2017-04-28 17:49:00

Viongozi wa kidini waunganishe nguvu kujenga na kudumisha amani!


Sheikh Muhammad Al Tayyib, Imam mkuu  wa Msikiti wa Al-Azhar, Cairo katika hotuba yake kwenye mkutano wa majadiliano ya kidini kimataifa mintarafu amani ulioandaliwa na Chuo kikuu cha Al-Azhar cha Cairo nchini Misri, Ijumaa, tarehe 28 Aprili 2018 amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kukubali mwaliko wa kuweza kushiriki katika mchakato unaopania kuwaunganisha viongozi wa kidini, wasomi na wanazuoni katika harakati za ujenzi wa amani duniani na hivyo, kuondokana na vita ambavyo vinaendelea kusababisha majanga makubwa kwa watu na mali zao kwa nyakati hizi.

Sheikh Muhammad Al Tayyib anasema, chanzo cha maafa makubwa ya vita yanayoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo ni biashara haramu ya silaha inayoendelea kupandikiza utamaduni wa kifo kwa kuwatajirisha watu wachache kutokana na damu ya watu wasiokuwa na hatia. Biashara hii imewafunga watu midomo kiasi kwamba hata jitihada za Jumuiya ya Kimataifa kupambana na biashara hii haramu bado hazijafua dafu! Matokeo yake ni vita, kinzani na mipasuko ya kijamii pamoja chuki za kidini na kiimani zinazoendelea kuzalisha makundi makubwa ya wakimbizi na wahamiaji, kiasi hata cha kuhatarisha maisha yao.

Sheikh Muhammad Al Tayyib anakaza kusema, licha ya maendeleo makubwa yaliyojitokeza katika karne ya ishirini na moja katika medani mbali mbali za maisha, lakini imekuwa pia ni karne ambayo amani na usalama vimetoweka sana kiasi hata cha kutishia mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa. Kumekuwepo na mateso makali kwa watu, amani kutoweka na haki msingi za binadamu kuwekwa rehani kutokana na mauaji ya kimbari. Hii inatokana na ukweli kwamba, dini haina tena kipaumbele kwa maisha ya mwanadamu wa nyakati hizi na matokeo yake watu wengi wanamezwa na malimwengu kwa kupenda raha, starehe na anasa.

Kanuni maadili na utu wema vimetundikwa mbali kabisa na maisha ya watu, udugu, mahusiano mema, huruma na upendo vimetoweka na binadamu amegeuka kuwa mnyama wa kutisha! Ili kurekebisha hali ya kutopea kwa imani na utu wema, kuna haja tena ya dini kupewa kipaumbele cha pekee katika maisha ya watu kwa kukazia: haki, amani, usawa pamoja na kuondokana na aina zote za ubaguzi na Mwenyezi Mungu kupewa nafasi yake katika maisha ya mwanadamu! Dini inapaswa kuheshimiwa na kuondolewa kwenye vitendo vinavyodhalilisha utu na heshima ya binadamu na kwamba, kamwe dini isikubali kubebeshwa mzigo kinyume kabisa cha dhamana yake.

Kwa mfano dini ya Kiislam si dini ya kigaidi, lakini kuna baadhi ya waamini wanaotafsiri vibaya Koran Tukufu kama ilivyo hata kwa Wakristo wenye misimamo mikali. Katika hali kama hii, kuna wafadhili wanaojitokeza kutoa fedha, wafanyabiashara kuuza silaha na hata kutoa mafunzo na matokeo yake ni maafa makubwa kwa watu na mali zao. Lakini katika historia ya maisha ya binadamu kumekuwepo na vitendo vya kigaidi kama ilivyokuwa kwa Wapalestina kupokonywa ardhi yao; Bara la Ulaya kujikuta likijitumbukiza katika utamaduni wa kifo kwa njia ya vita ya kwanza na ile ya pili ya dunia na matokeo yake ni maafa makubwa yaliyojitokeza kule Hiroshima na Nagasaki. Kimsingi, katika historia, kila dini, tamaduni na serikali imeguswa na makovu ya vitendo vya kigaidi.

Sheikh Muhammad Al Tayyib amempongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kusimamia ukweli kuhusu misimamo mikali ya kidini na vitendo vya kigaidi ambavyo vimekuwa vikiipaka matope dini ya Kiislam. Wanampongeza kwa juhudi zake za kutaka kuimarisha na kukuza majadiliano ya kidini kwa kujikita katika tunu msingi za maisha ya kidini pamoja na viongozi wa kidini kushikamana ili kukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo. Waamini wa dini mbali mbali washikamane katika kupambana na ujinga, umaskini na magonjwa; wasaidie kutoa huduma kwa wafungwa wa kivita na wale wote wanaoteseka kutokana na nyanyaso pamoja na kubaguliwa. Waamini washikamane katika kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, kupambana rushwa pamoja na ufisadi; utepetevu wa imani na utu wema. Mwenyezi Mungu daima awe ni chemchemi ya huruma, asaidie mkutano huu, uwe ni fursa ya ushirikiano ili kujenga na kudumisha utamaduni wa amani, udugu na maridhiano kati ya watu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.