2017-04-28 18:13:00

Papa Francisko: Misri ina dhamana ya ujenzi wa amani duniani!


Baba Mtakatifu Francisko akiwa nchini Misri, Ijumaa, tarehe 28 Aprili 2017 amepata nafasi ya kukutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, kisiasa na Mabalozi na wawakishi wa nchi mbali mbali Misri pamoja na viongozi wa kidini. Amekumbuka kwa namna ya pekee uhusiano mwema uliopo baina ya viongozi kutoka Misri na Vatican, uliojidhihirisha kwa namna ya pekee kwa kutembeleana. Baba Mtakatifu anasema, Misri imebahatika kuwa na utajiri mkubwa wa Mapokeo ya Kanisa pamoja na waamini wa dini mbali mbali. Ni mahali walipoishi Mababa wa imani wanaotajwa kwenye Maandiko Matakatifu. Ni mahali ambapo Mwenyezi Mungu alijifunua mbele ya Musa na kumpatia Amri kumi; ni mahali ambapo Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ilipata hifadhi.

Hizi ni kumbu kumbu zenye utajiri mkubwa katika historia na maisha ya nchi ya Misri ambayo kimsingi inaweza kuhesabika kuwa ni Mama wa ulimwengu kama inavyojulikana “Misr um al dugna”. Misri bado inaendelea kuwa ni kimbilio la wahamiaji na wakimbizi kutoka Sudan, Eritrea, Siria na Iraq. Misri ina umaarufu mkubwa katika Jumuiya ya Kimataifa anasema Baba Mtakatifu Francisko katika kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza hasa kuhusiana na vita,inayokuzwa kutokana na biashara haramu ya silaha duniani; uchu wa mali na madaraka; misimamo mikali ya kidini, ndiyo maana Misri inapaswa kuendelea kuwa ni mahali ambapo hakuna mtu anayekosa mahitaji yake msingi, uhuru na haki jamii, changamoto ni kuhakikisha kwamba, sheria zilizopo zinatekelezwa kwa uaminifu mkubwa kwa kuheshimu na kuthamini utu wa wananchi wa Misri.

Misri inapaswa kusimama kidete kujenga na kuimarisha misingi ya haki na amani kwenye Ukanda wa Mashariki ya Kati, kwa ajili ya watu wanaoteseka kutokana na vita “isiyokuwa na kichwa wala miguu”. Baba Mtakatifu amewakumbuka wale wote waliosadaka maisha yao kwa ajili ya uzalendo kwa nchi yao kama Askari wa vikosi vya ulinzi na usalama, wahanga wa mashambulizi ya kigaidi; mauaji ya wakristo pamoja na kutambua dhamana na mchango mkubwa unaotolewa na wadau mbali mbali kwa ajili ya kuwasaidia wahanga na waathirika wa vitendo vyote hivi.

Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwaombea Wakristo waliouwawa kikatili hivi karibuni nchini Misri, ili Mwenyezi Mungu aweze kuganga na kuwaponya waliojeruhiwa na kutikiswa sana na mashambulizi haya. Lakini, ikumbukwe kwamba, watu wana kiu ya amani, ustawi na maendeleo ya kweli; wanahitaji kuona amani ikitawala kati yao; amani ambayo inapaswa kulindwa kwa nguvu zote kwa kuhakikisha kwamba, haki msingi, utu na heshima ya binadamu; usawa kwa wote, uhuru wa kuabudu na kujieleza vinakuzwa na kudumishwa kwa wananchi wote pasi na ubaguzi. Kuna haja ya kutoa kipaumbele cha pekee kwa dhamana na mchango wa wanawake na vijana, kwa huduma makini kwa wagonjwa na maskini.

Maendeleo ya kweli yanapimwa kwa huduma makini kwa binadamu hasa katika masuala ya elimu, afya, ustawi na maendeleo endelevu bila mtu awaye yote kutengwa. Kuna haja anasema Baba Mtakatifu ya kuondokana na Vita Kuu ya tatu ya Dunia inayopiganwa vipande vipande sehemu mbali mbali za dunia kutokana na misimamo mikali ya kidini. Vijana wa kizazi kipya wanapaswa kufundwa kuhusu umuhimu wa kulinda na kudumisha amani na kwamba, Mwenyezi Mungu anajitegemea na kujilinda mwenyewe hana sababu ya kulindwa na watu na wala hafurahii kifo cha mtu awaye yote, bali anawatakia waja wake furaha na maisha tele! Anafurahia kuona haki na amani vikitawala na kudumishwa; huruma, upendo, umoja na udugu vikidumishwa; amani na upatanisho vikiimarishwa; utu na heshima ya binadamu vikipewa msukumo wa pekee na waamini wakishuhudia imani inayomwilishwa katika matendo mema!

Baba Mtakatifu anasema, Jamii inahitaji vyombo na wajenzi wa amani, watu wanaoweza kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa jirani zao; watu wanaojikita katika huruma, upendo na udugu ili kusitisha kabisa vitendo vya kigaidi vinavyosababisha maafa makubwa kwa watu na mali. Imani kwa Mungu na uzalendo kwa nchi yao ni mambo muhimu sana katika kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini. Itakumbukwa kwamba, Msiri miaka 70 iliyopita ilikuwa ni nchi ya kwanza ya Kiarabu kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Vatican ili kudumisha urafiki na ushirikiano na kwamba, kuna haja ya kuendelea kuimarisha misingi hii kwa ajili ya mafao ya wengi. Baba Mtakatifu ameombea amani kwa Misri na  majirani zake wote pamoja na watu wote wenye mapenzi mema. Ameikumbuka na kuitakia mema familia yote ya Mungu nchini Misri na kuitaka kujenga na kuimarisha umoja, upendo na mshikamano wa dhati; kwa kukuza: usalama, amani na maridhiano kati yao. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewaombea wote amani, ustawi, maendeleo na haki.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.