeleo endelevu ya binadamu!

Patriaki Ibrahim Isaac Sedrack anampongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kujielekeza katika maisha na utume wake katika majadiliano ya kiekumene kama sehemu ya utekelezaji wa agizo la Kristo Yesu, ili wote wawe wamoja. Yote haya ameyafanya kwa kukutana, kusali na kuzungumza na viongozi wa Makanisa mbali mbali ya Kikristo na kwamba, mkutano wake na Papa Tawadros II mjini Vatican, umeacha chapa ya kudumu kwa familia ya Mungu nchini Misri mintarafu mahusiano kati ya Makanisa haya mawili. Anawashukuru viongozi wa Serikali na Kidini waliothubutu kumwalika Baba Mtakatifu Francisko nchini Misri na kwamba, hata kama imekuwa ni hija ya siku chache, lakini imewashehenesha waamini furaha na baraka tele. Maadhimisho ya Ibada ya Misa takatifu yatabaki kuwa ni mhimili mkuu katika safari yao ya maisha ya kiroho, kitume na kijamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.